Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-05 16:31:56    
Mwongozaji wa michezo ya TV Zhang Jizhong

cri

Bw. Zhang Jizhong anajulikana sana kwenye fani ya michezo ya TV kwa wote kwani michezo yake mingi inawavutia sana watizamaji.

Mchezo wa "Madola Matatu ya Kifalme" ulitengenezwa kwa mujibu wa riwaya yenye jina hilo, unaeleza mapambano ya kijeshi na ya kisiasa kati ya madola matatu ya Wei, Shu na Wu katika karne ya tatu nchini China. Mchezo huo una sehemu 84, mazingira ya vita vilivyopiganwa na watu wengi na jinsi wahusika walioelezwa kwa kina viliwaingia sana watazamaji akilini. Mwongozaji alipokumbuka utengenezaji wa mchezo huo alikuwa na mawazo mengi. Alisema, katika siku za kutengeneza mchezo huo aliongoza waigizaji karibu mia moja kwenda huku na huko kiasi cha kilomita elfu kadhaa nchini China, alikumbwa na matatizo mengi. Alisema,

"Ili kupta mazingira yanayofaa tulisafiri karibu nchi nzima, tulifika sehemu ya kaskazini kupiga picha ya hali ya vita vya askari wapanda farasi, tulisafiri hadi sehemu ya kusini ili kupata mazingira yenye ndovu, na tulisafiri hadi mashariki na magharibi mwa China ili kupata mazingira yanayolingana na riwaya iliyoyaelezea. Tulipata matatizo mengi katika safari hizo."

Zhang Jizhong ana umri wa miaka 54. Tangu alipokuwa mtoto alipenda sana michezo ya sanaa, alitamani kuwa mwigizaji. Lakini mapinduzi ya utamaduni yaliyofanywa motomoto mwaka 1966 nchini kote China yaliharibu ndoto yake, kama ilivyokuwa kwa vijana wengi, alipelekwa vijijini mkoani Shanxi. Huko alikuwa akifanya kazi za kilimo, kuwa kibarua wa ujenzi na kuishi pamoja na wakulima, maisha yalikuwa magumu na ni mbali sana na tumaini lake alilokuwa nalo utotoni. Alisema,

"Katika majira ya baridi hakuna kazi ya kilimo, tulitumwa kutengeneza barabara, wakati huo tulipata nafasi ya kuona mji wa wilaya ulivyo. Kila siku tulikuwa tunakula mikate ya sembe na unga wa mtama, nilikaribia kushinwa kuvumilia, nilitamani sana kula tambi mjini. Siku moja baada ya kazi nilisafiri zaidi ya kilomita 10 na kufika mjini nikapata chakula cha tambi, kisha nikarudi vijijini nikiwa na furaha tele moyoni."

Maisha ya vijijini yalikuwa magumu, lakini hayakutikisa nia yake ya kuwa mwigizaji wa michezo ya sanaa. Baada ya mapinduzi ya utamaduni kumalizika, alijiunga na kundi la tamthilia la mji wa Xi'an na katika tamthiliya ya "Tukio la Xi'an" aliigiza kama mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu. Baadaye alipata nafasi za kuigiza katika filamu na michezo ya TV. Ingawa kwa mara nyingi alichaguliwa kuwa mchezaji mkuu lakini alijikuta anaweza kuwa hodari zaidi katika uongozaji wa michezo, na kweli baadaye akawa mwongozaji.

Baada ya kutengeneza mchezo wa "Madola Matatu ya Kifalme", mwaka 1994 alikuwa mwongozaji wa mchezo wa "Mashujaa kwenye Vinamasi". Huu ni mchezo unaoeleza mashujaa wenye hulka tofauti katika uasi wa wakulima uliotokea mwanzoni mwa karne ya 12. Bw. Zhang Jizhong alieleza vilivyo hadithi zilizojulikana kwa wote na kuonesha kwa kina mashujaa katika hadithi hizo. Mchezo huo ulipooneshwa katika TV uliwafanya watazamaji wengi majumbani waangalie, na wimbo katika mchezo huo mara ukaenea kila mahali nchini China.

Mwishoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, michezo ya kung fu ilikuwa mingi katika michezo ya TV, wakati huo Zhang Jizhong aliyependa hadithi za kung fu alikuwa na hamu ya kutengenza michezo ya aina hiyo.

Licha ya kutengeneza michezo ya riwaya za kale za China, Zhang Jizhong pia alitengeneza michezo mingi ya TV ya hadithi za siku hizi. Mwaka 2002 alimaliza mchezo wa TV wa "Miaka ya Hisia Iliyowaka". Hii ni hadithi ya kueleza mume na mke wanajeshi toka walipokuwa ugenini hadi kupendana na kuwa mume na mke wa dhiki na faraja. Mchezo wake mwingine unaozungumzia jamii ya hivi leo ni "Kibarua kutoka Vijijini", ukieleza mkulima aliyefanya kazi ya ujenzi mjini jinsi alivyokumbwa na matatizo na mikasa mjini. Kwa kupitia mchezo huo ameonesha shukrani zake kwa wakulima waliotoa mchango katika ujenzi wa mji na kumbukumbu zake alipoishi vijijini alipokuwa kijana.

Kuhusu kuchagua waigizaji, Bw. Zhang Jizhong ana kigezo chake. Anaona kuwa, mwigizaji hodari sio tu awe na sura inayolingana na mhusika aliyeelezwa katika hadithi bali pia lazima awe na uhodari wa kuigiza, alisema,

"Waigizaji lazima waridhishe mahitaji ya mchezo wenyewe, mwigizaji fulani asipoweza kucheza kama anavyotakiwa, nitambadilisha, kufanya hivyo ni kuwajibika kwa watizamaji."

Bw. Zhang Jizhong aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mke wake pia ni mwongozaji wa michezo, maishani wao ni wanandoa, na katika kazi ni wasaidizi.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-05