Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-01 21:07:06    
Bi. Bahargul aliyestaafu kuanzisha shule ya kazi za kiufundi

cri

Bi. Bahargul alikuwa mwalimu kwenye mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, kaskazini magharibi mwa China. Baada ya kustaafu, tofauti na watu wengine wa rika lake waliopumzika nyumbani na kujiburudisha kwa kutalii hapa na pale, yeye alianzisha shule ya kazi za kiufundi kwa kukusanya fedha.

Bi. Bahargul mwenye umri wa miaka 55 alistaafu zaidi ya miaka mitatu iliyopita, baada ya kufanya kazi ya ualimu kwa miaka 25. Anajua kuwa, mkoa wa Xinjiang una upungufu mkubwa katika sekta ya elimu ya kazi za kiufundi, watu wengi wanashindwa kupata kazi kutokana na kutokuwa na ufundi maalum. Baada ya kuzingatia vya kutosha, aliamua kuanzisha shule ya ufundi huko Urumqi, mji mkuu wa Xinjiang kwa kukusanya fedha kutoka kwa pande mbalimbali, ili kutoa mafunzo ya ufundi kwa watoto wa makabila madogo madogo wanaotarajia kujifunza ufundi na wenye matatizo ya kiuchumi.

Katika muhula ya kwanza shule ya Bi. Baharguli iliwaandikisha wanafunzi ambao walikosa ajira na wenye matatizo ya kiuchumi. Ili kupunguza mzigo wa wanafunzi hao, Bi. Bahargul aliwapunguzia au kuwafutia kabisa ada zao. Akisema:

"Kila mtu anatakiwa kufanya shughuli fulani zenye umuhimu kwa jamii, nitakuwa na furaha kubwa nikiona wanafunzi wangu wanapata kazi na kujiunga na jamii kwa mafanikio."

Bw. Sayircan aliwahi kusoma katika shule ya ufundi ya Bi. Bahargul. Yeye ana watoto wawili na alikuwa hana kazi. Familia yake yenye watu wanne wanaishi kwa kutegemea msaada wa serikali. Alijiandikisha kujifunza ufundi wa kutengeneza vyombo vya umeme vya nyumbani, wakati mwingine alikuwa anaenda darasani hata bila kula chakula kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.

Baada ya kujua taabu yake Bi. Bahargul hakumtoza ada yoyote Bw. Sayircan, na pia alimsaidia kifedha mara kwa mara. Kutokana na msaada wa Bi. Bahargul na walimu wengine wa shule hiyo, Bw. Sayircan alimaliza masomo yake na kuanza kuendesha duka la kutengeneza vyombo vya umeme vya nyumbani. Hivi sasa biashara yake inaendelea motomoto, na anaishi maisha mazuri.

Mwezi Agosti mwaka huu, Bi. Bahargul alipotoa mhadhara katika sehemu ya kusini ya mkoani Xinjiang alipata habari kuwa, watoto yatima 20 walionusurika katika tetemeko la ardhi walishindwa kuendelea na masomo yao baada ya kumaliza shule ya sekondari. Ili kuwasaidia watoto hao yatima, Bi. Bahargul aliamua kuwaandikisha katika shule yake ili kuwafundishia kazi za kiufundi. Akisema:

"Nilipokwenda kuwapokea watoto hao kwenye kituo cha garimoshi, watoto wote walinikumbatia na kuahidi kuwa, watatumia vizuri fursa hii na kusoma kwa bidii. Mimi nimetiwa moyo sana, sikuwa na la kufanya ila tu kujaribu kuwaandaa watoto hao wawe watu watakaotoa mchango kwa jamii."

Bi. Bahargul si kama tu aliwafundishia watoto hao kazi za kiufundi, bali pia aliwatunza kama mama yao. Mvulana wa kabila la wauygur mwenye umri wa miaka 18 Bw. Mavulan alisema:

"Siku moja niligunduliwa kuwa na upungufu wa damu, nililazimika kulazwa hospitalini kwa siku tatu. Bi. Bahargul alipoambiwa kuwa nimelazwa alininunulia chakula na kunitunza hospitalini kwa siku tatu usiku na mchana."

Bi. Bahargul anapanga masomo ya wanafunzi wake kutokana na matakwa yao. Kwa mfano wasichana wanapenda kujifunza ufundi wa kushona nguo. Bw. Mawulan alitaka kujifunza ufundi wa kutengeneza vyombo vya umeme vya nyumbani. Baada ya miezi miwili, sasa amejua namna ya kutengeneza friji, televisheni na mashine za kufua nguo. Bi. Bahargul ametoa mchango mkubwa kwa watoto hao, na juhudi zake zimepata matokeo mazuri. Msichana Asyia alitunga shairi maalum kueleza upendo wake kwa Bi. Bahargul:

Shairi hilo linasema kuwa, wazazi wetu wamezikwa chini ya ardhi kutokana na tetemeko la ardhi, tumekuwa watoto yatima. Lakini kwa bahati nzuri tumempata mama mwingine mwenye roho ya malaika, jina lake ni Bahargul, yeye si kama tu anatusaidia kimaisha, bali pia anatufundisha ujuzi.

Katika miaka mitatu iliyopita, watu zaidi ya 3600 wamehitimu kutoka kwenye shule ya kazi za kiufundi ya Bi. Bahargul. Karibu wote wamefaulu kupata ajira mpya, na maisha yao yameboreshwa kidhahiri. Mshauri wa shule hiyo Bw. Maimatcan alisema:

"Wale waliopata tena ajira hurudi shuleni kumtembelea Bi. Bahargul na walimu wengine wakileta zawadi. Hali hii imetulia moyo sana na tumedhamiria kuwafuatilia watu wenye matatizo ya kiuchumi."

Idhaa ya kiswahili 2005-12-02