Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-14 17:58:00    
Mkahawa wa Makye Ame katika Mji wa Lhasa

cri

Katika mji wa Lhasa, mji mkuu wa Mkoa wa Tibet uliopo kwenye uwanda wa juu wa mita 3600 kutoka usawa wa bahari, kuna jumba moja dogo la ghorofa kwenye barabara ya Bajiao. Jumba hilo limepakwa rangi ya njano na kulifanya livutie kati ya majengo yote yenye rangi nyeupe kwenye barabara hiyo. Hili ni jumba la mkahawa unaoitwa Makye Ame. Jina la mkahawa huo "Makye Ame" linatokana na beti moja ya shairi ambalo linajulikana kwa Watibet wote.

Siku moja alasiri, pamoja na watalii wengi tulitembea kwenye barabara ya Bajiao iliyotandazwa kwa mawe. Kelele za wachuuzi, watalii wa nchi mbalimbali, wenyeji na majumba meupe yaliyoko kando ya barabara.... inaifanya barabara hiyo ijulikane mjini Lhasa.

Tulifuatana na watalii wengi na kuangalia huku na huko, jumba moja la manjano lilivutia macho yetu. Hilo ni jumba la mkahawa wa Makye Ame. Mkahawa huo umekuwepo kwa miaka minane. Rangi ya jumba hilo ni tofauti na majumba yote mengine, kwa nini? Meneja wa mkahawa huo Bw. Chungkyi Nyima alitusimulia hadithi moja iliyosimuliwa kwa miaka mingi.

"Mkoani Tibet rangi ya manjano inamaanisha utukufu, kwa hiyo mahekalu na makazi ya masufii wazee hupakwa rangi ya manjano, lakini kwa nini jumba hilo la mkahawa limepakwa rangi hiyo? Sababu ni hadithi moja iliyotokea katika jumba hilo miaka mingi iliyopita."

Miaka 300 iliyopita, kiongozi wa dini ya Buddha mkoani Tibet Dalai Lama wa sita, alimkuta msichana mmoja mrembo mahali ambapo jumba hilo lipo, baadaye huyo Dalai Lama mara kwa mara alifika huko akitamani kumkuta tena lakini hakumwona. Kwa masikitiko aliandika shairi lake: Kila mwezi angavu unapojitokeza kutoka nyuma ya mlima, hunikumbusha msichana Makye Ame.

Tulipokuwa ndani ya mkahawa huo tuligundua mwangaza wa jua ulikuwa umepenya ndani kupitia shashi dirishani, mara ukakumbusha hadithi ya Dalai Lama wa sita iliyotokea miaka 300 iliyopita. Meneja wa mkahawa alituambia kisa cha kweli kilichotokea katika mkahawa wake.

"Mwezi Oktoba mwaka 1998, watalii wawili wa Ujerumani wambao walikuwa hawafahamiani, walikutana katika mkahawa wangu, na kisha walikwenda kutalii kwa pamoja, baadaye hao wawili walikuwa wapenzi. Mwaka 2000 walikuja tena na mtoto wao kwenye mkahawa wangu. Jambo hilo linanifurahisha sana."

Watu waliofika huko mkahawani hukumbuka hadithi yao au husimulia hadithi zao walizopata katika mkahawa huo. Huko watu wanaweza kuandika hadithi zao kwenye kitabu cha kuacha ujumbe. Ndani ya kitabu hicho, watalii wameandika hisia zao na mambo yao mengi kwa lugha mbalimbali.

Mkahawa wa Makye Ame ni mahali pa kuwakutanisha wapenzi, ni mahali pa kupumzisha akili kwa starehe na kuufurahia utamaduni wa Kitibet. Jumba lilipambwa kwa utamaduni wa Kitibet. Ndani ya ukumbi picha ya Buddha ilitundikwa ukutani, rangi ya ukuta inalingana na rangi ya nje ya jumba hilo, picha za siku za zamani na za sasa zilizotundikwa ukutani zinaonesha wazi mabadiliko ya Tibet, kaunta ya baa iliyotengenezwa na kwa chongwa kwa sanaa ya Kitibet inachangia kuonesha utamaduni huo.

Utamaduni ndani ya jumba hilo uliufanya mkahawa huo uwe tofauti na mikahawa yote mingine, umekuwa kama ni dirisha la kuwafahamisha utamaduni wa Kitibet wenyeji, watalii wa nchini na wa nchi za nje. Bw. Zhang Jian ni mwenyeji wa Tibet, alituambia kuwa katika mkahawa wa Makye Ame watu wanaweza kufahamu mambo mengi ya utamaduni wa Kitibet. Alisema,

"Unapokuwa hapa sio tu unaweza kuhisi utamaduni wa kabila la Watibet, bali pia unaweza kuelewa mambo mengi ya historia ya utamaduni na maendeleo yake."

Mtalii kutoka Italia Bi. Tracy July alivutiwa sana na utamaduni wa jumba hilo. Alisema,

"Najisikia raha nikiwa hapa. Sisikii njaa, lakini napenda kukaa kidogo nipate furaha nisiyoweza kuipata katika mikahawa mingine."

Kama ilivyo kwa Bi. Tracy July, watalii wengi wanapopita huko hawakosi kuingia, wakakaa karibu na dirisha wakiangalia watu wakipita na huku wakinywa kahawa na chai au mtindi katika mazingira yenye harufu nzito ya utamaduni wa Kitibet.