Baada ya kufanya majadiliano kwa siku 3, wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 80 walioshiriki kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu suala la homa ya mafua ya ndege huko Geneva, tarehe 9 walipitisha mpango wa utekelezaji wa dunia wa kukabiliana na homa ya mafua ya ndege.
Mpango huo unapanga shughuli za udhibiti wa homa ya mafua ya ndege katika hatua 5 zikiwa ni pamoja na kabla ya kuenea kwa virusi vya homa ya mafua ya ndege, wakati virusi vyake vinayakumba maeneo makubwa na kuambukizwa duniani, na kutaka kuikinga na kuidhibiti katika pande 5 zikiwa ni pamoja na "Kupunguza uwezekano wa kuambukizwa kwa binadamu", "Kuimarisha mfumo wa tahadhari", "Kudhibiti kutoka chanzo au kuchelewesha maambukizi yake", "Kupunguza idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa aina hiyo, vifo na uharibifu dhidi ya jamii" na "Kuanzisha utafiti ili kuelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa."
Mpango unaona kuwa katika miezi 6 ijayo, kipaumbele kingetolewa katika baadhi ya nchi za Asia ya kusini mashariki, hususan kwenye mashamba ya ufugaji kuku na mabata ya Indonesia na Vietnam, ili kuzuia kulipuka kwa ugonjwa huo miongoni mwa wanyama na kupunguza uwezekano wa virusi vya homa ya mafua ya ndege kuambukizwa kwa wingi kwa binadamu. Katika miaka 3 ijayo, mkazo wa shughuli za udhibiti unatakiwa kuwekwa katika uanzishaji wa mfumo wa upimaji kuhusu virusi vya homa ya mafua ya ndege kuambukiza kuku na binadamu. Mpango unaona kuwa utekelezaji wake unahitaji dola za kimarekani bilioni 1.
Katika mkutano huo washiriki walikuwa na maoni mengi yanayofanana, wanaona kuwa haifai kuhaingaika sana au kuipuuza, wanaona kuwa hivi sasa ni kipindi ambacho maambukizi ya virusi vya homa ya ndege yanakaribia wakati wa kulipuka katika maeneo mengi zaidi tokea mwaka 1968, na kumekuwa na mazingira ya kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo, isipokuwa tu yamekosa njia ya kuleta maambukizi miongoni mwa binadamu. Hivi sasa, virusi hivyo vinaambukizwa kwa kuku na mabata, lakini havijaambukizwa kwa watu wengi, endapo hatua mwafaka zitachukuliwa, maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yanaweza kuzuiliwa au kudhibitiwa, hivyo watu hawana haja ya kuhangaika.
Washiriki wa mkutano wanaona kuwa shida kubwa na changamoto inayoikabili kazi ya udhibiti ni namna ya kuzisaidia nchi maskini kuchukua hatua ipasavyo na kujenga mfumo wa dharura unaoaminika. Hivi sasa nchi tajiri zimejiandaa ipasavyo, lakini nchi zile zinazokumbwa na maambukizi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege na zenye uwezekano mkubwa wa kulipuka maambukizi makubwa, ziko nyuma sana ikilinganishwa na nchi matajiri, ambapo bara la Afrika ni moja ya sehemu dhaifu duniani.
Kwenye upande wa hali ya kuweka akiba dawa za kupambana na virusi vya homa ya mafua ya ndege ni vivyo hivyo. "Tami flu" ni dawa pekee iliyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani, WHO ya kuwa na ufanisi katika tiba ya wagonjwa wa aina hiyo. Lakini nchi zilizoweka akiba kwa wingi ya dawa hiyo karibu zote ni nchi zilizoendelea, wakati nchi zenye maambukizi makubwa ya virusi hivyo bado hazijajiandaa ipasavyo kutokana na matatizo ya kiuchumi au sababu nyingine.
Sehemu zilizokumbwa na maambukizi mengi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege katika nchi zinazoendelea hasa ni katika sehemu za vijiji, ambapo ni zenye hali dhaifu zaidi katika upimaji, udhibiti na tiba za wagonjwa wanaoambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege. Hivyo Shirika la Afya ya Wanyama Duniani linataka kuanzisha shirika la utoaji msaada kuhusu afya ya wanyama kwa kuanzisha mfumo wa upimaji na matibabu. Kwa upande mwingine endapo nchi zenye maambukizi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege za zinazoendelea zikishindwa kutoa fidia ya kutosha kwa familia za wakulima wanaochinja kuku na mabata, basi familia hizo hazitakuwa na motisha wa kuripoti hali ya maambukizi. Lakini kinga na udhibiti wa maambukizi ya virusi unatakiwa kufanywa kwa haraka, endapo ukicheleweshwa na kutotumia fursa nzuri ya kuyazuia maambukizi, shida ya kuyazuia maambukizi ya virusi itaongezeka kwa haraka sana. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani unaonesha kuwa hivi sasa kuna nchi 120 ambazo bado hazijatenga fedha kwa ajili ya fidia.
Taarifa ya utafiti iliyotolewa na shirika husika la Umoja wa Mataifa inasema kuwa, uzoefu wa zamani unaonesha kuwa fedha zinazotumika katika udhibiti ni kidogo sana ikilinganishwa na hasara zinazoletwa na maambukizi makubwa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-11-10
|