Wizara ya kilimo ya China tarehe 4 imetoa habari ikisema kuwa, homa ya mafua ya ndege imeibuka katika wilaya ya Heishan mkoani Liaoning, kaskazini mashariki ya China. Hivi sasa idara husika za China na serikali ya sehemu hiyo zinachukua hatua za kukabiliana na tukio la dharura.
Habari zilizotolewa na Wizara ya kilimo ya China zinasema kuwa, maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yaliyotokea katika wilaya ya Heishan mkoani Liaoning huenda yalitokana na ndege wanaohamahama kutokana na majira, maambukizi hayo yalienea katika baadhi ya familia zinazofuga kuku katika vijiji 6, ambapo kuku karibu elfu 9 wamekufa.
Mkurugenzi wa ofisi ya uongozi wa kazi ya kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege ya mkoa wa Liaoning Bwana Fu Jingwu akifahamisha hatua zinazochukuliwa na sehemu hiyo juu ya kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege alisema:
Kwanza tumeziwekea karantini sehemu zilizokumbwa na maradhi hayo, na kuanzisha vituo 30 vya muda vya ukaguzi na kunyunyizia dawa kwenye sehemu zilizo karibu na sehemu iliyokumbwa na maradhi. Pili tumetuma watu wengi kwenda kunyunyiza dawa za kuua vijidudu katika sehemu zilizokumbwa na maradhi, aidha tunawapigia chanjo kwa dharura kuku wanaofugwa.
Tokea majira ya mpukutiko yaingie, mbali na homa ya mafua ya ndege iliyotokea mkoani Liaoning, maradhi hayo pia yametokea katika sehemu tatu nyingine nchini China. Wizara ya kilimo ya China na serikali za mitaa zimechukua hatua za kukabiliana na matukio ya dharura, na kudhibiti kwa ufanisi maambuziki ya maradhi hayo. Hivi sasa katika sehemu zilizokumbwa na maradhi, hakuna mtu yeyote aliyeambukizwa homa ya mafua ya ndege.
Naibu waziri wa kilimo wa China Bwana Ying Chengjie anaona kuwa, hivi sasa hali ya kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege nchini China ni changamoto kubwa sana, akisema:
Nchini China zaidi ya asilimia 60 ya mifugo ya kuku imesambaa katika familia mbalimbali, hivyo kazi ya kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege ni ngumu sana; aidha nchini China mifugo ya bata maji ni mingi sana, ambayo inachukua asilimia 70 ya ile ya duniani. Mifugo ya bata maji ikiambukizwa virusi ni rahisi kuwaambukiza kuku; zaidi ya hayo njia 3 kati ya 8 za kuhamahama kwa ndege kutokana na majira ziko nchini China, hivyo kutokana na ongezeko la ndege wanaohamahama nchini China, hatari pia imeletwa kwa maambukizi ya maradhi.
Kutokana na hali hiyo, baraza la serikali la China hivi karibuni limeitisha mkutano wa kuweka mpango wa kuimarisha kazi ya kinga na udhibiti wa maradhi.
Wizara ya kilimo ya China hivi karibuni imetoa mpango wa kukabiliana na hali ya dharura ya homa ya mafua ya ndege na kuweka ngazi 4 za utoaji tahadhari za hali mbaya zaidi, mbaya, mbaya kidogo na hali mbaya ya kawaida.
Profesa wa chuo kikuu cha kilimo cha China Bwana Chen Fuyong alisema:
Kuweka ngazi 4 za tahadhari kutaoneshea hali wazi zaidi kuhusu maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, hii inasaidia kulinda shughuli za mifugo pia kuwasaidia watu kuongeza mawazo ya kujikinga na maradhi hayo.
Hivi sasa sehemu mbalimbali nchini China zinaimarisha kazi ya ukaguzi na ufuatiliaji wa maradhi ili kuchukua hatua kwa wakati.
|