Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-15 18:21:06    
China inaendeleza uchumi kwa kutegemea maliasili za nchini

cri

Mkutano wa kimataifa wa shughuli za migodi wa mwaka 2005 umefanyika tarehe 15 hapa Beijing, mkutano huo unafuatiliwa na idara mbalimbali za migodi kote duniani. Waziri wa maliasili ya ardhi wa China Bwana Sun Wensheng amesema kwenye ufunguzi wa mkutano huo kuwa, China inatilia maanani hifadhi na matumizi mwafaka ya maliasili za madini na inategemea hasa maliasili zake katika kuendeleza uchumi wake. Akisema:

Serikali ya China inatilia maanani sana hifadhi na matumizi mwafaka ya maliasili za madini, inategemea hasa maliasili za nchini kwa kudumisha maendeleo endelevu ya uchumi na jamii yaliyo na uwiano kwa pande zote. Tunafanya juhudi kubwa katika kusukuma mbele kazi ya kubana matumizi ya maliasili na hifadhi ya mazingira, kuendelea kuongeza uchimbaji na uendelezaji wa maliasili nchini, na China inajitahidi kutafuta njia mpya ya kuendeleza shughuli za migodi ili ziwe na kiwango cha juu cha kisayansi na kiteknolojia, ziwe na ufanisi mzuri wa kiuchumi, ambazo ufanisi wa matumizi ya maliasili ni wa kiwango cha juu, na hazitaweza kuleta uchafuzi mkubwa kwa mazingira, tena kazi za migodi ziwe na uhakikisho wa usalama.

Kutokana na maendeleo ya haraka ya miji midogo ya wilaya, mahitaji ya nchini juu ya mafuta, makaa ya mawe, chuma, shaba na madini mengine yanaongezeka siku hadi siku, na uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za madini unaongezeka siku hadi siku.

Ili kuimarisha uwezo wa uhakikisho wa maliasili za madini kwa maendeleo ya uchumi na jamii, China inaongeza siku hadi siku nguvu ya uchimbaji na utafutaji wa maliasili muhimu za madini, hivi sasa imekamilisha uchambuzi wa nguvu ambazo bado hazijatumika za maliasili ya madini muhimu kama vile mafuta, gesi, makaa ya mawe, chuma na shamba; wakati huo huo China inaweka mkazo katika utafiti wa teknolojia muhimu za sekta za nishati na maliasili, na kuanzisha miradi mingi ya utafiti wa kisayansi na kiteknolojia ili kupata maendeleo makubwa.

China pia inawatia moyo wafanyabiashara kutoka nchi za nje kuanzisha shughuli zao za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini China. Katika miezi minane ya mwanzo ya mwaka huu, China imetoa leseni zaidi ya 110 za utafutaji wa madini na leseni zaidi ya 10 za uchimbaji wa madini kwa wafanyabiashara wa nje. Waziri wa maliasili ya ardhi wa China Bwana Su Wensheng alisema, hivi sasa teknolojia na zana za China za kuchimba madini bado ni duni, na fedha za uchimbaji wa madini pia hazitoshi, na usimamizi wa kazi hiyo unapaswa Kuboreshwa zaidi, katika siku zijazo China inataka kuimarisha ushirikiano na nchi za nje kwenye sekta hizo.

China itaimarisha zaidi mazingira ya kisheria na kisera yaliyo ya utulivu, usawa na uwazi, ili kuhakikisha haki na maslahi halali ya wafanyabiashara katika shughuli zao za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini China; kukamilisha sera husika, kuvutia uwekezaji kutoka nje na kuingiza teknolojia na usimamizi wa kisasa kutoka nje. Aidha itahamasisha mashirika husika ya nchini yaende nje kufanya ushirikiano wa kunufaishana katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.

Waziri Sun anaona kuwa, kuanzisha ushirikiano wa kimataifa katika utafutaji, uchimbaji na usimamizi wa maliasili za madini, hakika kutasukuma mbele ustawi na maendeleo ya shughuli za migodi kati ya China na nchi za nje kwenye msingi wa kunufaishana.

Wajumbe zaidi ya 1600 kutoka China na nchi za nje wamehudhuria mkutano wa kimataifa wa siku 3 kuhusu shughuli za migodi wa mwaka 2005 unaofanyika hapa Beijing, China, ambapo wajumbe watajadili masuala husika kuhusu sera za shughuli za migodi, maendeleo ya shughuli za migodi kote duniani na soko la bidhaa za madini.