Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-15 16:15:21    
Nini kitazungumzwa zaidi kwenye mkutano wa viongozi wa APEC ?

cri

Mkutano wa 17 wa mawaziri wa APEC unafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 16 mjini Busan nchini Korea ya Kusini, huu ni mkutano wa maandalizi ya mkutano usio rasmi wa viogozi wa APEC utakaofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 19 katika mji huo. Kutokana na jinsi mkutano huo unavyokaribia, nini kitakachozungumzwa kwenye mkutano huo wa viongozi kinafuatiliwa zaidi.

Kutokana na maelezo ya Korea ya Kusini, mada ya mkutano huo ni "Kwenda kwenye familia moja, kukabiliana na changamoto na kufuatilia mageuzi". Wakati wa mkutano, viongozi watafanya mkutano mkuu mara mbili, mada ya mkutano wa kwanza ni "mchakato wa biashara huria", kwenye mkutano huo watatathmini mazungumzo ya Doha ya WTO yaani DDA, "lengo la Bogor" lililowekwa mwaka 1994 kwenye mkutano usio rasmi wa viongozi wa APEC uliofanyika nchini Indonesia, kujadili biashara ya kikanda na makubaliano ya biashara huria, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupunguza tofauti kati ya matajiri na maskini. Mada ya mkutano wa pili ni "Kanda ya Asia na Pasifiki Yenye Usalama na Uwazi", viongozi watabadilishana maoni kuhusu namna ya kuimarisha ushirkiano katika mapambano dhidi ya ugaidi, kupambana kwa pamoja na magonjwa ya kuambukiza, madhara ya maafa ya kimaumbile, usalama wa nishati na mapambano dhidi ya ufisadi. Mkutano utamalizika kwa kutoa "Taarifa ya Busan" na taarifa maalumu ya kusukuma mazungumzo ya Doha.

Mkutano huo usio rasmi wa viongozi wa APEC unafanyika katika mazingira ya mtandao wa uchumi duniani na ushirikiano wa kikanda. Hivi sasa mazungumzo ya Doha yaekwama bila kupiga hatua yoyote, na mkutano wa mawaziri wa WTO utakaofanyika mwezi ujao huko Hong Kong pia hautakuwa na matumai yoyote. Huu ni mwaka wa kutathmini "lengo la Bogor" lililowekwa na mkutano wa APEC uliofanyika mwaka 1994. pamoja na yote hayo, mkutano huo wa viongozi wa APEC unakabiliwa na changamoto mpya katika masuala ya usalama wa binadamu na wa nishati. Yote hayo yanaathiri moja kwa moja mwelekeo na maendeleo ya uchumi wa nchi za APEC. Kwa hiyo, kitu kitakachozungumzwa zaidi katika mkutano huo kitakuwa ni kutathmini "lengo la Bogor", kusukuma mzungumzo ya Doha, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya homa ya mafua ya ndege, ugaidi na ufisadi.

"Lengo la Bogor" limeweka wazi ratiba ya kutimizwa, yaani nchi wanachama wa APEC zilizoendelea zinatakiwa kufikia lengo hilo kabla ya mwaka 2010, na nchi wanachama zinazoendelea zifikie lengo hilo kabla ya mwaka 2020. Hivi sasa muda uliobaki si mrefu kwa nchi zilizoendelea kufikia lengo hilo, lakini baadhi ya nchi hizo, kwa mfano, Japan, Australia, zinasema kuwa bado haziko tayari na zinaomba muda wa kufikia lengo hilo urefushwe, na nchi wanachama zinazoendelea zinataka nchi zilizoendelea zitimize ahadi zao mapema. Katika mazingira kama hayo watu wana wasiwasi kama lengo la biashara na uwekezaji huria linaweza kutimizwa. Mkutano huo utatathmini "lengo la Bogor" na kutunga "ramani" ya kulifikia lengo hilo.

Aidha, suala la kupambana na magonjwa mapya ya kuambukiza na maafa makubwa ya kimaumbile na uokoaji, pia ni masuala yatakayozungumzwa na viongozi wa APEC. Baada ya mkutano usio rasmi wa APEC uliofanyika mwaka jana, tsunami ya Bahari ya Hindi na kimbunga cha Katrina vilileta hasara kubwa ya mali na maisha ya watu. Hivi sasa homa ya mafua ya ndege imekuwa ikifuatiliwa sana duniani, na ni tishio jipya kwa usalama wa binadamu na uchumi wa APEC. Mkutano wa viongozi wakuu wa APEC uliomalizika tarehe 13 ulitoa "mapendekezo kuhusu kukinga na kudhibiti homa ya mafua ya ndege na kupunguza madhara yake" kwa mkutano usio rasmi wa viongozi wa APEC. Mkutano huo pia ulikubali kuitisha mkutano wa mawaziri wa APEC kuhusu kinga na udhibiti wa homa ya mafua ya ndege katika nusu ya kwanza ya mwaka 2006 nchini Viet Nam, na katika mwezi Aprili mwaka huo kongamano kuhusu magonjwa mapya ya kuambukiza litafanyika mjini Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-15