Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-24 16:14:00    
Wagonjwa wa Ukimwi wafuatiliwa ipasavyo nchini China

cri

Katika miaka ya karibuni, kutokana na kuenea kwa ujuzi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, hofu ya Wachina kwa ugonjwa wa Ukimwi na unyenyepa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi unapungua siku hadi siku, watu wengi wameanza kuwafuatilia wagonjwa hao na kuwasaidia kwa njia mbalimbali.

Bwana Tao Tongxue mwenye umri wa miaka 43 ni mkulima anayeishi katika mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China. Yeye aliambukizwa virusi vya Ukimwi miaka 10 iliyopita na kuwa mgonjwa wa Ukimwi kuanzia miaka mitatu iliyopita. Baada ya kupata matibabu, hivi sasa hali yake ya afya imekuwa nafuu. Muda si mrefu uliopita Bw. Tao Tongxue alipokuja Beijing kuhudhuria baraza lisilo la kiserikali kuhusu kinga na tiba ya ugonjwa wa Ukimwi alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika maskani yake watu elfu mbili hivi wameambukizwa virusi vya Ukimwi, na wote wanapewa msaada wa serikali na jamii. Akisema:

"Tulipimwa virusi vya Ukimwi na kupewa matibabu bila ya malipo yoyote, watoto wetu pia wanasoma shuleni bila kutoa malipo yoyote. Nikiwa mgonjwa wa Ukimwi ninayeishi kijijini, sina uwezo wa kugharamia dawa za hospitalini, hivyo ni muhimu sana kwangu kupimwa na kutibiwa bure."

Bw. Tao Tongxue alisema hivi sasa hali yake ya afya imedhibitiwa vizuri, maisha yake hayana tofauti sana na ya watu wasio wagonjwa, hayo yote yanatokana na msaada wa serikali na upendo wa jamii.

Tangu mgonjwa wa kwanza wa Ukimwi agunduliwe katikati ya miaka ya 80 ya karne iliyopita hadi leo, inakadiriwa kuwa Wachina laki nane na elfu 40 wameambukizwa virusi vya Ukimwi. Jinsi ya kuwasaidia watu hao kudhibiti hali yao ya afya, na jinsi ya kuwasaidia waishi maisha kama ya watu wengine limekuwa jambo linalofuatiliwa sana na idara za afya za serikali ya China na watu wa jamii.

Ili kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa wagonjwa wa Ukimwi, serikali ya China imetunga sera kadhaa wa kadhaa za kuwasaidia wagonjwa hao, kwa mfano, kuwapatia wagonjwa wa Ukimwi wenye matatizo ya kiuchumi dawa na tiba bila ya malipo yoyote, wajawazito walioambukizwa virusi vya Ukimwi wanapewa ushauri wa kiafya, maelekezo kabla ya kujifungua na huduma za kujifungua bila ya malipo yoyote. Serikali za ngazi mbalimbali na watu wa jamii pia wanawapatia wagonjwa wa Ukimwi wenye matatizo ya kiuchumi na jamaa zao msaada wa fedha kwa maisha yao. Watoto yatima ambao wazazi wao walikufa kwa Ukimwi wanapewa uangalifu katika maisha, elimu na afya ya akili.

Watu wengi wa fani mbalimbali za jamii pia wamejitolea kuwasaidia wagonjwa wa Ukimwi. Jumuiya isiyo ya kiserikali iitwayo "nyumba ya mwangaza wa jua" iliyoko huko Kunming, mji mkuu wa mkoa wa Yunnan, kusini magharibi mwa China, ni moja ya jumuiya za kijamii zinazowasaidia wagonjwa wa Ukimwi. Bwana Li Yun wa jumuiya hiyo alisema:

"Mkoani Yunnan asilimia 80 ya wagonjwa wa Ukimwi waliambukizwa virusi vya Ukimwi kwa kujidunga sindano za dawa za kulevya kwenye mishipa ya damu. Watu hao wamejitenga na jamii kwa muda mrefu, na wamepoteza uwezo wa kujimudu. Jukumu kubwa la jumuiya ya mwangaza wa jua ni kuwasaidia kisaikolojia ili waweze kurejea katika jamii."

Juhudi moja ya jumuiya ya mwangaza wa jua ni kuwafundisha watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi ufundi wa kikazi ili waweze kujitegemea kimaisha, pia inawaandalia wagonjwa na jamaa zao mafunzo kuhusu jinsi ya kuwatunza wagonjwa wa Ukimwi. Tokea mwaka 2003 hadi sasa, jumuiya ya mwangaza wa jua imeandaa semina ya aina hiyo kwa wagonjwa 270 wa Ukimwi na familia 115.

Watoto yatima ambao wazazi wao walikufa kwa Ukimwi, na watoto walioambukizwa virusi vya Ukimwi pia wamepata uangalifu na upendo kutoka kwa serikali na jamii.

Katika mji wa Fuyang mkoani Anhui, sehemu ya mashariki ya China, kuna jumuiya inayowasaidia watoto 280 wagonjwa wa Ukimwi na wenye matatizo ya kiuchumi. Jumuiya hiyo ilianzishwa na wanakampuni. Mkuu wa jumuiya hiyo Bi. Zhangying alisema:

"Zamani watoto hao walipuuzwa na jamii, sasa watoto wote wanapata fursa ya kusoma shuleni, wanaweza kutoa maoni yao na kuonesha tabia zao wapendavyo. Tumeona kuwa miaka miwili baada ya kuja hapa, watoto hao wamerejesha imani yao moyoni na tabasamu usoni."

Hivi sasa watu wengi zaidi nchini China wanaweza kuwatendea vizuri wagonjwa wa Ukimwi na wale walioambukizwa virusi vya Ukimwi. Baadhi ya wachezaji maarufu wa filamu na vipindi vya televisheni wanajishirikisha na shughuli za kuwasaidia wagonjwa wa Ukimwi, na kuitaka jamii iwaoneshe wagonjwa wa Ukimwi ufuatiliaji mwingi zaidi. Mwanzoni mwa mwaka huu, wanafunzi kadhaa wa shule za msingi za Beijing hata waliweza kuwapokea watoto yatima ambao ni wagonjwa wa Ukimwi nyumbani kwao.

Watu wengi walioambukizwa virusi vya Ukimwi wanashirikiana pamoja katika kupambana na Ukimwi. Bwana Lixiang mwenye umri wa miaka 29 ni mgonjwa wa Ukimwi, miaka mitatu iliyopita yeye na wagonjwa wengine wa Ukimwi walianzisha jumuiya iitwayo "mikoko", ambayo imefanya kazi nyingi katika kueneza ujuzi kuhusu Ukimwi na kupunguza unyenyepa wa jamii dhidi ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi. Bw. Lixiang alisema:

"Tunatumia njia mbalimbali kuwahimiza watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi kushiriki katika shughuli zetu. Kwa mfano kuanzisha mfumo wa upashanaji habari, kuweka simu maalum za kuwahudumia watu wenye matatizo, kuanzisha mtandao wa Internet na magazeti. Pia tumeandaa semina husika za aina mbalimbali."

Hivi sasa, China ina jumuiya zaidi ya 40 zilizoanzishwa na watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi. Wanachama wa jumuiya hizo wanatiana moyo, na kuwafahamisha watu wengi zaidi ujuzi kuhusu Ukimwi, wamefanya juhudi zao ipasavyo katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-24