Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-05 16:19:39    
Uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa Hariri kuanza upya

cri

Maofisa watano wa Syria wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kuuawa kwa waziri wa zamani wa Lebanon tarehe 4 walisafiri kwenda Vienna kwenye ofisi ya Umoja wa Umoja wa Mataifa ili kuhojiwa. Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na shahidi mmoja muhimu kubadilisha ushahidi wake, mkuu wa tume ya uchunguzi ya kimataifa Detlev Mehlis huenda atajiuzulu, na uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa Bw. Hariri huenda utaanza upya.

Tarehe 14 Februari, waziri wa zamani wa Lebanon Rafik al-Hariri aliuawa katika mlipuko wa bomu lililofichwa ndani ya gari. Kwa mujibu wa azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili, tume ya uchunguzi wa kimataifa inayoongozwa na Bw. Mehlis ilianza kuchunguza tukio hilo katikati ya mwezi Juni. Mwezi Oktoba Baraza la Usalama uliamua kurefusha muda wa uchunguzi hadi tarehe 15 Desemba.

Kazi ya kuwahoji watuhumiwa hao watano ilipangwa kuanza tarehe 5 mwezi huu. Kutokana na makubaliano kati ya Syria na Mehlis, maofisa hao watafuatana na mawakala wao kwenda Vienna na baada ya kumaliza kuwahoji wataweza kurudi nchini Syria moja kwa moja, tume ya uchunguzi ya kimataifa haina haki ya kuwazuia huko Vienna.

Mahojiano hayo yalipangwa kwa matakwa ya tume ya uchunguzi ya kimataifa baada ya kushauriana na Syria. Lakini kutokana na kuwa shahidi muhimu wa tukio hilo alibadilisha ushahidi wake mwishoni mwa mwezi uliopita na kukiri kwamba alitoa ushahidi wa uwongo uliodhuru Syria kutokana na vitisho na kuhongwa, ripoti ya Mehlis iliyokabidhiwa kwa Umoja wa Mataifa kuhusu tukio la Hariri mwezi Oktoba haiaminiki, kwa hiyo Syria inataka matokeo ya ripoti hiyo yapimwe upya. Hali ya kutoaminika kwa tume ya uchunguzi ya kimataifa imeiletea vikwazo kwenye kazi ya uchunguzi ambayo ilikuwa ikienda pole pole, hatima ya mkuu wa tume hiyo Bw. Mehlis inafuatiliwa sana.

Vyombo vya habari vya Ujerumani vilinukuu habari za Umoja wa Mataifa, vikisema kuwa Mehlis amekabidhi ombi lake la kujiuzulu kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan. Mehlis alisema kujiuzulu kunatokana na sababu binafsi, kwamba mwanzoni mwa mwaka kesho atateuliwa kuwa mwendesha mkuu wa mashitaka wa Ujerumani. Kuna maoni tofauti kuhusu habari ya kujiuzulu kwa Mehlis. Waziri mkuu wa Lebanon Fouad Siniora, jioni ya tarehe 3 aliwasiliana na Kofi Annan kwa simu akisema kuwa, serikali ya Lebanon inatumai Mehlis ataendelea na kazi yake mpaka mwisho. Na kwamba alitaka muda wa uchunguzi urefushwe zaidi kwa miezi sita au kwa mujibu wa hali itakavyokuwa ya uchunguzi. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa John Bolton alitumai kuwa Bw. Kofi Annan atamshawishi Bw. Mehlis aendelee na kazi yake "ili kuzuia Syria isiache ushirikiano kikamilifu na tume ya uchunguzi ya kimataifa kwa kutumia fursa ya mabadiliko ya kiongozi". Syria inaendelea kushikilia msimamo wake wa awali. Waziri wa habari wa Syria Bw. Dakhelallah alisema, Syria haina uhasama na Mehlis, na haijali nani ataongoza tume ya uchuguzi ya kitamaifa, lakini cha muhimu ni kuwa uchunguzi lazima ufanywe kwa utaalamu na uwe unaaminika, na usiwe wa kisiasa. Bwana huyo alisisitiza kwamba Syria haina kosa lolote katika tukio la kuuawa kwa Bw. Hariri na Syria imeshirikiana na itaendelea kushirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi ya kimataifa. Serikali ya Ujerumani imesema kuwa uchunguzi wa Mehlis umeacha njia yake ya kawaida na "utatishia maslahi yake katika Mashariki ya Kati".

Tarehe 15 Mehlis atawasilisha matokeo ya ripoti yake kwenye Umoja wa Mataifa, lakini kutokana na kukosa ushahidi bayana Mehlis atakuwa na hali ya kufedheheka. Vyombo vya habari vinaona kuwa bila kujali nani atakayeongoza tume ya uchunguzi ya kimataifa, kazi ya uchunguzi itaanza upya.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-05