Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-07 17:45:40    
Matembezi katika Makazi ya Kale Wilayani Yixian

cri

Mlima Huangshan unajulikana kwa watalii wa nchini na nje ya China. Karibu na mlima huo kuna wilaya moja inayoitwa Yixian, huko wilayani kuna makazi ya kale zaidi ya 3600 ambayo mpaka sasa bado yanahifadhiwa vizuri.

Jina la wilaya hiyo Yixian inatokana na jina la Mlima wa Huangshan, kwani zamani Mlima Huangshan uliitwa Mlima Yi. Katika mazingira yenye miti na mito, makazi hayo yanavutia sana kwa mapaa meusi na kuta nyeupe. Mwenyeji aliyezaliwa na kukulia huko Bw. Zhang Weifeng alisema kuwa, sababu ya makazi hayo kuwa yanahifadhiwa vizuri hadi leo, inatokana na mahali maalumu yalipo makazi hayo kijiografia. Alisema, "Wilayani kuna milima mingi, mawasiliano yalikuwa magumu sana katika historia, vita havikufikia hapa. Makazi haya ni mengi na hayapatikani katika mahali pengine."

Makazi hayo yalijengwa miaka 500 iliyopita, China ilipokuwa katika enzi za Ming na Qing. Makazi yalijengwa kwa ufundi mkubwa na mapambo ya kuvutia, na yanasifiwa kama ni makumbusho ya makazi ya enzi za Ming na Qing. Mwaka 2000 vijiji viwili vyenye makazi hayo viliorodheshwa na UNESCO katika kumbukumbu za urithi wa dunia. Kijiji kimoja kiitwacho Xidi kimekuwa na miaka zaidi ya 600, ingawa kimepita miaka mingi lakini makazi yake hayakuharibika. Makazi hayo yanapoangaliwa kutoka angani umbo la kijiji linaonekana kama meli, makazi zaidi ya 120 yanaonekana kama vijumba vya meli. Mwongozaji wa watalii Bi. Li Hua alieleza kuwa majengo katika kijiji hicho yalipangwa kwa makini sana, alisema, "Safu za makazi ni kama bodi la meli, na mashamba yaliyozunguka kijiji hicho yanakifanya kijiji hicho kiwe kama meli iliyotia nanga ndani ya ghuba."

Kati ya makazi, kuna jumba moja linalovutia zaidi, ambalo upenu wake unajitokeza nje na kuinuka kwenye kona, roshani inaonekana kama jukwaa la michezo. Inasemekana kwamba jumba hilo lilitumiwa na mabinti wa matajiri walipochagua waume zao kwa kurusha mpira wa rangi ya hariri. Katika mazingira ya muziki laini unapopigwa, msichana mmoja mwenye mavazi mekundu ya kale aliyeiga kama mtumishi wa tajiri alijitokeza jukwaani kwa hatua za taratibu, alifungua pazia la roshani. Baada ya msichana kuangalia hali ilivyo watu waliokuwa mbele ya jukwaa alirudi ndani, na baada ya muda alijitokeza mwingine aliyejipamba kama binti wa tajiri huku alikiziba uso kwa mkono mrefu wa nguo, huku akichungulia watu waliokuwa mbele ya jukwaa, kisha alitaka kutupa mpira lakini hakutupa, alitaka tena hakutupa tena, vivyo hivyo kwa mara kadhaa mwishowe alitupa mpira wake kwenye watu walio mbele ya jukwaa. Lakini aliyepata mpira huo hatakuwa mumewe bali atapigwa picha pamoja na bibi huyo.

Bila shaka hivi sasa watu hawatumii njia hiyo kuchagua ndoa yao, lakini inawafurahisha kwa kuwafahamisha watalii hali ilivyokuwa zamani katika mambo ya ndoa. Mwenyeji aliyetoka kutoka sehemu ya kaskazini ya China Bi. Wang Tao alisema, alikuwa kama kweli amerudishwa katika siku za kale. Alisema, "Ninapotembelea kati ya majengo hayo ya kale na kuangalia mchezo wa kuchagua bwana arusi naona kama kweli nimekuwa katika China ya kale." Kijiji kingine kinaitwa Hongcun, kiko umbali wa kilomita 20 hivi kutoka kijiji cha Xidi. Umbo la kijiji hicho linaonekana kama ng'ombe aliyelala ndani ya milima na mashamba ya mpunga. Ndani ya kijiji michirizi inapishana, wenyeji wengi wanaingiza maji hadi majumbani kwa mifereji.

Jumba la Chengzhitang ni jengo la fahari kabisa kati ya makazi kijijini. Jumba hilo lilikuwa makazi ya mfanyabiashara mkubwa wa chumvi. Jumba lenyewe lilijengwa kwa mbao, lakini kwa ndani lilijengwa kwa matofali na mawe likionekana la kifahari sana. Eneo la jumba hilo ni mita za mraba 3000. kitu kinachovutia zaidi ndani ya jumba hilo ni vinyago vyenye sura za watu wengi na kupakwa rangi ya dhahabu, watu wanasifu kuwa ni "kasri la kifalme" vijijini.

Ndani ya ukumbi wa mbele kuna milango miwili midogo kwenye pande mbili, na juu ya kila mlango limeandikwa neno "mfanyabiashara". Mwongozaji wa watalii alisema, "Katika zama za kale, biashara ilikuwa ni kazi ya kudharauliwa. Kutokana na kuzongwa na dhana hiyo, mwenye jumba alitumia ujanja huo wa kuandika neno hilo juu ya mlango, maana yeyote anayekuja lazima apite chini ya miguu ya mfanyabiashara hata akiwa anafanya kazi gani.

Katika karne ya 15 hadi 18, biashara ilikuwa inastawi sana katika sehemu hiyo. Watoto wa kiume walipotimiza umri wa miaka 15 hivi, karibu wote walitoka nje kufanya biashara. Katika kipindi hicho huko maduka yalikuwa mengi, biashara ilikuwa motomoto. Hata hivyo, kufanya biashara kulikuwa ni njia ya kujipatia riziki tu wala sio kwa ajili ya kujitajirisha, kazi waliyoiheshimu ilikuwa ya uofisa tu.

Watalii wanapotembelea huko wanapata huduma za malazi na chakula majumbani kwa wenyeji, gharama ni za chini sana.