Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-25 18:27:37    
Ushirkiano kati ya China na Afrika una mustakbali mzuri

cri

Kuanzia tarehe 12 hadi 24, mwezi Novemba mwaka huu, mjumbe wa kudumu wa ofisi ya siasa ya kamati kuu ya chama cha kikomunisti cha China Bw. Li Changchun alifanya ziara za kirafiki katika nchi nne barani Afrika, nchi hizo ni Sudan, Namibia, Afrika ya Kusini na Tanzania.

Hii ni shughuli muhimu za kidiplomasia za China katika kuimarisha mawasiliano urafiki na ushirikiano kati yake na nchi za Afrika, pia ni moja ya ziara ya viongozi wa ngazi ya juu wa China zinazofanyika barani Afrika tokea mwaka huu.

Mkuu wa ofisi ya mambo ya Afrika ya idara ya mawasiliano na nje ya kamati kuu ya chama cha kikomunisti cha China Bi. Li Liqing amesema kuwa, Chama cha kikomunisti cha China na serikali ya China siku zote zinatilia maanani uhusiano wa kirafiki na Afrika, na imeweka mkazo katika kukuza uhusiano kati yake na nchi za Afrika tangu ianze kutekeleza sera ya kufanya mageuzi na kufungua mlango. Mwaka 2004, rais Hu Jintao wa China alitembelea Afrika, na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya pande hizo mbili. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa pande hizo mbili wamekuwa wakizidi kuwasiliana, na mawasiliano ya kisiasa yamekuwa yakiongezeka, na kuaminiana kwa pande hizo mbili katika mambo ya siasa pia kumeimarishwa siku hadi siku. Kutokana na juhudi za viongozi wa pande hizo mbili, urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, umepita changamoto za mabadiliko mengi yaliyotokea duniani, na kupata maendeleo mapya katika sekta mbalimbali.

Imefahamika kuwa, mwaka jana, viongozi wa nchi 11 za Afrika walitembelea China, mwaka huu, viongozi 10 wa Afrika wametembelea China. Viongozi wengi wa serikali mpya ya China wametembelea Afrika au wanajiandaa kufanya ziara barani Afrika. Chama cha kikomunisti cha China kimeanzisha uhusiano wa mawasiliano ya aina mbalimbali kati yake na vyama zaidi ya 60 vya nchi zaidi ya 40 za Afrika, na mawasiliano hayo yametoa mchango muhimu katika kuhimiza uhusiano kati ya pande hizo mbili katika sekta zote.

Tangu kiongozi wa kwanza wa China atembelee bara la Afrika, katika nusu karne iliyopita, China siku zote inashikilia kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani, kuheshimu nchi za Afrika kujichagulia mfumo wa kisiasa na njia ya maendeleo, na kuzihimiza China na nchi za Afrika ziwe marafiki wa kuaminiana. Li Liqing anaeleza kuwa, uhusiano wa kisiasa kati ya China na Afrika umepata maendeleo mapya chini ya hali mpya ya kimataifa. China inafanya juhudi kuhimiza jumuiya ya kimataifa itilie maanani amani na maendeleo ya Afrika, kuunga mkono nchi za Afrika zishiriki katika mambo ya kimataifa kwa usawa. Kuhusu suala la mageuzi ya Umoja wa Mataifa, China inaunga mkono kuongeza viti vya nchi zinazoendelea hususan nchi za Afrika katika baraza la usalama. Aidha, China imepeleka walinzi zaidi ya 800 wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Liberia na nchi nyingine za Afrika.

China na nchi za Afrika zote zinabeba jukumu la pamoja la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, na kuimarisha hali ya kuaminiana kati ya pande hizo mbili katika mambo ya siasa kumetoa mazingira mazuri kwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika. Mwaka jana, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilikaribia dola za kimarekani bilioni 30, kiasi ambacho kimeongezeka kwa zaidi ya mara 30 kikilinganishwa na miaka 25 iliyopita. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ongezeko la biashara kati ya pande hizo mbili limefikia asilimia 42.

Li Liqing amesema kuwa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika umeleta manufaa ya pamoja kwa pande hizo mbili. Katika miaka ya hivi karibuni, thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nchi za Afrika ilizidi thamani ya bidhaa za China zilizosafirishwa kwenda barani Afrika, na serikali ya China inahimiza kampuni za China kuanzisha biashara katika nchi za nje, na kuzileta fedha na kwenda huko na mitaji na teknolojia zao. Hadi kufikia nusu ya kwanza ya mwaka huu, jumla ya kampuni 700 za China zimewekeza vitega uchumi barani Afrika, na thamani ya jumla ya uwekezaji imefikia dola za kimarekani milioni 75. Aidha, kampuni za China zinajishughulisha na ujenzi wa miradi mingi ya miundo mbinu ya nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na mawasiliano na upashanaji habari. Hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka jana, thamani ya mikataba ya ujenzi imefikia dola za kimarekani bilioni 30.6, na ushirikiano wa kilimo kati ya pande hizo mbili umetoa mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la upungufu wa chakula la nchi za Afrika.

Pia serikali ya China imetimiza ahadi yake kupunguza hata kusamehe madeni yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 10.5 zilizodaiwa nchi 31 za Afrika, na kupunguza au kufuta ushuru wa forodha kwa nchi 25 zilizoko nyuma kiuchumi duniani. Misaada hiyo iliyotolewa na China kwa nchi za Afrika haina masharti yoyote ya kisiasa.

Kwa upande mwingine, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara unaozidi kuimarishwa unasukuma mbele maendeleo ya uhusiano wa kisiasa kati ya China na Afrika. Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika lililoanzishwa mwaka 2000 limetoa fursa mpya kwa pande hizo mbili kukuza maelewano, kuimarisha urafiki na kupanua ushirikiano.

Chini ya mfumo wa baraza hilo, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umepata maendeleo katika sekta nyingi zaidi. Licha ya kupeleka wataalamu, madaktari, walimu na mafundi katika nchi za Afrika, serikali ya China pia imeahidi kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta ya uendelezaji wa nguvu kazi, na kuwaandaa wataalamu elfu 10 wa sekta mbalimbali kwa nchi za Afrika kuanzia mwaka 2004 hadi 2006.

Li Liqing amesifu hali nzuri ya ushirikiano kati ya China na Afrika. Anaamini kuwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili utakuwa na mustakabali mzuri, na ziara ya Bw. Li Changchun katika nchi 4 barani Afrika itazidi kusukuma mbele uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta zote.