Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-17 16:43:13    
Watu wa kabila la Wamongolia waabudu rangi nyeupe

cri

Kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kaskazini ya China, wanaishi watu wa kabila la Wamongolia ambao wanaoishi maisha ya kuhamahama. Chini ya anga ya buluu na mawingu meupe, kwenye mbuga za majani zisizokuwa na mwisho wa upeo wa macho, mahema meupe ya kimongolia yamesambaa hapa na pale, na kondoo wengi wanaotapakaa wanaonekana kama lulu, ndiyo mazingira wanayoishi wafugaji wa kabila la Wamongolia. Katika maisha ya kila siku na imani ya kidini ya Wamongolia, rangi nyeupe inaonekana hapa na pale.
Watu wa Mongolia wanapenda rangi nyeupe, wanaipenda rangi hiyo kutokana na kuathiriwa na mazingira ya kimaisha, bali pia kutokana na uamini wao wa kidini na hadithi za mapokeo za kabila hilo. Watu wengi wa kabila la Wamongolia wanaishi katika mbuga za majani za kaskazini ambazo zimefunikwa na theluji nyeupe kwa kipindi kirefu wakati wa baridi.
 Rangi nyeupe ni rangi inayovutia uangalifu wa watu zaidi kuliko rangi nyingine, inaashiria utukufu, usafi, mustakabali mzuri na haki. Profesa He Xiangliang wa Idara ya utafiti wa makabila ya taasisi ya sayansi na jamii ya China alisema:
"Kwa upande wa kiutamaduni, mila na desturi zinaathiri utamaduni wa kikabila. Tabia ya kuabudu rangi nyeupe ya kabila la Wamongolia inahusiana na desturi zao za maisha, kwa sababu maziwa ya ng'ombe na mbuzi, na mahema yao yote ni ya rangi nyeupe."
 Profesa He alisema kuwa, desturi ya kupenda rangi inahusiana na tabia ya kikabila. Watu wa kabila la Wamongolia wanaishi kwenye mbuga za majani kizazi hadi kizazi, katika maisha yao ya kuhamahama ya kufuata maji na majani, Wamongolia wamekuwa na tabia ya ushupavu na kutopenda kujizuia.
 Tabia ya kuabudu rangi nyeupe pia inaonekana katika desturi zao za maisha ya kila siku. Kwa mfano Wamongolia wanapotoa heshima kwa Mungu na kuwakaribisha wageni, hutoa Hada, ambayo ni kitambaa kirefu chembamba na cheupe, na kuwapatia wageni pombe nyupe ya maziwa ya farasi. Wafugaji Wamongolia wanapenda sana farasi na ngamia weupe, na kuwachukua kama ni vitu vinavyoweza kuleta baraka na mali nyumbani kwao.
 Mahema ya kimongolia hujengwa kwa kitambaa kigumu cheupe, pamoja na vikundi ya kondoo, huonesha desturi ya Wamongolia ya kuabudu rangi nyeupe. Mahema manane meupe yaliyowekwa masalio ya vitu alivyotumia mwanasiasa na mwanajeshi maarufu katika historia ya kabila la Wamongolia Bw. Chenjiesihan ni sehemu takatifu kwa Wamongolia.
 Mwanzoni mwa karne ya 13 baada ya Bw. Chenjiesihan kufariki dunia, wajukuu wake waliweka vitu alivyotumia alipokuwa hai kama vile tandiko la farasi, mavazi ya kijeshi na kiboko cha farasi katika mahema hayo manane meupe, na kuandika maandishi maalum na sherehe maalum ya kumtambika. Wamongolia waishio katika sehemu mbalimbali wanatakiwa kufanya sherehe kubwa ya kumtambika Chenjiesihan katika majira manne ya mwaka. Kuanzia hapo, imekuwa desturi kwa Wamongolia kutoa heshima kwa mahema manane meupe kama njia muhimu ya kuwatambika mababu na kukumbusha historia ya kabila la Wamongolia.
Watu wa kabila la Wamongolia pia wamekuwa na desturi ya vyakula inayohusiana na rangi nyeupe ambayo ni pamoja na karamu nyeupe. Kwa desturi, karamu nyeupe huandaliwa baada ya kupata mavuno makubwa au kupata ushindi kwenye vita, inaashiria baraka na heri. Karibu vyakula vyote vinavyoandaliwa kwenye karamu hiyo vinatokana na maziwa, kama vile keki kavu ya maziwa, jibini, chai ya maziwa, pombe ya maziwa, tambi na kadhalika. Bi. Alatanwimuge wa kabila la Wamongolia ni hodari katika kutengeneza vyakula vya maziwa, alisema:
 "Njia ya kutengeneza vyakula vya maziwa vya kabila la Wamongolia ni kuchemsha maziwa, yaliyoganda juu ni ngozi ya maziwa, keki ya maziwa inatengenezwa baada ya kuchemshwa na kuacha mvuke utoke."
 Kwa watu wa Mongolia, rangi nyeupe pia ni dalili ya baraka katika harusi. Kwa mfano kwenye sherehe ya kuchumbia, pande mbili zinatakiwa kupatiana Hada nyeupe; kwenye karamu ya kuchumbia, mshenga atampatia mchumba wa kike pombe inayowekwa katika chombo cha kauri nyeupe pamoja na Hada nyeupe na vyakula vya maziwa. Bwana harusi anatakiwa kufunga kitambaa cheupe kiunoni, na kunywa bakuli moja ya maziwa na bi harusi kwa pamoja.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-17