Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-21 16:48:36    
Uhondo wa muziki, tamasha la muziki la kimataifa mjini Beijing

cri

Hivi karibuni tamasha la muziki la kimataifa lilifanyika mjini Beijing. Tamasha hilo liliwaletea uhondo mkubwa wa muziki wakazi wa Beijing. Kwenye tamasha hilo kundi la Simfoni la Berlin, Berliner Philharmoniker, lilionesha muziki wake.

Kundi la Simfoni la Berlin ni kundi la muziki wa okestra linaloongoza duniani, kila mtu katika kundi hilo ni mpigaji hodari wa ala aliyechaguliwa kutoka sehemu mbalmbali duniani. Mwaka 1979, mwongozaji muziki wa kundi hilo hayati Karajan alikuja na kundi hilo nchini China. Sasa, baada ya kupita miaka 26, kundi hilo limekuja tena likiongozwa na mwongozaji muziki Simon Rattle, na kushiriki katika tamasha hilo, Bw. Simon Rattle alisema, "Wenzangu wote wanafurahi sana kuja hapa China na kuonesha muziki wetu. Watu wengi waliniuliza, kwa nini tumechagua kuja China kuonesha muziki. Jibu langu ni rahisi, kwamba China inawakilisha maendeleo na mustakbali mzuri wa muziki. Kwa kutumia fursa hii, ningependa kuwapongeza waandaaji wa tamasha hili, kwani wamewapatia wakazi wa Beijing nafasi nzuri ya kusikiliza muziki mtamu. Tunafurahi kuja hapa China na tunaifarahia safari yetu ya muziki pamoja na Wachina."

Tamasha la muziki la kimataifa liliandaliwa na wizara ya utamaduni ya China na serikali ya Beijing. Tamasha hili lilianza mwaka 1998 na linafanyika kila mwaka. Hivi sasa tamasha hilo limekuwa moja ya matamasha makubwa ya muziki duniani, na limekuwa shughuli kubwa ya utamaduni mjini Beijing.

Katika tamasha hilo kuna maonesho 18 ikiwa ni pamoja na opera, simfoni, muziki wa chumbani, muziki wa piano unaopigwa na mpigaji mmoja na wawili wawili. Wanamuziki karibu elfu moja waliotoka nchi zaidi ya kumi za Ufaransa, Ujerumani, Czech, Marekani na nchi nyingine walishiriki kwenye tamasha hilo, kati yao mpigaji fidla maarufu Sarah Chang, mpigaji piano Pogorelich na ndugu yake mdogo wa kike Labeque, mwimbaji maarufu Studer, wote ni wanamuziki wanaojulikana miongoni mwa mashabiki wa muziki wa China, na waongozaji muziki Norrington, Edo De Waart, Simon Rattle na mpiga fidla kubwa Gerhardt, mpiga fidla ya kiasi Zimmermann, wote ni wanamuziki wakubwa katika nyanja ya muziki.

Katika tamasha hilo mchezo uliofuatiliwa zaidi ni opera ya "Pete ya Nibelungen" iliyotungwa na mwanamuziki wa Ujerumani Wagner ambayo inaoneshwa na Jumba la Opera la Taifa la Nurnberg la Ujerumani. Hii ni mara ya kwanza kwa opera hiyo kuoneshwa mjini Beijing baada ya kuhaririwa upya. Opera hiyo ina sehemu nne, na kila sehemu inatumia muda wa saa nne, opera hiyo ilimalizika kwa siku nne, kila sehemu watazamaji walijaa na hawakuondoka hata mmoja kabla ya sehemu moja kumalizika zaidi ya saa sita za usiku. Mwongozaji muziki wa China Bw. Bian Zushan kwa furaha aliwaambia waandishi wa habari, akisema, "Nimetizama opera ya 'pete' sehemu zote nne, nimesubiri opera hiyo kwa zaidi ya miaka hamsini, nilipokuwa mwanafunzi nilitaka kuiona, lakini sikupata nafasi, leo nimeridhika."

Aliongeza kusema, tamasha hilo limechangia maisha ya utamaduni ya wakazi wa Beijing, na inasaidia kuinua upeo wao wa kufahamu simfoni na opera ya Kimagharibi.

Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Qinghua Bibi Yang pia alisema, "Nimetizama sehemu zote nne, zimenivutia sana. Sasa nimefahamu jinsi opera ya Kimagharibi ilivyo."

Katika tamasha hili opera ya Kibeijing ambayo inasifiwa kama ni johari ya utamaduni wa jadi pia ilioneshwa. Muziki wa opera ya Kibeijing ulipigwa katika tamasha hilo. Muziki wa opera hiyo uliohaririwa kwa simfoni ulipopigwa uliwavutia sana wasikilizaji. Mchezaji mkuu katika opera hiyo Yuan Huiqin alisema, hili ni jaribio la kuunganisha sanaa ya jadi ya Kichina na ya Kimagharibi. Alisema, "Simfoni ya opera hiyo imeunganisha muziki wa jadi opera ya Kibeijing na kuifanya opera hiyo ivutie zaidi. Ni wajibu wetu sisi wachezaji namna ya kuifanya michezo yetu inavutia zaidi watizamaji. Hili ni jaribio zuri."

Watazamaji wana maoni tofauti kuhusu jaribio hilo, msikilizaji mmoja alisema, "Naona opera ya Kibeijing inavutia zaidi ikisaidiwa na simfoni, muziki umekuwa na msukumo mkubwa zaidi."

Lakini mwanafunzi Kris wa Chuo Kikuu cha Beijing aliyetoka Poland alisema, "Naona opera ya jadi ya Kichina inawakilisha utamaduni mtupu wa Kichina, haina haja kusaidiwa na muziki wa Kimagharibi, mimi napenda utamaduni wa Kichina, sipendi utamaduni wake uathiriwe na utamaduni wa nje."

Ni kweli kwamba kuna maoni tofauti kuhusu kuingiza simfoni kwenye opera ya Kibeijing. Lakini kuwaletea watazamaji wa Beijing aina mbalimbali za muziki lilikuwa ni lengo la tamasha hilo.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-21