Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-05 19:27:32    
(Maelezo husika)Ufaransa na Afrika zafanya ushirikiano ili kukabiliana na changamoto

cri

Mkutano wa 23 wa siku mbili wa wakuu wa Ufaransa na nchi za Afrika tarehe 4 ulifungwa huko Bamako, mji mkuu wa Mali. Rais Chirac wa Ufaransa na wakuu wa nchi au serikali za nchi 53 za Afrika walihudhuria mkutano na kufikia maoni mengi ya pamoja. Wachambuzi wanaona kuwa, huu ni mkutano muhimu wa Ufaransa na nchi za Afrika katika kuongeza ushirikiano na kukabiliana kwa pamoja na changamoto.

Watu waliohudhuria mkutano huo walibadilishana maoni kuhusu hali ilivyo ya uhusiano kati ya Ufaransa na Afrika, kuongeza misaada ya kiserikali ya nchi zilizoendelea juu ya maendeleo ya Afrika, kupunguza madeni, kutimiza lengo la maendeleo ya milenia.

Suala la wahamiaji ni suala kubwa linalozikabili nchi za Afrika na Ufaransa. Rais Chirac aliainisha kuwa, kwa upande wa Afrika, kupoteza kwa nguvu kazi ya vijana na makamo kumesababisha maendeleo ya uchumi wa Afrika yako nyuma. Na vijana wengi wa Afrika waliofika Ufaransa wanakabiliwa na ukosefu wa ajira na matatizo mengine mengi, pia kuleta matatizo mengi ya kijamii kwa Ufaransa, hata kusababisha hali isiyo ya utulivu kwa jamii, vurugu zilizotokea muda mfupi baadaye huko Paris zilihusiana kweli na ushiriki wa wahamiaji.

Rais Chirac anaona kuwa, umaskini wa nchi wanakoishi ni sababu kuu ya kuwafanya vijana wengi wa Afrika wahamie Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya. Hivyo jambo muhimu la kutatua suala la wahamiaji ni kuzisaidia nchi za Afrika katika kuendeleza uchumi na kuondokana na umaskini. Hivyo Rais Chirac ametangaza kuwa, misaada ya serikali ya Ufaransa kwa maendeleo ya Afrika itafikia asilimia 0.5 ya thamani ya jumla ya uzalishaji wa Ufaransa ifikapo mwaka 2007, na mwaka 2012 misaada hiyo itafikia asilimia 0.7 ya thamani ya jumla ya uzalishaji wa Ufaransa. Ufaransa pia imeamua kuongeza nyongeza za ushuru ndani ya tikiti za ndege kuanzia mwezi Julai mwaka 2006, na mapato ya ushuru huo yatatumiwa hasa kuzisaidia nchi maskini za Afrika. Wakati huo huo Rais Chirac amezitaka nchi nyingi zaidi ziige hatua za Ufaransa kuongeza misaada kwa nchi maskini za Afrika. Juu ya hiyo, wajumbe wa nchi nyingi za Afrika wamekubali. Rais Amadou Toure wa Mali pia amependekeza kuitisha mkutano kuhusu suala la wahamiaji kati ya Ulaya na Afrika, ili kujadili kwa kina utatuzi wa suala la wahamiaji.

Ingawa rais Gbagbo wa Cote d'ivoire hakuhudhuria mkutano huo, mgogoro wa nchi hiyo pia ulifuatiliwa na kujadiliwa zaidi kwenye mkutano huo.

Baada ya majadiliano, wakuu wa nchi na serikali za nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wameamua kwa kauli moja kuharakisha utatuzi wa mgogoro wa Cote d'ivoire ili kuepusha mgogoro kuleta hali isiyo ya utulivu kwa sehemu hiyo.

Zaidi ya hayo rais Chirac ameeleza wazi kuwa, Ufaransa inaunga mkono Umoja wa Afrika kuanzisha jeshi lake yenyewe la kulinda amani kabla ya mwaka 2010. Rais Chirac alisema, hivi sasa Ufaransa ina vituo vitano vya kijeshi barani Afrika na askari zaidi ya elfu 10, lakini jukumu la kulinda amani na usalama wa Afrika linahitaji Umoja wa Afrika uanzishe jeshi lake wenyewe.

Rais Chirac pia ameutaka mkutano wa mawaziri wa WTO utakaofanyika huko Hong Kong uzingatie zaidi maslahi ya nchi za Afrika. Alisema sera ya utoaji ruzuku kubwa za kilimo ya Marekani imedhuru maslahi ya wakulima wengi wa kawaida wa Afrika, na kusababisha umaskini kwa watu milioni kadhaa wa nchi za Afrika. Ameitaka Marekani ifute sera hiyo ya kutoa ruzuku za kilimo, ili kuanzisha utaratibu mpya wa kibiashara ulio wa haki na halali duniani.

Rais Toure wa Mali alieleza kuwa, nchi 33 barani Afrika zinalima pamba, lakini nchi zilizoendelea zinatekeleza sera ya kutoa ruzuku za kilimo, hivyo wakulima wa pamba wa Afrika wamekuwa maskini siku hadi siku. Wakuu wengine waliohudhuria mkutano pia wameutaka mkutano wa Hong Kong ubadilishe hali hiyo isiyo halali.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-05