Milipuko mitatu ya kujiua ilitokea kwenye hoteli tatu huko Amman, mji mkuu wa Jordan, tarehe saa mbili na dakika 50 usiku saa za huko. Msemaji wa serikali ya Jordan ambaye pia ni naibu waziri mkuu Bw. Marwan Musaher alithibitisha usiku huo kuwa milipuko hiyo imewaua watu wasiopungua 67 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 300. Hii ni milipuko mikubwa kabisa ya kigaidi kutokea nchini Jordan.
Ubalozi wa China nchini Jordan umethibitisha kuwa hoteli ambayo ujumbe wa kijeshi wa China umefikia ukiwa katika ziara mjini Amman pia ulishambuliwa kwa mabomu, ambapo watu wawili wa ujumbe huo walikufa, wengine wawili walijeruhiwa akiwemo mmoja aliyejeruhiwa vibaya.
Mlipuko ulitokea kwanza kwenye hoteli ya Grand Hyatt iliyoko katikati ya mji huo. Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa mabomu yalilipuka kwenye ukumbi wa hoteli hiyo. Dakika kadhaa baada ya kutokea kwa mlipuko huo, mlipuko mwingine pia ulitokea kwenye hoteli ya Radisson Sas iliyoko kwenye mtaa wa Hussein. Polisi wa Jordan alisema kuwa mlipuko huo ulitokea kwenye ukumbi ambako harusi ilikuwa ikifanyika, watu wasiopungua watano walikufa papo hapo. Polisi huyo alisema kuwa mlipuko wa tatu ulitokea kwenye hoteli ya Days In, ambapo gari dogo lililokuwa limebeba baruti lilijaribu kukaribia hoteli hiyo, lakini baada ya kuzuiliwa na vizuizi, mlipuaji alilipua baruti nje ya hoteli hiyo na kusababisha vifo na majeruhi.
Ni dhahiri kuwa milipuko mitatu hiyo ilifanywa dhidi ya wageni walioko kwenye hoteli hizo. Hadi hivi sasa, hakuna mtu au jumuiya iliyotangaza kuhusika na milipuko hiyo. Lakini msemaji wa serikali ya Jordan Bw. Manwan Musaher alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa kundi la Al Qaeda la Iraq linaloongozwa na Al Zarqawi linahusika na milipuko hiyo mitatu.
Baada ya kutokea milipuko hiyo tarehe 9 usiku, mfalme Abdullah wa pili wa Jordan aliamua mara moja kukatisha ziara yake nchini Kazakhstan na kurudi nyumbani. Alitoa taarifa usiku huo akilaani vikali milipuko hiyo mitatu ya kujiua. Alisema kuwa kuwashambulia watu wasio na hatia ni kitendo kinachofanywa na waoga na waliofanya mashambulizi hayo lazima waadhibiwe kisheria nguvuni. Wakati huo huo, polisi wa Jordan waliimarisha ulinzi mjini Amman, hasa kwenye balozi za nchi za nje na hoteli kubwa. Zaidi ya hayo, serikali ya Jordan ilitangaza kuwa tarehe 10 ni siku ya mapumziko ya taifa, ili serikali inaweza kuchukua hatua imara za ulinzi.
Wakati huo huo, jumuiya ya kimataifa ilifululiza kulaani milipuko iliyotokea mjini Amman. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliyekuwa akiwa katika ziara huko Mashariki ya Kati tarehe 9 alitoa taarifa kupitia msemaji wake, akitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za pamoja kupambana na ugaidi. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Bw. Scott McClellan siku hiyo alitoa taarifa akieleza kuwa Jordan ni rafiki mkubwa wa Marekani na Marekani inapenda kushirikiana na Jordan kuchunguza tukio hilo, ili kuwaadhibu kisheria wahusika wa tukio hilo.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-10
|