Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-04 17:47:10    
Duru jipya la mazungumzo ya pande sita kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea lakaribia kuanza

cri

Tarehe 3 msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Kong Quan alitangaza kuwa duru la tano la mazungumzo ya pande sita kuhusu suala la nyuklia la Peninsula ya Korea litaanza tarehe 9.

Ili kuandaa duru hili la tano la mazungumzo, katika muda wa zaidi ya mwezi mmoja uliopita, China iliwasiliana sana na pande nyingine tano. Inasemekana kwamba baada ya duru la nne la mazungumzo balozi anayeshughulikia mambo ya peninsula ya Korea katika wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Li Bin alifanya ziara katika nchi za Korea ya Kaskazini, Marekani na Korea ya Kusini, na kujadiliana na nchi hizo kuhusu maandalizi ya duru jipya la mazungumzo. Jambo linalostahili kutajwa ni kuwa rais wa China na katibu mkuu wa chama Bw. Hu Jintao alifanya ziara nchini Korea ya Kaskazini mwishoni mwa mwezi Oktoba, na alibadilishana maoni na rais wa Korea ya Kaskazini Bw. Kim Jong Il kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea, pande mbili ziliona kuwa duru la nne la mazungumzo ya pande sita lilipata matokeo mazuri na zitatekeleza "taarifa ya pamoja" na kuendelea kufanya juhudi kwa lengo la kukomesha silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea. Korea ya Kaskazini imeahidi kushiriki kwenye duru la tano la mazungumzo ya pande sita. Juhudi za usuluhishi za China zimeyawekea msingi mazungumzo hayo.

Bw. Kong Quan alisema, muda wa mazungumzo hayo utaamuliwa na hali ya mazungumzo itakavyokuwa, China haijaweka muda maalumu wa mazungumzo. China inapendekeza kuwa mazungumzo yafanyike kwa vipindi. Bw. Kong Quan alisema, duru la tano la mazungumzo litajadili namna ya kutekeleza "taarifa ya pamoja" iliyotolewa katika duru la nne la mazungumzo. Alisema, China itashirikiana na pande nyingine kufanikisha mazungumzo hayo.

Wachambuzi wanaona kuwa pengine tofauti kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani kuhusu hatua za kufikia lengo la kuacha kabisa mpango wa silaha za nyuklia itakuwa tatizo kubwa katika mazungumzo hayo. Msemaji wa mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini tarehe 20 Septemba alitangaza kuwa Korea ya Kaskazini haitabomoa zana za nyuklia kabla ya Marekani haijaipatia kinu cha maji mepesi. Waziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini Bw. Choe Su Hon tarehe 22 Septemba kwenye mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa alizitaka pande zote za mazungumzo zifuate kanuni za "vitendo kwa vitendo" na kuipatia Korea ya Kaskazini kinu cha maji mepesi haraka iwezekanavyo. Lakini Marekani inaona kuwa ni lazima Korea ya Kaskazini iache kwanza mpango wa nyuklia na kujiunga tena na "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia" ndipo jumuiya ya kimataifa itakapofikiria kuisaidia kinu cha maji mepesi.

Kama waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alivyosema hapo kabla kwamba, misimamo ya pande husika bado inatofautiana, mazungumzo pengine yatakuwa na matatizo ya aina mbalimbali. Lakini kuweko kwa tofauti kati ya pande mbalimbali ni hali ya kawaida, kwa sababu kuna matatizo ndio maana mazungumzo yanahitajika. Hali nzuri iliyopo sasa ni kwamba "taarifa ya pamoja" iliyotolewa katika duru la nne la mazungumzo imeweka msingi wa mazungumzo ya baadaye. Kukutana tena hapa Beijing na kufanya mazungumzo kwa ajili ya kufikia lengo la kutokomeza silaha za nyuklia, ni maendeleo yanayostahili kupongezwa. Ukweli umedhihirishwa kuwa mazungumzo ni chaguo pekee lililo sahihi la kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea. Watu wanaweza kuamini kuwa iwapo pande zote zitashikilia msimamo wa kuzingatia hali ilivyo, kuheshimiana na kushauriana vya kutosha na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana, mazungumzo ya duru hilo jipya hakika yatatapa maendeleo mapya.