Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-22 10:27:12    
Barua 1122

cri

Msikilizaji wetu Franz Manco Ngogo wa Tarime Tanzania ametuletea barua pepe akisema kuwa, anayo heshima kubwa kutuarifu kuwa, kwa muda mrefu sasa amekuwa kimya kiasi, japo yuko nasi bega kwa bega kuimarisha usambazaji wa habari kuhusu China na Radio China kimataifa yenyewe.

Anasema ama kwa upande wa vipindi na mipango yetu yote ya utangazaji wa matangazo ya idhaa ya Kiswahili, anashindwa aanzie wapi kutupongeza kwa jinsi tunavyojali matakwa ya wasikilizaji wetu. Si vipindi vilivyoboreshwa wala muda wa matangazo uliokidhi matakwa ya wasikilizaji, ama watangazaji waliojitolea kwa moyo kuendeleza hayo yote. Hivyo vyote vinaenda kwa pamoja na kwa uhakika sana.

Kwa upande wa Club yake ya Kemogemba, wao wako bega kwa bega kuuendeleza urafiki huu wa tangu enzi ya maelewano baina ya mataifa haya mawili Tanzania na China. Mfano mzuri ni pale watakapojibu maswali ya chemsha bongo kuhusu Taiwan kisiwa cha hazina cha China.

Mwisho ni juu ya zawadi yake ambayo anasikitika kuona kuwa Bw. Wambwa ameichelewesha sana, anatia mashaka kuwa labda ameipoteza na hivyo anaona haya kueleza. Licha ya Bw. Mogire Machuki kujitolea kuileta, hapo pote Xavier hakujaribu hata kidogo kutekeleza hilo.

Na Bwana Ngogo anasema tovuti yetu ya idhaa ya Kiswahili inasomeka vizuri na inatosheleza kabisa.

Tunamshukuru sana Bwana Ngogo kwa barua pepe yake, kweli yeye ni msikilizaji wetu bora ambaye kila baada ya muda fulani hutuletea barua pepe na kutoa maoni yake bila kuficha. Tunamshukuru sana kwa juhudi zake za kusambaza habari za Radio China kimataifa na kushirikiana na wanachama wa klabu yake kusukuma mbele urafiki kati ya China na Tanzania. Tena tunashukuru sana kila mara anatutia moyo sisi watangazaji na watayarishaji kwa kazi yetu. Tutaendelea kuchapa kazi ili kuwahudumia vizuri wasikilizaji wetu.

Na kuhusu zawadi yake ambayo tulimkabidhi Bwana Wambwa ambaye ni msikilizaji wetu aliyepata ushindi katika mashindano ya chemsha bongo ya mwaka jana na kubahatika kuja kuitembelea China kwa matembezi ya siku 10, kweli ni kosa letu pia, tulidhani kuwa ni rahisi kumtumia zawadi Bwana Ngogo kupita kwa Bw Wambwa kuliko kutuma kwa njia ya posta, hivyo tunamwomba Bwana Wambwa ambaye aliahidi kuwakilisha hiyo zawadi kwa Bwana Ngogo afanye hivyo. Lakini pia inawezekana kuwa huenda ana tatizo fulani, kwani yeye mwenyewe tangu aondoke hapa Beijing na kurudi nyumbani hajatuandikia barua hata mara moja, na sisi tuna wasiwasi na hali yake ya sasa. Hapa tunapenda kumwomba radhi Bwana Ngogo, labda tutaweza kutafuta njia nyingine ya kuweza kukutumia zawadi, tukishindwa tutakuambia. Ni matumaini yetu kuwa hautasikitishwa tena kutokana na jambo hilo, endelea kutuunga mkono.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Sharif wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya anasema katika barua yake kuwa, kuhusu mashindano ya chemsha bongo ya mwaka huu yaliyoandaliwa na Radio China kimataifa kuhusu Taiwan, kisiwa cha hazina cha China, alichelewa kupata habari, kwani saa ya matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa kupitia Radio KBC imebadilika kuwa saa 9 alasiri badala ya saa 10.

Anasema jambo la kushangaza hata angeelewa kidogo ingawa angepata hiki kipindi kikiendelea angependa kutujulisha kuwa alipigwa na butwaa baada ya kufungua radio muda mfupi baada ya saa 9, na kusikia kuwa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa yamekwisha. Anasema aliingiwa na hasira nyingi na kwa kinaga ubaga hakuwa na hata hamu ya kula chakula chochote alipofahamu amekosa habari hizi, kwa hivyo anauliza kwa nini matangazo haya yamewekwa saa 9 badala ya saa 8 ? Ni saa au ni radio iliyokuwa ina matatizo? Anaomba tafadhali angependa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa imjulishe vizuri, kwani ikiwa vivyo hivyo hii italeta balaa, kwani wao kama mashabiki wataweza kuchanganyikiwa. Anataka tuwaeleze vizuri kama ni saa 9 au saa 8.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyo Mutanda Ayubu Sharif kwa barua yake na malalamiko yake. Kuanzia mwezi Septemba, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya CRI na KBC, matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya CRI yameongezwa muda na kuwa saa moja badala ya nusu saa, lakini saa ya kutangazwa kwake pia imebadilika, kuwa saa tisa badala ya saa 11 jioni kutokana na ombi la KBC kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, lakini jumapili muda wa matangazo yetu ni kuanzia saa 8 badala ya saa 9, hii vilevile ni kutokana na ombi la KBC, kabla ya tarehe mosi Septemba, tuliwahi kutangaza taarifa juu ya hayo kila wiki, labda baadhi ya wasikilizaji wetu hawakuweza kupata habari hii. Hapa tunaomba radhi.

Na kuhusu malalamiko yake mengine ya salamu zenu, Bwana Sharif anataka sisi tusirudie salamu kila mara, anataka tusome mara moja au mara mbili tu, kutokana na hali yetu ya sasa, labda tunashindwa kufanya hivyo, lakini kuanzia mwaka ujao, hali itabadilika, tafadhali tuelewe na utuvumilie kidogo, ili tuweze kurekebisha vizuri kazi zetu.

Na msikilizaji wetu Onesmo H. Mponda wa sanduku la posta 6117, Morogoro Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, hatimaye anajitokeza tena katika kipindi maarufu cha sanduku la barua cha idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Na kubwa zaidi anapenda kuitumia fursa hii kuipongeza na kuishukuru Radio China kimataifa kwa kuyaheshimu na kuyazingatia maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wake juu ya kuongezwa kwa muda wa matangazo, ambapo hivi sasa matangazo yanasikika kwa muda wa saa moja badala ya nusu saa.

Kwa hakika amevutiwa mno na mabadiliko hayo kwani inaonesha ni kwa jinsi gani Radio China kimataifa inavyowajali wasikilizaji wake. Mwisho yeye akiwa miongoni mwa wasikilizaji wa Radio China kimataifa, anaahidi kuendelea kuyaunga mkono daima matangazo ya Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Onesmo H. Mponda ambaye ni rafiki yetu wa tangu zamani kwa barua yake ya kututia moyo kuchapa kazi zaidi ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu .

Idhaa ya kiswahili 2005-11-22