Mkutano wa 11 wa nchi wanachama zilizosaini "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa" utafanyika kuanzia tarehe 28 mwezi Novemba hadi tarehe 9 mwezi Desemba huko Montreal, Canada. Katika muda wa mkutano huo utafanyika mkutano wa kwanza wa nchi zilizosaini "Mkataba wa Kyoto" wa kudhibiti utoaji hewa zinazoweza kusababisha kuongezeka kwa joto duniani wa nchi za viwanda, pamoja na "mkutano wa 4 wa viongozi wa serikali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa". Kufanyika kwa mikutano hiyo kunaonesha kuwa udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa unafuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa.
Kutokana na mpango uliowekwa, mkutano huo wa nchi wanachama zilizosaini "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa" zitajadili athari zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwa binadamu pamoja na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa dhidi ya mabadiliko hayo zikiwa ni pamoja na sera kuhusu utoaji wa hewa zinazoweza kusabaisha hali ya dunia kubadilika kuwa joto, utafiti na uhamishaji wa teknolojia ya kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa. Wawakilishi zaidi ya 8,000 kutoka nchi na sehemu zaidi ya 190 duniani watashiriki kwenye mkutano huo. Habari zinasema kuwa mawaziri wa mazingira wa nchi mbalimbali watashiriki kwenye mkutano wa siku 3 za mwisho ambapo wataeleza misimamo ya serikali yao kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa.
Toka kusainiwa rasmi kwa "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa" tarehe 21 mwezi Machi mwaka 1994, nchi karibu 190 zilizosaini mkataba huo zimejitahidi kadiri ziwezavyo kudhibiti utoaji wa hewa zinazofanya joto la dunia kuongezeka na kuzuia athari mbaya zinazoletwa na mabadiliko hayo kwa uchumi na jamii ya binadamu.
Mkutano wa mwaka huu wa nchi zilizosaini "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa mataifa" umefanyika katika mazingira magumu. Mwaka huu maafa mengi yalitokea ambayo yamesababisha vifo vingi na hasara kubwa ya mali kwa binadamu yakiwemo Tsunami iliyotokea mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, kimbunga cha Katrina na kimbunga cha Wilma vilivyozikumba nchi za Amerika ya kati na kaskazini kati ya Julai na Agosti mwaka huu pamoja na tetemeko la ardhi lililotokea mwezi Oktoba nchini Pakistan. Maafa hayo ya kimaumbile yanawafanya watu wafikiri, je ni kisasi kutoka kwa mazingira dhidi ya uharibifu wa binadamu? Endapo binadamu hatutachukua hatua halisi kuhifadhi mazingira ya asili, basi tutakabiliwa na maafa makubwa zaidi ya kimaumbile.
Mkutano wa kwanza wa nchi zilizosaini "Mkataba wa Kyoto" pia ni shughuli muhimu inayofuatiliwa na watu kuhusu mikutano itakayofanyika huko Montreal. "Mkataba ya Kyoto" ulipitishwa mwezi Desemba mwaka 1997 kwenye mkutano wa tatu wa nchi zilizosaini "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa" uliofanyika huko Kyoto nchini Japan, ukiwa na lengo la kudhibiti hewa zinazotolewa na nchi za viwanda zinazofanya hali ya dunia ibadilike kuwa joto. Lakini kutokana na msimamo wa kutowajibika wa serikali ya Bush ya Marekani, mkataba huo ulianza kufanya kazi rasmi mwezi Februari mwaka huu baada ya miaka minane kupita tangu uliposainiwa. Kutokana na mkataba huo, tokea mwaka 2008 hadi mwaka 2012 hewa za aina 6 ikiwemo carbon dioxide zinazotolewa na nchi za viwanda zitapungua kwa asilimia 5.2. Habari zinasema kuwa nchi zilizosaini mkataba huo zitakuwa na majadiliano wakati wa mkutano huo kuhusu namna ya kufikia kiwango hicho kabla ya mwaka 2012.
Vyombo vya habari vimesema kuwa ingawa hadi mwaka huu mkutano kuhusu "Mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa" umefanyika mara 11, lakini hali halisi bado siyo ya kuridhisha, hadi hivi sasa Marekani ambayo ni nchi inayotoa hewa nyingi zinazofanya hewa ya dunia kubadilika kuwa joto, bado haijaidhinisha "Mkataba wa Kyoto", licha ya hayo baadhi ya nchi nyingine zilizoendelea bado hazijapiga hatua katika kudhibiti utoaji wa hewa za aina hiyo, na kinyume chake zinatoa hewa za aina hizo nyingi zaidi kuliko zamani. Hivyo jumuiya ya kimataifa katika siku za baadaye inatakiwa kutilia mkazo katika vitendo halisi kuhusu udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa, siyo kujali utungaji na mazungumzo kuhusu nyaraka na kanuni hizo, bali ni utekelezaji wa ahadi na vitendo halisi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-11-28
|