Rais Hu Jintao wa China alifanya ziara ya kiserikali katika nchi za Uingereza, Ujerumani na Hispania kuanzia tarehe 8 hadi 15 mwezi Novemba, kutokana na mwaliko. Hiki ni kitendo kikubwa cha kidiplomasia cha kiongozi wa China katika sehemu ya Ulaya. Mkurugenzi wa idara ya Ulaya ya wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Zhao Jun alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa, ziara hiyo ya rais Hu Jintao imetimiza lengo lililotazamiwa na imepata mafanikio mazuri.
Rais Hu Jintao akiwa na nia ya kuimarisha kuaminiana, kukuza maoni ya namna moja, kuimarisha ushirikiano na urafiki, alibadilishana maoni na viongozi wa nchi tatu zilizotembelewa kuhusu uhusiano wa pande mbili na masuala yanayofuatiliwa nao kwa pamoja, katika ziara yake hiyo alikuwa na mazungumzo na maofisa na watu mashuhuri wa sekta mbalimbali na kuwaeleza sera za China kuhusu maendeleo ya amani. Alipozungumzia mafanikio ya ziara yake katika Ulaya, mkurugenzi wa idara ya Ulaya ya wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Zhao Jun alisema,
"Ziara hiyo imeimarisha uhusiano wa kisiasa wa pande mbili, kuhimiza ushirikiano wa mambo ya kiuchumi na kibiashara, kuimarisha msingi wa ushirikiano wa kirafiki wa pande mbili, kuthibitisha mwelekeo wa maendeleo ya uhusiano wa pande mbili katika siku za baadaye na kuhimiza maendeleo ya uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati ya China na nchi hizo tatu na Umoja wa Ulaya. Katika ziara hiyo China na nchi hizo tatu zilisaini baadhi ya mikataba au mapatano muhimu. Ziara hiyo imefanikiwa na kutimiza lengo lililotarajiwa."
Rais Hu Jintao akiwa nchini Uingereza alitoa mapendekezo manne kuhusu maendeleo ya uhusiano kati ya China na Uingereza katika siku za baadaye: Kudumisha mwelekeo mzuri wa maingiliano ya viongozi wa ngazi ya juu; Kuimarisha mazungumzo na ushirikiano wa kisiasa; Kukuza ushirikiano katika maeneo mbalimbali, Kutatua kwa njia mwafaka tofauti za maoni na masuala makubwa yanayofuatiliwa na pande mbili. Maofisa katika ngazi mbalimbali nchini Uingereza wanaona kuwa maendeleo ya China siyo tishio bali ni nafasi nzuri, Uingereza si kama tu inatarajia kuwa mwenzi wa China katika mambo ya uchumi, bali pia inatarajia kuwa mwenzi wake katika mambo ya siasa. Katika ziara ya rais Hu Jintao nchini Uingereza, pande mbili zilianzisha mfumo wa mazungumzo kuhusu maendeleo endelevu.
Hivi sasa Ujerumani iko katika kipindi cha uchaguzi mkuu, ziara hiyo ya rais Hu Jintao ina umuhimu wa kujihusisha na serikali mpya na ya zamani. Rais Hu Jintao alisisitiza kuwa hata kama hali ya dunia na hali ya nchi mbili itabadilika namna gani, maoni ya kuwa na ushirikiano wa kirafiki ya nchi hizo mbili hayatabadilika. Ujerumani ilieleza kuwa serikali mpya itadumisha uhusiano na sera zake za nje, na inapenda kuona kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaendelezwa na kuimarishwa kwa msingi wa taarifa ya pamoja ya Ujerumani na China na kukuza uhusiano halisi wa kiwenzi.
Rais Hu Jintao alipotembelea Hispania, China na Hispania zilitoa taarifa ya pamoja tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi, ambayo imetangaza kuanzisha uhusiano wa pande zote wa uhusiano wa wenzi wa kimkakati na kuthibitisha wazi maeneo ya ushirikiano yatakayotiwa kipaumbele.
Kukuza uhusiano na Umoja wa Ulaya pamoja na nchi za Ulaya ni moja ya sehemu muhimu ya sera ya kidiplomasia za China. Lengo la ziara hiyo ya rais Hu Jintao ni kwa ajili ya kuhimiza zaidi maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ulaya.
"Kufanikiwa kwa ziara ya rais Hu katika nchi za Uingereza, Ujerumani na Hispania kunadhihirisha kuwa uhusiano wa China na Ulaya umeshinda majaribio ya nyakati na mabadiliko ya hali ya dunia na kuingia katika kipindi tulivu cha maendeleo. Hivi sasa viongozi wa pande hizo mbili wameimarisha mazungumzo, uhusiano wa pande mbili katika maeneo ya uchumi na biashara unakuzwa kwa mfululizo, idadi ya watu wanaoshirikiana imeongezeka, msingi wa imani ya watu umeimarishwa zaidi, ushirikiano katika maeneo mbalimbali umekuzwa na pande hizo mbili zimekuwa na ushirikiano mzuri katika masuala mengi ya kimataifa na kikanda."
Bw. Zhao Jun alisema kuwa China na Ulaya zitaimarisha uhusiano wa pande zote wa wenzi wa kimkakati usiolenga upande wa tatu, njia ambayo itanufaisha maendeleo ya dunia na maslahi ya kimsingi ya watu wa nchi mbalimbali.
|