Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-22 10:12:53    
Wafanyabiashara wa kigeni walioko kwenye soko la Yiwu

cri

Yiwu ni mji mdogo wa mkoa wa Zhejiang, sehemu ya mashariki ya China, ambao unajulikana sana kutokana na uzalishaji na uuzaji wa bidhaa ndogondogo zinazohitajiwa na watu katika maisha ya kila siku. Kuna aina nyingi za bidhaa hizo zinazouzwa kwa bei rahisi, hivyo zinawavutia wafanyabiashara wa nchi nyingi duniani, na bidhaa zinazosafirishwa kila siku kwenda kwenye sehemu mbalimbali duniani zinazidi makontena 1,000. Katika kipindi cha nchi yetu mbioni cha leo, nitawafahamisha kuhusu biashara ya mfanyabiashara mmoja kutoka nchi ya Ujerumani kwenye soko la mji wa Yiwu.

Bw. Florian Satzinger ni mfanyabiashara kutoka Ujerumani, jambo linalomfurahisha zaidi kila siku ni kutoa habari kuhusu bidhaa kwa wateja wake walioko kwenye sehemu mbalimbali duniani na kuwapatia huduma za usafirishaji bidhaa. Alipozungumzia biashara yake mjini Yiwu alisema kwa furaha,

"Tunavutiwa na sehemu hii. Katika Yiwu tunaweza kupata bidhaa za aina mbalimbali bila matatizo, tunaweza kuagiza kontena zima la bidhaa, vilevile tunaweza kuagiza baadhi za sampuli tu, watu wa hapa wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, tunashirikiana vizuri."

Bw. Florian alifika Yiwu kufanya biashara miaka miwili iliyopita, na amesajili kampuni yake inayojulikana kwa jina la "Dunia ya Utajiri na Akili" na kushughulikia usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za nje. Ndani ya kampuni yake kuna bidhaa nyingi alizoleta Bw. Florian kutoka nchi za Ulaya zikiwemo viatu vya ngozi vya Italia, bia za Ujerumani na mvinyo kutoka Ufaransa, lakini bidhaa nyingi zaidi anazoshughulikia ni bidhaa ndogondogo zinazozalishwa kutoka sehemu mbalimbali za China.

Bw. Florian ambaye anapenda kuvaa mavazi ya jadi ya enzi ya Tang ya China, alisema kuwa hivi sasa biashara yake bado siyo kubwa sana, lakini anavutiwa na mustakabali wa kampuni yake iliyoko kwenye soko la mji wa Yiwu.

Yiwu ni mji ulioendelea sana katika shughuli za biashara, miongoni mwa watu 8 wa mji huo wenye idadi ya watu milioni 1.6, kuna mtu mmoja anayefanya shughuli za biashara. Katika soko la Yiwu zinauzwa aina zaidi ya elfu 320 za bidhaa, hivyo solo hilo limesifiwa kuwa bahari ya bidhaa ndogo ndogo na ni kama paradiso kwa wateja. Thamani ya biashara inachukua nafasi ya kwanza kwa miaka 14 mfululizo miongoni mwa masoko yote ya nchini China, hivi sasa limechukua nafasi ya kwanza kwa usafirishaji wa bidhaa zinazohitajiwa na watu katika maisha duniani na kuwa kituo muhimu cha usafirishaji bidhaa kwa nchi za nje cha China.

Hivi sasa wafanyabiashara wa kigeni zaidi ya 8000 wanafanya kazi katika mji wa Yiwu kama Bw. Florian, ambao wanatoka katika nchi na sehemu zaidi ya 100 duniani, na wengi wao walitoka nchi za kiarabu zikiwemo Jordan, Misri na Palestina.

Bw. Khaderalmenawi mwenye umri wa miaka 28 mwaka huu anatoka Palestina, kabla ya kufika mji wa Yiwu aliwahi kusoma katika chuo kikuu cha mawasiliano cha Shanghai, China. Kutokana na kuwa anaweza kuongea lugha ya Kichina, aliposoma katika chuo kikuu aliwahi kuwa mkalimani wa marafiki zake waliofika China kufanya biashara kutoka nchi za kiarabu, polepole akajua soko la China na kufahamu mji wa Yiwu. Mwaka 2001 baada ya kumaliza masomo yake ya uhandisi ya elektroniki katika chuo kikuu cha mawasiliano cha Shanghai, alianza biashara na kuanzisha kampuni ya usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za nje mjini Yiwu.

