Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-28 16:10:23    
Tamasha la Sanaa la Asia Lafanyika Mjini Foshan, China

cri
Kuanzia tarehe 11 hadi 17 Novemba Tamasha la Sanaa la Asia lilifanyika katika mji wa Foshan, kusini mwa China. Wasanii zaidi ya 500 kutoka nchi 21 za Asia walishiriki kwenye tamasha hilo.

Kwenye ufunguzi michezo 26 kutoka nchi 21 za Asia ilioneshwa.

Tamasha la sanaa la Asia lilianzishwa na Wizara ya Utamaduni ya China mwaka 1998, ni tamasha linalofanyika kila mwaka. Mada ya tamasha la mwaka huu ni "kukutana na kustawisha utamaduni", baadhi ya nchi ambazo hazikushiriki katika tamasha hilo pia zimetuma wasanii wake. Waziri wa utalii na utamaduni wa Uturuki Bw. Attila Koc aliyeongoza kundi lake la wasanii la taifa kushiriki tamasha hilo alisema, China ikiwa ni nchi kubwa katika bara la Asia inapaswa kutoa mchango mkubwa zaidi katika kustawisha ushirikiano wa utamaduni. Alisema, "Napongeza sana tamasha hili, China ikiwa kwenye upande mmoja wa njia ya hariri na Uturuki ikiwa kwenye upande mwingine wa njia hiyo, zinapaswa kuimarisha ushirikiano. China inapaswa kuunganisha nchi zote ambazo zipo kwenye sehemu ilipopita njia ya hariri."

Licha ya michezo ya aina mbalimbali kutoka nchi za Asia, michezo kutoka sehemu mbalimbali humu nchini China pia ilioneshwa katika tamasha hilo. Opera ya Kunqu ambayo imeorodheshwa na UNESCO katika kumbukumbu za urithi wa utamaduni duniani, opera ya Kibeijing, na opera za aina nyingine za kisehemu za China pia zilioneshwa. Mkuu wa kundi la wasanii la Malaysia Bi. Haniah Hassan alisema, tamasha hilo limewaleta wasanii wa nchi za Asia fursa nzuri ya mawasiliano ya utamaduni. Alisema, "China na Malaysia zimesaini mkataba wa mawasiliano ya utamaduni. Tumewahi kupokea makundi mengi ya wasanii katika tamasha la sanaa nchini Malaysia. Mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Malaysia sio tu yanahusu kuonesha michezo ya sanaa, bali pia yanahusu kuonesha mawasiliano mengine ya utamaduni. Tamasha la sanaa ni fursa nzuri kwa wasanii kuwasiliana na kubadilishana ujuzi wa usanii."

Mwenyeji wa tamasha hilo ni mji wa Foshan, ambao ni moja ya sehemu zenye hali nzuri ya kiuchumi nchini China na pia ni moja ya machimbuko ya utamaduni katika sehemu ya kusini ya China. Katika karne ya 16, mji huo pamoja na miji ya Zhuxian, Hankou na Jingdezhen ilikuwa ni miji minne maarufu kwa sanaa za vyombo vya kauri na picha za kusherehekea mwaka mpya wa Kichina. Kutokana na hayo, tamasha hili pia lilifanya shughuli nyingi za kuonesha utamaduni wa kusini mwa China ikiwa ni pamoja na picha za kukatwa, picha za kusherehekea mwaka mpya, sanaa za vyombo vya kauri, mashindano ya mbio za mashua na maonesho ya taa za jadi. Bw. Naeem Tahir wa kundi la wasanii la Pakistan alisema, michezo na maonesho, yote inasaidia sana kupanua upeo wa macho. Alisema, "Maingiliano ya utamaduni kati ya nchi za Asia yanasaidia maendeleo na maelewano, na maelewano yanasaidia kuongeza elimu, na elimu inasaidia kuleta amani na urafiki, tunatumai kuimarisha maingiliano ya utamaduni kwa aina na njia nyingi."

Pamoja na tamasha hilo, Baraza la Mawaziri wa Utamaduni pia lilifanyika na kulifanya tamasha hilo lifuatiliwe zaidi. Baraza hilo lilianzishwa kwa ushauri wa waziri mkuu wa China Wen Jiabao na pengine litafanyika kila mwaka wakati wa tamasha la sanaa. Baraza la mwaka huu lilitoa Taarifa ya Foshan, ikisema kuwa washiriki wa tamasha hilo wanadhamiria kuimarisha zaidi maingiliano na mazungumzo kati ya aina tofauti za utamaduni kwa msingi wa usawa na kunufaishana, ili kuongeza maelewano ya watu wa Asia na dunia nzima kuhusu utamaduni tofauti na kuimarisha maingiliano ya utamaduni ya kiserikali na kuhimiza wasanii na makundi ya sanaa kuingiliana. Tamasha la mwaka huu limetoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya utamaduni, kufanyika kwa baraza la mawaziri wa utamaduni pamoja na tamasha hilo kumeonesha nia ya China ya kuimarisha ushirikiano na matumaini yake mapya kwa utamaduni ya kikanda.

Naibu waziri wa utamaduni wa China Bi. Meng Xiaosi alisema kuwa serikali ya China inatilia mkazo kuhifadhi aina tofauti za utamaduni na kutetea maingiliano baina ya aina tofauti za utamaduni, ili kuondoa kutokuelewana, kuzidisha urafiki na kupata maendeleo ya pamoja ya watu wa mataifa yote duniani. Alisema, "Katika siku za usoni China itafanya juhudi kubwa zaidi kuimarisha tamasha la sanaa la Asia na baraza la mawaziri wa utamaduni, ili kustawisha maingiliano na maelewano ya utamaduni."

Ofisa huyo alisema, siasa, uchumi na utamaduni ni nguzo tatu muhimu katika ushirikiano na maingiliano kati ya China na nchi nyingine za Asia, na ushirikiano na maingiliano ya utamaduni yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kuzidisha urafiki na maelewano.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-28