Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-29 14:31:34    
Barua 1129

cri
Msikilizaji wetu Maluha Martin wa sanduku la posta 3021 Moshi Kilimanjaro Tanzania anasema katika barua yake kuwa jambo mojawapo ambalo limemfanya akae chini na kuandika waraka huu, ni kutupa hongera na kutupongeza kwa kuweza kufanya marekebisho katika vipindi vinavyorushwa na Radio China kimataifa. Anasema anapenda kutushukuru kwa kuongeza muda wa matangazo yetu, kwa sababu hiyo sasa wamepata muda mwingi wa kusikiliza matangazo kutoka Radio China kimataifa kuliko zamani, kwani hapo matangazo yalikuwa ni nusu saa tu, si hivyo tu bali kwa mfano katika kipindi cha sanduku la barua au salamu zenu, salamu zinazosomwa hivi sasa ni nyingi kuliko za kipindi kilichopita, kwa hilo pia anapenda kutupongeza.

Jambo lingine ambalo limemfanya kuandika waraka huu ni kutaka kutufahamisha kuwa, anasikitika sana kwa kupoteza bahati yake kwani hakuweza kushiriki kwenye shindano zuri tulilowaandalia wasikilizaji wetu, la chemsha bongo ambalo linafanyika kila mwaka. Hii ni kwa sababu anashindwa kusikiliza kila siku matangazo yetu kutokana na sababu mbalimbali, na kutokuwa na uwezo wa kujibu maswali ya chemsha bongo, kwa kweli amejisikia vibaya. Lakini anasema mwakani baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita mnamo mwezi wa pili atakuwa huru kushiriki kwenye shughuli zote na matangazo yote tutakayokuwa tukitangaza.

Anachosisitiza kwetu ni kwamba hawezi hata siku moja kuiacha Radio China kimataifa, kwani ametokea kuvutiwa nayo sana, anaweza kusema hajaona kama Radio China kimataifa. Tunamshukuru sana kwa urafiki wake kwa Radio China kimataifa.

Msikilizaji wetu Albert M. Anari wa sanduku la posta 2995 Kisii Kenya ametuletea barua akisema kuwa, yeye huko Kisii, Kenya anapokea matangazo ya Radio China kimataifa kwa njia iliyo safi kabisa na wanatupa pongezi kubwa kutokana na vipindi vyetu na matangazo yote kwa ujumla. Yeye huko Kisii katika shule yake ya upili ya Mokwerero amefungua klabu ya Radio China kimataifa inayoitwa CRI listeners club, yeye ni mwenyekiti wa klabu hiyo, ameandika majina ya wanachama wake, lakini kwa kweli, baadhi ya majina ni vigumu kuthibitisha, kwani Bwana Albert ameandika baadhi ya herufi kama amechora, ingawa mwandiko wenyewe ni mzuri, lakini kwa sisi hasa mimi mchina ni vigumu kuweza kufahamu ni herufi gani alizoandika. Lakini majina yote tumeyapata.

Bwana Albert anasema yeye akiwa mwanachama wa Radio China kimataifa anatuomba tuende hapo kwake Kisii Kenya kuwatembelea na kujionea utamaduni wa Kisii, na kama tutaweza kutembelea huko, tutaona milima na mabonde yaliyo katika upande wa Kisii Kenya, vilevile kujionea jinsi kaka yake anavyochora michoro ya wanyama pori kama simba, ndovu, milima, pundamilia, nyati, twiga, na ndege walioko kwenye ziwa, tena hajui kama zile picha aliyotutumia kwa njia ya posta tumezipokea au la.

Hapa tunapenda kumwambia kuwa, tumepata picha aliyotutumia, na tunamshukuru kwa dhati.

Na Bwana Albert anasema, amesikiliza na kujibu maswali ya kipindi cha chemsha bongo cha mwaka huu na tena hajui kama atakuwa mmoja wa wale watakaopewa tuzo maalum ya kuitembelea China, lakini yeye amependezewa na China kwa kuwa ni moja ya nchi zinazoendelea inayopata maendeleo ya kasi anaipongeza kwa mafanikio hayo.

Msikilizaji wetu Francis Mulera Keya ambaye barua yake huhifadhiwa na John Amwayi Atenya wa sanduku la posta 3448 Nakuru Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu na kutupongeza kwa jarida dogo la daraja la urafiki, kwa sababu linawaunganisha wasikilizaji na marafiki wengi wa duniani, kama vile Oman Uarabuni, Tanzania, China, Uganda, Malawi na pia vijiji vidogo kama vile Tabora, Tarime, Butere, Khwisero, Nyeri, na hata Mombasa. Anatupa hongera kwa kazi nzuri tunayofanya kujulia hali na historia baadhi ya sehemu hizo.

