Serikali ya Jordan tarehe 13 ilithibitisha kuwa milipuko iliyotokea tarehe 9 usiku mjini Amman ilifanywa na wanachama wanne wa Jihad wa kundi la Al-Qaeda wenye pasipoti za Iraq. Jambo hilo linatia wasiwasi kuwa uhusiano kati ya Jordan na Iraq utaathiriwa na milipuko hiyo.
Naibu waziri mkuu wa Jordan ambaye pia ni msemaji wa serikali Bw. Marwan Muasher, alithibitisha kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 13 mjini Amman kuwa, serikali ya Jordan imethibitisha uraia wa washambulizi wanne waliofanya milipuko hiyo, ambao wote ni wanachama wa Jihad wa kundi la Al-Qaeda. Washambulizi hao ni Ali Hussein Al-Shamari, Rawad Jassen Mohammed Abed, Safaa Muhamme Ali na mke wa Shamari waliokufa kwenye milipuko hiyo ya kujiua, pamoja na mwanamke Sajida Mubarak Atrous Al-Rishawi aliyeshindwa kulipua mabomu aliyoyafunga ubavuni mwake. Msemaji huyo amesema washambulizi hao wanne waliokuwa na pasipoti ya Iraq waliingia nchini Jordan tarehe 5 kutoka Iraq na kukaa kwenye nyumba moja iliyoko sehemu ya magharibi ya mji wa Amman. Tarehe 9 waliondoka nyumbani humo na kwenda mahali pa kuanzisha mashambulizi. Sajida Al-Rishawi aliyejipenyeza kwenye Radisson SAS Hotel alishindwa kulipua mabomu yaliyofungwa ubavuni mwake na kuondoka katika hoteli hiyo kutokana na maagizo ya Ali Al-Shamari, baadaye Ali Al-Shamari alifanya mlipuko wa kujiua. Sasa Sajida Al-Rishawi amekamatwa na idara ya usalama ya Jordan na kukiri kushiriki kwenye mashambulizi hayo.
Sajida Al-Rishawi pia ni dada mdogo wa Samer Mubarak Al-Rishawi ambaye ni msaidizi wa Al Zarqawi, kiongozi wa tawi la Iraq la kundi la Al-Qaeda. Samer Mubarak Al-Rishawi alipigwa risasi na jeshi la Marekani na kufa mjini Fallujah, Iraq. Jambo lililothibitishwa ni kuwa hakuna raia wa Jordan kati ya washambulizi hao. Tukio la milipuko mikubwa iliyofanywa na Wairaq mjini Amman lilitokea wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili unakuwa mbaya. Katika kipindi cha utawala wa Saddam Hussein, Jordan iliwahi kuwa rafiki mkubwa wa Iraq. Lakini katika vita vya Iraq, Jordan iliiruhusu Marekani itumie ardhi yake kuishambulia Iraq, jambo hilo liliwaghadhabisha Wasunni wa Iraq. Baada ya vita vya Iraq, Jordan aliwahifadhi mabinti wawili wa Saddam na kusababisha malalamiko kutoka kwa Washia na Wakurd wa Iraq. Ubalozi wa Jordan nchini Iraq ulishambuliwa mara nyingi kutokana na jambo hilo. Katika vita vya Iraq, idadi kubwa ya matajiri wa Iraq walimiminikia nchini Jordan ili kujiepusha na vita. Habari zinasema kuwa Wairaq laki nne wanakaa nchini Jordan na kufanya maisha ya watu milioni tano wa nchi hiyo kuwa mabaya.
Katika hali hiyo, magaidi ya kundi la Al-Qaeda walipanua mashambulizi yao nchini Jordan kutoka nchini Iraq. Hata hivyo msemaji Muasher wa serikali ya Jordan alieleza kuwa Jordan inaheshimu mamlaka ya Iraq na haitapeleka askari nchini Iraq kuwasaka magaidi wanaohusika na milipuko ya Amman. Ingawa milipuko hiyo imewachochea Wajordan kuwafukuza Wairaq kutoka Jordan, lakini watu wanatumai kuwa pande mbili Jordan na Iraq zitachukua tahadhari kukabiliana na hali iliyoletwa na mashambulizi hayo katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-14
|