Mkutano wa kinga na tiba ya homa ya mafua ya ndege duniani ulioitishwa na Shirika la afya duniani, Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, Shirika la afya za wanyama duniani na Benki ya dunia unafanyika huko Geneva kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 9 mwezi huu. Mkutano huo utajadili hali ilivyo ya sasa ya maambukizi ya homa ya mafua ya ndege duniani, namna ya kuzuia maradhi hayo yasiambukizwe kati ya watu na watu na namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na maradhi hayo.
Mkutano huo unahudhuriwa na maofisa wa serikali na wataalamu wa zaidi ya nchi 80, wajumbe wa jumuiya zinazohusika za kimataifa na makampuni maarufu duniani. Mkutano huo utafanyika chini ya hali ambayo, wagonjwa walioambukizwa homa ya mafua ya ndege wamegunduliwa mara kwa mara katika nchi kadhaa za Asia, virusi vya homa ya mafua ya ndege ambavyo vimeenea hadi kwenye nchi za Ulaya vikiendelea kuambukiza katika sehemu kadhaa za Asia na Ulaya, mpaka sasa ni bara la Afrika na bara la Ocenia tu ambayo bado hayajatoa ripoti kuhusu homa ya mafua ya ndege. Lakini kutokana na kuwadia kwa majira ya siku za baridi, ndege wanaohamahama kutoka na kubadilika kwa majira pia wanalifanya bara la Afrika likabiliwe na tishio la homa ya mafua ya ndege, na kidhahiri, bara la Afrika ni sehemu yenye uwezo dhaifu zaidi duniani katika kukabiliana na maradhi hayo.
Tarehe 4 Novemba, mkutano wa 7 wa mawaziri wa kilimo na mifugo wa Umoja wa Afrika kwa mara ya kwanza ulijadili suala la kukabiliana na homa ya mafua ya ndege. Mkutano huo unaona kuwa, kazi ya dharura ya nchi za Afrika kwa hivi sasa ni kuanzisha na kukamilisha kwa nguvu mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege. Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa linaona kuwa, hivi sasa jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi kuwa, kama nchi moja yoyote ya Afrika kusini mwa Sahara haina bajeti ya kutosha au haichukui hatua halisi, hali hii huenda italifanya bara zima la Afrika hata dunia nzima kushindwa katika juhudi zao za kupambana na homa ya mafua ya ndege, matokeo yake yataleta balaa kubwa. Benki ya dunia tarehe 4 ilitangaza kuwa itatenga dola za kimarekani milioni 300 hadi 500 kuzisaidia nchi maskini katika kuimarisha kazi zao za upimaji na ukaguzi wa maradhi ya mifugo, kutoa chanjo au kuteketeza mifugo. Namna ya kuzisaidia nchi maskini za Afrika na sehemu nyingine duniani kupata fedha za kinga na kutibu homa ya mafua ya ndege, litakuwa suala muhimu litakalojadiliwa kwenye mkutano huo.
Kwenye mkutano huo, suala lingine kubwa kuhusu namna ya kutumia fedha katika kazi muhimu yenye ufanisi wa kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege pia litajadiliwa. Katibu mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa Bwana Jacques Diouf aliainisha hivi karibuni kuwa, kazi ya kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege inapaswa kufanyika kuanzia udhibiti wa maambukizi ya maradhi hayo kati ya mifugo, kwani maradhi hayo ni maradhi ya wanyama na mifugo. Hivi sasa jumuiya ya kimataifa inafuatilia zaidi athari ya maradhi hayo kwa afya za binadamu, na haitilii maanani zaidi kuhusu utaratibu usiokamilika kuhusu huduma za tiba kwa mifugo katika nchi nyingi maskini.
Hivi sasa hali ya kukosa uratibu imekuwepo katika utafiti na utengenezaji wa dawa na chanjo za kupambana na virusi vya homa ya mafua ya ndege duniani kote, hili litakuwa suala la tatu litakalojadiliwa kwenye mkutano huo.
Kutokana na kukabiliwa na maambukizi ya maradhi ambayo huenda yatatokea duniani kote, nchi mbalimbali duniani zinapaswa kusaidiana na kuungana mkono, ndipo mwishowe zitakapoweza kuishinda homa ya mafua ya ndege.
Idhaa ya Kiswahili 2005-11-07
|