Anasema kwa hivi sasa Radio China kimataifa imewafundisha mengi sana na pia kuwafanya wafahamiane na watu wengi duniani kama Said Awadi wa Misri, Mutanda Ayub Shariff wa Tanzania na Fraz Manko Ngogo na msichana ndogo wa miaka 9 shabiki wa kimataifa pamoja kumjua Bwana Fadhili Mpunji wa Radio China kimataifa. Anasema anaomba dunia iwe na amani pia. Na kutokana na kuliona jarida dogo walikuwa kama wametembelea Radio China kimataifa, na kuvutiwa sana na jinsi wanyama 12 walivyoelezewa. Anasema alifurahi pia kwa sababu baadhi ya hao wanyama pia huko Kenya wanatumika kama wanavyotumika China. Vilevile anasema alifurahishwa na habari kuhusu chai nzuri iliyotengenezwa Hangzhou, China, pia kujua mapishi ya hali ya juu ya kichina, pongezi nyingi kwa Radio China.

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anapenda kutumia fursa hii ili kuipa hongera nyingi na mwanana usio kifani Radio China kimataifa, hususan naibu mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa pamoja na mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji la Kenya KBC, kwa kutia saini ya makubaliano ya kuongezwa muda wa matangazo ya idhaa mbili za kigeni zinazotangazwa na Radio China kimataifa, yaani Idhaa ya Kiswahili na idhaa ya kiingereza, ambazo zitakuwa zinatangaza kila siku kwa muda wa saa moja kwa kila idhaa.

Anasema kutiwa saini kwa makubaliano hayo kuhusu kuongezwa muda wa matangazo ya Radio China kimataifa ya idhaa ya Kiswahili na idhaa ya kiingereza kati ya naibu mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa na mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji la Kenya KBC Nairobi yalifanyika tarehe 4 Septemba mwaka 2005, ambayo yalifanyika katika mji wa Beijing China, ambapo mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji la Kenya KBC alikuja Beijing, China kwa ziara ya wiki moja. Kwa hiyo anapenda kuwapa hongera sana wakuu wa Radio China kimataifa na mkuu wa shirika la utangazaji la Kenya KBC kwa hafla yao hiyo waliyoifanya mjini Beijing China iliyokuwa ikihusu kuongezwa kwa muda wa matangazo kwa idhaa ya Kiswahili na idhaa ya kiingereza zinazotangazwa na Radio China kimataifa.

Anasema kwa hiyo maoni yake anaomba Radio China kimataifa iwe inaanza kutangaza muda wa saa kumi na moja kamili mpaka saa kumi na mbili kamili kwa saa za Afrika ya mashariki kupitia masafa ya kati huko Nairobi Kenya, kwenye shirika la utangazaji la Kenya KBC. Na amefurahi sana kusikia kuwa kipindi cha salamu zenu na kipindi cha burudani ya muziki kuwa vimeongezwa muda. Vilevile pia anafurahia mabadiliko yaliyopo kwenye baadhi ya vipindi kama vile ijue China, kuwa nami jifunze kichina, safari nchini China, klabu ya utamaduni, sayansi na teknolojia, wapenzi wa michezo na kadhalika.

Na msikilizaji wetu Mogire O. Machuki wa Kijiji cha Nyankware sanduku la posta 646 Kisii Kenya anasema katika barua yake kuwa, mwaka 2005 unaelekea ukingoni na bila shaka Radio China kimataifa idhaa ya Kiswahili imekuwa mbioni kurekebisha taratibu za matangazo yake. Tangu tarehe 1 Septemba mwaka 2005, amekuwa akifuatilia matangazo yetu kwa karibu na kwa makini, tarehe 6 Septemba mwaka 2005 baada ya Bw Fadhili Mpunji kusoma taarifa ya habari, maelezo baada ya habari yalimulika uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na taifa la watu wa China, vipengele muhimu kwenye maelezo hayo vililenga mabadiliko ya hali ya hewa, ushirikiano katika sekta mbalimbali, mapambano dhidi ya ugaidi, mapambano kati ya makundi mbalimbali, maendeleo endelevu na mengine mengi. Baadaye kilifuata kipindi cha yaliyojiri Barani Afrika ambapo mama Chen wa Radio China kimataifa aliripoti kuwa kikosi cha kulinda amani cha Afrika ya kusini nchini Burundi chamaliza kazi yake, ni shukrani za dhati kwa kutoa kipaumbele kwa habari za Afrika.

Bwana Machuki anasema, vipindi vya siku hiyo vilikuwa vya aina yake na hatua ya Radio China kimataifa kuzidisha muda wake hadi saa moja, anaona ni wazo zuri. China ni taifa la kuigwa hususan kwenye karne hii ya utandawazi na teknolojia. Radio China kimataifa ni kituo ambacho daima wanakienzi na kukithamini. Hivyo anataka tusichoke kuwapasha mambo mbalimbali kuhusu China.

Tunamshukuru sana Bwana Mogire Machuki kwa barua yake ya kuhusu usikilizaji na maoni yake juu ya vipindi vyetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-29