Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-05 16:37:25    
Safari ya utalii kwenye "njia ya hariri" ya kale

cri

Njia ya hariri ilikuwa ni njia ya biashara katika zama za kale, ambayo ilipita bara la Asia na Ulaya, hadi leo imekuwa na miaka zaidi ya 2,000. Njia hiyo ilianzia kwenye mji wa Xi'an na kupita mikoa ya Shaanxi, Gansu, Ningxia, Qinghai na Xinjiang nchini China na baada ya kupita Jumuyia ya Madola Huru, Afghanistan, Iran, Iraq na Syria ilifika kwenye ukingo wa bahari ya Mediterranean, kutoka hapo bidhaa za hariri za China zilisafirishwa hadi kwenye nchi za Ulaya, jumla ilikuwa na safari kilomita 7,000. Katika safari hiyo karibu nusu yake ilikuwa nchini China. Ingawa njia hiyo iliacha kutumika tangu zamani, lakini shughuli za biashara zimeacha miji mingi na kumbukumbu nyingi za hostoria kwenye njia hiyo. Hii ndio sababu ya kuwavutia sana watalii kutoka nchi za nje kwa siku zote.

Urumqi ni mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, ulikuwa mji muhimu kwenye njia ya hariri. Watalii wakitembea kwenye barabara mjini humo watasikia harufu nzito ya mshikaki na pilau na kuona wazee waliovaa baraghashia na wasichana waliovaa kama shela wa kabila la Wauygur, na kelele za kutangaza biashara zinasikika kutoka magengeni......kwenye mazingira hayo watajikuta kama wako kwenye gulio la zama za kale.

Mwanafunzi uzamili wa kozi ya historia katika Chuo Kikuu cha Beijing Bi. Niu Diandian analikumbuka sana gulio hilo, alisema,

"Nakumbuka sana safari kwenye njia ya hariri, lakini ninalokumbuka zaidi ni gulio mjini Urumqi. Wenyeji wa huko, wanaume na wanawake, wazee na watoto, wote walivaa na kujipamba vizuri, wanawake wa Kiislamu walivaa hijabu wakitembea tembea gulioni. Kwenye magenge ya chakula watalii wanaweza kupata vyakula vya udohodoho vya kila aina vya kabila la Wauygur; na kuchagua hariri za rangi mbalimbali."

Bi. Niu Diadian alisema, kitu anachokumbuka na hawezi kukisahau ni tunda la pea la Kurle katika mkoa huo Xinjiang. alisema, tunda hilo ni tamu sana hata ukila njiani unafuatwa na nyuki!

Katika sehemu ya Kurle pea zinapokomaa, utaona miti mingi iliyozaa matunda mengi mashambani na nyumbani kwa wenyeji. Upandaji wa miti hiyo katika sehemu ya Kurle umekuwepo kwa miaka 2,000, wenyeji wanasema, miti hiyo ikipandwa katika sehemu nyingine haizai matunda matamu kama ya Kurle, lakini miti ya sehemu nyingine ikihamishswa katika sehemu ya Kurle matunda yatakuwa matamu, watu wakafahamu kuwa sababu yenyewe ni udongo na hali ya hewa ya Kurle.

Licha ya kuwa mila na desturi ya kabila la Wauygur zinawafanya watalii kujiona kama wako katika ulimwengu mwingine kabisa, kwenye njia ya hariri kuna mandhari na kumbukumbu nyingi za kale.

Kwenye njia ya hariri kuna mandhari nyingi na za ajabu kwenye mikoa ya Qinghai na Xinjiang. Kwa mfano, ziwa la chumvi na kisiwa cha ndege katika ziwa la Qinghai, bata wenye shingo ndefu katika mbuga za majani, "ziwa la mbinguni" kwenye kilele cha mlima wa Tianshan, na mlima wenye joto kali huko Turufan na sura ya ajabu ya ardhi iliyolika kutokana na upepo kwenye sehemu ya Kramai.

Kwenye njia ya hariri, mandhari kwenye bonde la Mto wa Kuche ni ya pekee. Mji wa Kuche uko katika sehemu ya kusini ya mkoa wa Xinjiang, ambao ni mji muhimu kwenye njia ya hariri. Maji ya theluji iliyoyeyuka mlimani Tianshan yanakwenda kasi miaka na miaka yalipasua majabali kuwa magenge mengi makali, lakini yalipofika kwenye mji wa Kuche mwendo ukapungua na kugawanyika kuwa mifereji mingi na mwishowe ikapotea jangwani.

Hivi leo kwenye bonde la Mto Kuche kuna megenge kama ukuta na majabali mengi ya misonge yenye rangi nyekundu. Wakati jua linapozama mwangaza mwekundu wa jua unafanya magange hayo yaonekane kama miujiza. Mwongozaji watalii Bw. Li Wenjun aliwaambia waandishi wa habari, kwenye bonde la mto Kuche watalii hawakuona mandhari ya maumbile peke yake. Alisema,

"Kwenye bonde hilo kuna kumbukumbu nyingi za kale na mapango ya kale, kama vile mji wa kale wa Dagu uliopo jangwani, na mapango yenye sanamu elfu moja za Buddha na mahandaki ya kuwashia moto wa kutangaza habari ya hatari katika zama za kale."

Licha ya mapango hayo, mji wa kale na mahekalu ya kale, pia kuna mji wa Dunhuang ambao ulikuwa mji muhimu katika njia ya hariri mkoani Gansu.

Mji wa Dunhuang ulikuwa ni mji wa kukutanisha tamaduni za Mashariki na wa Magharibi, wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali walikutana huko wakiwa na ngamia waliofunga kengele shingoni. Pango maarufu Mogaoku liko mlimani Mingsha mbali na Dunhuang kwa kilomita 25 upande wa kusini mashariki. Kwenye magenge yenye safari ya kilomita 1,600 yalichongwa mapango zaidi ya 600, na kati ya mapango hayo, mapango 469 yalichorwa picha kutani na sanamu ndani. Kutokana na uchunguzi, mapango hayo yalianza kuchongwa katikati ya karne ya nne, na katika muda wa miaka zaidi ya elfu moja baadaye mapango yaliendelea kuchongwa.

Siku zote watalii wanavutiwa na safari kwenye njia ya hariri. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, kutokana na ombi la watalii wa Japan, Shirika la Utalii la China limefungua njia hiyo ya hariri kwa watalii. Tokea hapo utalii katika njia hiyo unawavutia watalii wengi, licha ya watalii wa Japan, na pia watalii kutoka Ulaya na Marekani.

Meneja wa Shirika la Utalii la China Bw. Ji Xiaobu alieleza,

"Kwa sababu kwenye njia hiyo kuna mambo mengi ya kuvutia, na safari yenyewe ni ya ujasiri, furaha walizopata watalii kwenye njia hiyo hazitasahaulika maishani."

Idhaa ya kiswahili 2005-12-05