Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-11 19:42:42    
Urafiki kati ya China na Afrika aliousikia mwanadiplomasia wa China

cri

Jamhuri ya Watu wa China ilirejeshwa haki zote halali kwenye Umoja wa Mataifa tarehe 25, Oktoba, mwaka 1971. Ingawa ushindi huo ulitokana na sababu mbalimbali, lakini nchi nyingi za Afrika zilizoshikilia kulinda kanuni ya Katiba ya Umoja wa Mataifa zilitoa uungaji mkono mkubwa kwa China. Kama hayati mwenyekiti Mao Zedong wa China alivyosema, ni marafiki wa Afrika waliosaidia China irudi kwenye Umoja wa Mataifa.

Kabla ya ujumbe wa China kuhudhuria kwa mara ya kwanza Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwenyekiti wa China wa wakati huo Mao Zedong na waziri mkuu Zhou Enlai waliuagiza ujumbe huo kutoa shukrani kwa nchi zote za Afrika zilizoisaidia China baada ya kufika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York. Akiwa mjumbe wa ujumbe huo, Bw. Wu Miaofa, ambaye sasa ni mtaalamu wa Taasisi ya masuala ya Kimataifa ya China anayeshughulikia suala la Umoja wa Mataifa, alishuhudia shughuli za kurejeshwa kwa China katika Umoja wa Mataifa, na kuhisi urafiki mkubwa wa nchi za Afrika kwa China.

Bw. Wu alieleza kuwa, wakati huo Bw. Salim Ahmed Salim aliyekuwa mjumbe wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa alikuwa ameishi nchini China kwa miaka kadhaa kama balozi wa Tanzania nchini China. Akizungumzia kazi yake nchini China Bw. Salim alisema kuwa, maneno ya mwenyekiti Mao Zedong wa wakati huo yalimwachia kumbukumbu kubwa. Mwenyekiti Mao Zedong aliwahi kumwambia kuwa, si jambo rahisi kwa mtu kijana kuwa balozi kwa umri kama aliokuwa nao Bw. Salim. Pia alisema aliamini kuwa wanadiplomasia wa nchi za Afrika watafanya kazi vizuri zaidi kuliko wale wa nchi za magharibi. Bw. Salim alisema maneno hayo ya Mao Zedong yalikuwa yakimtia moyo katika maisha yake. Kutokana na uhodari wake mkubwa Bw. Salim alishika wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati maalum ya kuondoa ukoloni kwa miaka 11. Bw. Salim alisema, daima hataacha kuunga mkono kurejeshwa kwa haki zote halali za China katika Umoja wa Mataifa akiwa anafanya kazi katika Umoja wa Mataifa, na hakuona masikitiko yoyote baada ya matumaini yake hayo kutimizwa.

Balozi mdogo wa Zambia wa wakati huo nchini China Bw. Zimba alisema kuwa, jambo moja lililomtia moyo sana ni kuwa: Ingawa wakati huo China haikuwa na fedha nyingi za kigeni, lakini serikali ya China ilitoa mkopo kuzisaidia Tanzania na Zambia kujenga Reli ya TAZARA. Kwa upande mwingine, nchi za magharibi zilikataa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Misimamo tofauti kati ya China na nchi za magharibi iliwafanya watu wa Afrika wafahamu China ndiyo rafiki ya kutegemeka. Katika ujenzi wa reli hiyo, wataalamu wengi wa China walijitoa mhanga, na Zambia iliwajengea Makaburi ya Mashujaa. Bw. Zimba alisema kuwa alikwenda kwenye makaburi hayo mara kwa mara na kutoa rambirambi kwa mashujaa hao wa China. Kila mara aliona maua mengi mabichi yaliyowekwa mbele ya makaburi hayo, hii inaonesha kuwa, urafiki mkubwa kati ya Zambia na umetia mzizi mioyoni mwa watu wa Zambia.

Bw. Miganage aliyekuwa mjumbe wa kudumu wa Burundi wa wakati huo kwenye Umoja wa Mataifa alisema kuwa, alikuwa akisifu sana sera za China za kutatua suala la makabila madogomadogo. Aliona kuwa, ni sera ya busara kwa serikali ya China kuyachukulia kwa usawa makabila yote madogomadogo. Bw. Minganage aliamua kufanya utafiti wa kina juu ya sera kuhusu makabila madogomadogoChina, na kutoa ripoti kwa serikali yake, ili kutatua tatizo la ukabila la nchi yake yenyewe.

Kiongozi wa Chama SWAPO cha Namibia wa wakati huo Bw. Sam Nujoma na kiongozi wa chama cha ZANU PF cha Zimbabwe Bw. Robert Mugabe walifurahi na kusisimka sana baada ya kurejeshwa kwa haki zote halali za China kwenye Umoja wa Mataifa. Wakitambua kuwa Bw. Wu Maofa alitoka ujumbe wa China walimkumbatiana na kusema kwa furaha, "Wachina wamekuja, marafiki zetu wa China wamekuja!" Viongozi hao wawili walizungumzia ripoti za waandishi wa habari wa Marekani kuhusu vituo vya mapinduzi vya China. Bw. Nujoma alisema kuwa, nia thabiti ya viongozi wa mapinduzi wa China ilimwachia kumbukumbu kubwa, na vitendo vyao vilikuwa vikimhimiza ashughulikie mapambano ya watu wa Namibia kujipatia uhuru. Bw. Mugabe alisema, kuanzia wakati huo alikuwa anaamini kuwa, China mpya itaruka juu na mbele zaidi kama mwewe wa Afrika, na kuleta matumaini kwa watu wa Afrika.

Miaka 34 imepita tangu China irejeshwe kwenye Umoja wa Mataifa. Ingawa hali ya kimataifa imekuwa na mabadiliko makubwa, lakini urafiki kati ya watu wa China na Afrika wenye lengo moja hautabadilika hata kidogo, badala yake utazidi kuimarishwa siku hadi siku.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-11