Kutokana na kuwa nchi za Umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi zilizoendelea kukataa kurudi nyuma katika suala la kilimo, mkutano wa sita wa mawaziri wa WTO utakaofanyika huko Hong Kong mwezi Desemba umegubikwa na wingu jeusi, mazungumzo ya Doha yaliyoanza mwaka 2001 yanakabiliwa na hali ya hatari.
Wachambuzi wanaona kuwa tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, tatizo kubwa katika utandawazi duniani ni ugawaji usio na uwiano kati ya mapato na malipo. Nchi zinazoendelea zinapata faida kidogo lakini zinalipa kiasi kikubwa. Tatizo hilo liko katika kanuni za kimsingi za idara mbili muhimu katika utandawazi duniani, Shirika la Biashara Duniani WTO na Shirika la Fedha Duniani, na kanuzi hizo zinapotekelezwa suala hili linazidi kuonekana. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa hivi sasa matatizo yaliyotokea katika utandawazi duniani yamechangia kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na maskini na ni chimbuko fulani la nguvu za kupinga utandawazi duniani.
Kutofanikiwa kwa mkutano wa WTO uliofanyika huko Seattle mwaka 1999 na matukio mengi yaliyotokea katika utandawazi duniani yalizishitusha nchi za magharibi, na zilianza kuzifahamisha kuwa zitapata matokeo kinyume na matumaini yao ikiwa zitaendelea kutumia sera za jadi katika mazungumzo ya biashara, kwa hiyo zimeanza kujaribu kuzungumza na nchi zinazoendelea kwa wazo la kutaka ushirikiano. Kutokana na hali hiyo, "Taarifa ya Doha" inayoonekana yenye maendeleo ilitolewa, na nchi zilizohudhuria kwenye mazungumzo ziliongezeka hadi karibu nchi zote wanachama kutoka nchi 30 wakati mkutano wa Seattle ulipofanyika 1999.
Tofauti na mazungumzo mengine ya biashara, mazungumzo ya Doha yanaonesha wazi zaidi "mwelekeo wa maendeleo", yaani inaheshimu manufaa yanayostahiki ya nchi zinazoendelea na pia imezingatia mahitaji ya ukuaji wa uchumi na jamii. Kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia, kama Taarifa ya Doha ikitimizwa katika muda uliowekwa, faida za dola za Kimarekani bilioni 500 zitapatikana duniani kabla ya mwaka 2015 na nchi zinazoendelea zitapata sehemu kubwa ya faida hiyo.
Lakini hali ilivyo ni kwamba si rahisi kuutekeleza "mwelekeo wa maendeleo". Nchi zilizoendelea licha ya kutaka kulinda maslahi yao, zinataka kujipatia fursa nyingi zaidi za biashara, kwa hiyo mwelekeo huo umeacha njia iliyowekwa hapo awali. Nchi hizo licha ya kutaka kupunguza ushuru wa forodhani kwa bidhaa ambazo nchi hizo zina nguvu kubwa ya raslimali na teknolojia, zinataka kutunga kanuni mpya katika sekta ya hifadhi ya mazingira na urahishaji wa biashara, isitoshe, zinajaribu kukwepa kufungua soko la mazao ya kilimo na bidhaa zinazohitaji wafanyakazi wengi. Kutokana na hali iliyotajwa, nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea zinagongana moja kwa moja katika mazungumzo mengi.
Kuhusu kilimo, ruzuku kubwa na ushuru wa forodhani wa nchi zilizoendelea imesababisha kuwepo kwa bei mbaya katika soko la kimataifa la mazao, na kuzifanya nchi zinazoendelea zisiweze kustawisha sekta ya kilimo. Kutokana na takwimu za WTO, kiasi cha misaada ikiwa pamoja na ruzuku ya kilimo katika thamani ya jumla ya uzalishaji wa kilimo, nchini Uswis ni 47%, nchini Japan ni 41%, Umoja wa Ulaya 25%, Marekani 9.5%. lakini katika nchi zinazoendelea, isipokuwa Mexico, kila nchi haizidi 4%. Hata hivyo nchi zilizoendelea hazitosheki, zinataka kuongeza zaidi misaada hiyo kwa kilimo.
Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai, siku chache zilizopita alisema kwamba makubaliano ya mazungumzo ya Doha yapaswa kutekelezwa. Kupata au kutopata manufaa kwa nchi zinazoendelea ni kigezo cha kupima ufanisi wa mazungumzo ya Doha.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-18
|