Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-30 19:05:26    
Baraza la mawaziri wa elimu wa China na Afrika latoa taarifa ya Beijing

cri

Mawaziri wa elimu kutoka nchi 18 waliohudhuria kwenye Baraza la Mawaziri wa Elimu la China na Afrika tarehe 27 walitoa taarifa ya Beijing.

Taarifa hiyo inasema, mawaziri wa elimu walioshiriki kwenye baraza hilo walibadilishana maoni na walijadiliana na kutafiti kwa kina mkakati na utekelezaji wake wa kustawisha elimu katika nchi zinazoendelea. Mawaziri wa elimu walisisitiza kwamba elimu ni jiwe la msingi la maendeleo ya jamii, na kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya elimu ni njia ya lazima ya kustawisha taifa.

Mawazo yaliyofikiwa kwenye taarifa hiyo yakiwa ni pamoja na kwamba, kupata elimu ya msingi ya lazima ya bure ni haki ya kimsingi ya binadamu; elimu ipewe kipaumbele na kutoa nafasi za kutosha za elimu kwa usawa iwe sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo ya taifa, upungufu wa nyenzo za elimu unaendelea kuwa ni moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo ya elimu vinavyokumba nchi zinazoendelea; kutoa nafasi za kutosha zilizo sawa kwa wote bado ni jukumu kubwa la nchi zinazoendelea; nchi zinazoendelea zinapaswa kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya elimu ya msingi kadiri ziwezavyo; na sambamba na kueneza elimu ya msingi kwa hatua madhubuti siku hadi siku, na kuzingatia kuinua ubora wake; na kujenga mfumo unaolingana na hali halisi ya taifa sawia na kutumia mitindo iliyo bora ya kimataifa.

Kadhalika, taarifa inasisitiza kuwa, nchi zinazoendelea zinapaswa kutunga kwa makini sera za elimu ya ufundi na utekelezaji wake, na kujitahidi kuanzisha uhusiano mpya wa kiwenzi kati ya viwanda na elimu hiyo ili kuunganisha elimu na kazi halisi, kupanua elimu na kuongeza uzalishaji mali; elimu ya juu ipanuliwe na kuongezwa ubora ili kuandaa watu wenye taaluma ya juu na kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi. Taarifa inaona kwamba hii ni njia muhimu ya kuziwezesha nchi zinazoendelea kupata maendeleo endelevu.

Taarifa pia inatetea kwamba elimu lazima iwe ya aina nyingi, na lazima kulinda utamaduni wa aina tofauti na kuufanya uwe utamaduni duniani ili kuimarisha mapatano na uvumilivu wa kijamii. Katika mchakato wa utandawazi duniani, nchi zinazoendelea zinapaswa kuimarisha maingiliano na ushirikiano wa kielimu na kupitia maingiliano hayo kuzidisha maelewano ya aina tofauti za utamaduni, hasa utamaduni wa mataifa tofauti ili kuimarisha hali ya kuishi pamoja kwa amani na mazungumzo yenye haki sawa.

Aidha, taarifa inasema kwamba baraza la mawaziri wa elimu wa China na Afrika ni aina mpya ya ushirikiano wa pande nyingi kati ya China na Afrika, ni jukwaa muhimu lililojengwa na China na Afrika juu ya msingi wa usawa na kunufaishana, ni shughuli muhimu ya nchi zinazoendelea za kupigania maendeleo ya elimu. Mawaziri wa elimu wa China na Afrika wamesema, wataendelea kufanya juhudi kuimarisha maingiliano na ushirikiano wa kielimu katika siku za usoni. Baada ya mkutano wa baraza hilo, nchi mbalimbali zitaendelea kufanya majadiliano ya pande nyingi ili kuandaa mpango wa utekelezaji kuhusu maingiliano na ushirikiano wa kielimu kati ya China na Afrika.