Ofisa wa Wizara ya biashara ya China tarehe 5 hapa Beijing alisema kuwa, China inaunga mkono kithabiti na kufanya juhudi za kusukuma mbele mazungumzo ya Doha ya shirika la biashara duniani WTO, na kutarajia mkutano wa 6 wa mawaziri wa WTO utakaofanyika hivi karibuni huko Hong Kong utapata maendeleo halisi, aidha China inapendekeza kukamilisha mazungumzo ya biashara ya pande nyingi mwaka 2006.
Mkutano wa 6 wa mawaziri wa WTO utafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 18 mwezi huu huko Hong Kong. Huu ni mkutano muhimu katika mazungumzo ya Doha ya WTO. Mkurugenzi wa idara ya kushughulikia mambo ya WTO katika wizara ya biashara ya China Bwana Zhang Xiangchen tarehe 5 alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, China inapenda kufanya juhudi katika kusukuma mbele maendeleo halisi ya mkutano huo utakaofanyika huko Hong Kong. Akisema:
Tunaona kuwa pande mbalimbali zinazohusika zinapaswa kujitahidi kusukuma mbele mazungumzo ya Doha, ili matokeo ya mazungumzo hayo yaweze kuhimiza mchakato wa biashara huria duniani kote, na kuweza kutatua kihalisi ufuatiliaji wa nchi zinazoendelea. Tunaweza kufanya juhudi kadiri tuwezavyo ili kuhimiza mkutano huo uelekee kwa kupata matokeo halisi.
Mazungumzo ya Doha ni mazungumzo makubwa ya kwanza kuhusu biashara ya pande nyingi yaliyoanzishwa na shirika la WTO tokea shirika hilo lianzishwe mwaka 1995. Mazungumzo hayo yalianzishwa kwenye mkutano wa 4 wa mawaziri wa WTO uliofanyika huko Doha, mji mkuu wa Qatar mwezi Novemba mwaka 2001. Mazungumzo hayo yalithibitisha sekta 8 za mazungumzo kuhusu kilimo, ruhusa za kuingia kwenye soko la mazao yasiyo ya kilimo, na biashara ya huduma. Matokeo ya mazungumzo yatafanya kazi muhimu katika kuimarisha utaratibu wa biashara ya pande nyingi na kuhimiza ongezeko la uchumi wa dunia nzima.
Suala kuhusu kilimo ni mada kuu katika mazungumzo ya Doha, pia ni suala linalosababisha mkwaruzano kati ya pande mbalimbali. Ofisa wa wizara ya biashara ya China Bwana Zhang Xiangchen alisema, China inaona kuwa, hali ya upotovu iliyokuwepo kwa muda mrefu katika biashara ya mazao ya kilimo duniani inapaswa kurekebishwa kimsingi kwa kupitia mazungumzo. Akisema:
Tunatumai nchi kadhaa zilizoendelea hasa nchi zile zinazotoza ushuru mwingi wa forodha na kutoa ruzuku kubwa zitatangulia kufuta ruzuku kwa bidhaa zao zinazouzwa nje, kwani ruzuku hizo zimepotosha vibaya biashara ya mazao ya kilimo, na pia nchi hizo zitaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ruzuku zao kwa kilimo nchini na ushuru wa forodha.
Mbali na kilimo, Bwana Zhang Xiangchen pia alifahamisha msimamo wa kimsingi wa China kuhusu mazungumzo ya Doha.
Tokea China ijiunge na WTO mwaka 2001, imeshiriki katika mazungumzo ya Doha na kujitahidi kusawazisha msimamo na nchi wanachama husika. Ofisa huyo alisema:
Hii ni mara ya kwanza kwa China kushiriki kwenye mazungumzo ya biashara ya pande nyingi tangu China ijiunge na WTO. China ikiwa mwanachama mpya, pia ina ufuatiliaji wake halisi. Tunaweza kufahamisha pia msimamo wetu juu ya shughuli za China zenye hali dhaifu na idara zinazopaswa kulindwa, ili kueleweka na kuungwa mkono na nchi wanachama wengine. China inapenda kushirikiana na nchi wanachama wa WTO katika kujenga mazingira yenye usawa ya biashara duniani wakati inapolinda maslahi ya taifa.
|