China na Marekani tarehe 8 huko mjini London zilisaini "Kumbukumbu ya maelewano kuhusu biashara ya nguo". Katika kumbukumbu hiyo pande hizo mbili zimefikia makubaliano kuwa katika miaka 3 ijayo, ongezeko kwa aina 21 za bidhaa za nguo za China zinazosafirishwa kwenda Marekani lidhibitiwe kati ya 10% na 17% kwa mwaka. Wataalamu wa uchumi na wataalamu wa sekta ya nguo nchini China wanapongeza matokeo hayo na kuona kuwa hatua hiyo itaweka mazingira ya utulivu kwa sekta ya nguo kwa nchi hizo mbili.
Tarehe 8, waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai na mwakilishi wa Marekani kuhusu biashara Bw. Rob Portman wakiziwakilisha serikali zao walisaini kumbukumbu hiyo, ambapo mgogoro uliodumu kwa siku nyingi kati ya China na Marekani kuhusu biashara ya nguo ulimalizika.
Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai anaona kuwa kumbukumbu iliyosainiwa na China na Marekani kuhusu biashara ya nguo ni mkataba wa kunufaisha pande hizo mbili, lakini alisema kuwa nchi zilizoendelea zinatakiwa kufahamu kuwa utandawazi wa biashara ya nguo ni mwelekeo usiozuilika, na si mwafaka kuweka kikomo cha bidhaa katika biashara ya nguo. Mwakilishi wa Marekani Bw. Rob Portman baada ya kusaini kumbukumbu hiyo alisema kuwa, China na Marekani kufikia makubaliano kuhusu suala la mgogoro wa biashara ya nguo inaonesha kuwa pande hizo mbili zina uwezo wa kutatua mgogoro wa biashara, jambo ambalo pia linainufaisha Marekani kuongeza idadi ya wafanyakazi katika sekta zinazohusika na sekta ya nguo.
China na Marekani zote zimeonesha kufurahia kusainiwa kwa kumbukumbu ya maelewano kuhusu biashara ya nguo. Lakini mtafiti wa idara ya uchumi na siasa ya dunia ya taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bw. Song Hong alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema kuwa, kusainiwa kwa makubaliano hayo kunatokana na pande hizo mbili kulegeza masharti yao:
"Marekani imelegeza masharti yake kuhusu kiwango cha ongezeko hadi kufikia 17% kwa mwaka ikilinganishwa na kile ilichoshikilia hapo awali cha ongezeko la 7.5% kwa mwaka. China pia imelegeza msimamo wake katika kipindi cha udhibiti ambacho ni kufikia mwaka 2008 badala ya mwaka 2007 cha hapo awali. China pia imefanya suluhu kuhusu idadi ya bidhaa za nguo zinazodhibitiwa. Hapo awali China ilitaka kuwekewa kikomo kwa aina 10 tu za bidhaa za nguo. Hali halisi ni kuwa pande zote mbili zimelegeza masharti yao, na zinalingana."
Habari zinasema kuwa kumbukumbu hiyo iliyosainiwa na China na Marekani hivi karibuni, itaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2006 na kuishia tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2008. Katika kipindi hicho China na Marekani zimekubali kufanya udhibiti kuhusu aina 21 za bidhaa za nguo zikiwemo za suruali, mashati na sidiria, ambazo ongezeko lake linatakiwa kuwa kati ya 10% na 17%. Idadi ya nguo ya kuanzia ni ile ya nguo za China zilizosafirishwa nchini Marekani mwaka 2005, na idadi za nguo za kuanzia katika mwaka 2007 na mwaka 2008 ni idadi ambayo China na Marekani zilikubaliana katika mwaka uliotangulia.
Tangu kuondolewa kiwango cha udhibiti kuhusu biashara ya nguo kati ya nchi wanachama wa WTO tarehe 1 mwezi Januari mwaka huu, Marekani ilidhibiti idadi ya nguo zinazosafirishwa nchini mwake kutoka China kwa kisingizio cha soko lake la nguo kuvurugwa na ongezeko kubwa la bidhaa za nguo za China, hivyo ukazuka mgogoro wa bidhaa ya nguo kati ya China na Marekani na kuleta kivuli kwa biashara kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya kufikia makubaliano kuhusu biashara ya nguo kati ya China na Marekani, maofisa wa sekta ya nguo ya China walieleza furaha yao, msemaji wa jumuiya ya viwanda vya nguo ya China Bw. Sun Huaibin alisema,
"Ingawa udhibiti huo umethibitishwa na mapatano ya pande hizo mbili, lakini mustakabali na mazingira ya utulivu ya biashara ni dhahiri. Matokeo hayo ni bora zaidi kuliko Marekani kujiamulia kuweka vizuizi maalumu dhidi ya bidhaa za nguo kutoka China."
Bw. Sun aliongeza kuwa ingawa China imekubaliana na nchi za Ulaya na Marekani kwa nyakati tofauti, lakini ni vigumu kusema kuwa mgogoro wa biashara wa namna hiyo hauwezi kutokea tena.
|