"Wengi wa watu ninaowafahamu, wanajua mji wa Yiwu, na wanasema kuwa bidhaa zinazozalishwa huko ni nzuri na za aina nyingi. China inaendelea, wafanyabiashara wa nchi nyingi wamegundua fursa nzuri za biashara za hapa, mimi sitaki kukosa fursa hiyo. Kampuni yangu hasa ni kuwasaidia wafanyabiashara wa nchi mbalimbali kupata bidhaa nzuri hapa."

Bw. Khaderalmenawi alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa ingawa bidhaa anazozisafirisha kwenda nchi za mashariki ya kati ni za aina mbalimbali, lakini nyingi zaidi zilikuwa za hardware na mapambo ya wanawake. Bidhaa za Yiwu zina soko zuri katika nchi za mashariki ya kati, mwanzoni baada ya kufika huko kila mwezi alisafirisha makontena 15 ya bidhaa ndogo ndogo. Hivi sasa pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya biashara mjini Yiwu, ushindani umekuwa mkali, hata hivyo anaweza kusafirisha makontena 10 ya bidhaa kwa nchi za nje.

Tokea katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, maonesho ya biashara ya bidhaa ndogo ndogo yanafanyika kila mwaka mjini Yiwu, ambapo zinaonesha bidhaa zilizozalishwa katika sehemu nyingi za China na dunia. Katika maonesho ya biashara yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu mjini Yiwu, idadi ya wafanyabiashara wa kigeni waliofika huko kununua bidhaa ilizidi elfu 10.

Bw. Ruban Kainth kutoka Canada ana kampuni moja ya usafirishaji wa bidhaa kwa nchi za nje, kila mwaka anafika China mara kadhaa kuagiza bidhaa ndogo ndogo, na hakosi kutembelea Yiwu. Alisema kuwa bidhaa za Yiwu ni nzuri na za bei rahisi, hivyo kila mara alinunua kontena zima au makontena kadhaa za bidhaa. Katika maonesho ya biashara yaliyofanyika mjini Yiwu, Bw. Ruban alitembelea kaunta nyingi za bidhaa na kuuliza bei na kufikiri kuhusu uagizaji wa bidhaa.

"Kusema kweli, vitu ninavyotaka kuagiza ni vingi, nitaamua kiasi cha bidhaa nitakazonunua kutokana na hali ya bei za vitu."

Soko la biashara la kimataifa ni mahali ambapo hakosi kutembelewa na kila mfanyabiashara wa kigeni aliyefika mjini Yiwu, na pia ni soko la kwanza kwa ukubwa kwa uuzaji wa jumla duniani. Jengo hilo refu kama joka kubwa, ambalo mzunguko wake ni kilomita 6. Mtu mmoja alipiga hesabu kuwa, endapo mtu anasimama kwa dakika moja kwenye kila duka la huko, na kila siku alihesabu kuna saa 8 za kazi, basi mtu akimaliza kutembelea maduka yote ya huko atatumia muda wa miezi zaidi ya 2.

Katika soko hilo limetengwa eneo la biashara kwa wageni likiwemo Jumba la Wageni la Korea ya Kusini. Katika miaka ya karibuni, pamoja na kustawi kwa soko la Yiwu, wafanyabiashara zaidi ya 3,000 kutoka Korea ya Kusini walifika huko kuanzisha viwanda mjini Yiwu, viwanda 45 vya wafanyabiashara hao wa Korea ya Kusini vimejenga sehemu za maonesho ya bidhaa zao katika soko hilo. Wakitumia soko la biashara la kimataifa la Yiwu, wanauza bidhaa zenye umaalum wa kikorea zikiwemo za kielektroniki, vyombo vya umeme, vitu vya sanaa za kazi za mikono, vitu vya zawadi na nguo kwa wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Katika duka moja linalouza simu, mwenye duka aliyetoka Korea ya Kusini Bw. Lee Song Yong alisema kuwa aliingia kwenye soko hilo mwishoni mwa mwezi Julai, na anafurahia sana mazingira ya biashara ya huko. Alisema kuwa mazingira ya huko ni mazuri na safi, usimamizi wa soko pia ni mzuri, hivyo wanaona shughuli zao zinaendeshwa bila matatizo.

Bw. Lee Song Yong na wafanyabiashara wengi wa kigeni, pia wanaona ni rahisi kuendesha shughuli zao za biashara katika mji wa Yiwu, wanaona kuwa huduma nyingine za mji huo kama maghala, usafirishaji wa bidhaa, forodha, mambo ya fedha, bima na mtandao wa upashanaji habari pia ni bora.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-22