Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao ambaye hivi sasa anafanya ziara nchini Ufaransa, tarehe 5 akitoa hotuba kwa wanaviwanda na wafanyabiashara nchini Ufaransa aliwafahamisha hali ya maendeleo ya uchumi wa China, umaalum mpya wa ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya China na Ufaransa, na kutoa mapendekezo kwa uendelezaji wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa nchi hizo mbili.
Katika miaka ya karibuni ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi mbili za China na Ufaransa umekuwa ukiendelezwa kwa hatua mfululizo, thamani ya biashara kati ya pande mbili mwaka huu inatarajiwa kuzidi dola za kimarekani bilioni 20. Hivi sasa Ufaransa imekuwa nchi mwenzi wa pili kwa ukubwa katika ushirikiano wa teknolojia kati ya China na Umoja wa Ulaya, nchi ya tatu kwa ukubwa katika uwekezaji vitega uchumi na ya nne kwa ukubwa katika shughuli za biashara. Alipogusia umaalum mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Ufaransa Bw. Wen Jiabao alisema,
"Kwanza, ushirikiano wa kimkakati umetiliwa mkazo zaidi, pili ni kupanuka zaidi kwa ushirikiano, tatu ni kustawi kwa ushirikiano kati ya viwanda vidogo na vya wastani, na nne ni maendeleo ya ushirikiano na kuwekeana vitega-uchumi kati ya viwanda vya nchi hizo mbili yameonekana."
Bw. Wen Jiabao pia alielezea ushirikiano wa kimkakati, na alisema kuwa serikali ya China inaunga mkono kujenga kinu cha majaribio cha nyukilia cha kimataifa nchini Ufaransa, kuimarisha ushirikiano na Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuhusu mpango wa Galileo, na aliongeza kuwa nchi hizo mbili zimepiga hatua kubwa katika ushirikiano wa teknolojia ya viumbe na kazi za viwanda vya ndege. Licha ya kuimarishwa kwa msingi wa ushirikiano wa nchi hizo mbili katika mambo ya uchumi na biashara zikiwemo za sekta za ndege, nishati na njia za reli, maendeleo makubwa pia yamepatikana katika sekta za kilimo, hifadhi ya mazingira, teknolojia ya kisasa na mawasiliano ya habari. Viwanda na kampuni za Ufaransa zilizoko nchini China zinajiendeleza hadi sehemu za kati, magharibi na kaskazini mashariki kutoka mwambao wa sehemu ya pwani ya kusini mashariki ya China.
Ili kuhimiza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Ufaransa kuingia katika kiwango kipya cha juu, na kutimiza lengo jipya la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa China na Ufaransa la kuongezeka maradufu kwa thamani ya biashara ya pande hizo mbili, yaani kufikia dola za kimarekani bilioni 40 katika miaka 5 ijayo, Bw. Wen Jiabao amependekeza nchi hizo mbili kuimarisha ushirikiano wa teknolojia ya kisasa, kuongeza uwekezaji wa vitega uchumi kati yao, kuinua kiwango cha ushirikiano wa utoaji huduma na biashara, kuendelea kuhimiza ushirikiano wa viwanda vidogo na vya wastani vya pande mbili na kuboresha mfumo wa mawasiliano na mazungumzo kati ya nchi hizo mbili. Alisema,
"China inapenda kuimarisha ushirikiano na Ufaransa katika sekta za nishati ya nyukilia, ndege na njia za reli. Vilevile tunatarajia kuinua kiwango cha ushirikiano wa nchi hizi mbili katika sekta za tekinolojia ya usafiri wa anga ya juu, uhandisi wa viumbe na tekinolojia ya mawasiliano ya habari. Hivi sasa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa China na Ufaransa umeendelezwa vizuri na kwa mfululizo, hata hivyo imetokewa mikwaruzano ya kibiashara katika baadhi ya sekta. Nchi hizi mbili zinatakiwa kuimarisha mfumo wa mazungumzo, kushughulikia ipasavyo migogoro ya kibiashara na kuhakikisha maendeleo mwafaka ya biashara ya pande hizo mbili."
Bw. Wen Jiabao anatarajia nchi wenzi wa shughuli za biashara za nchi zilizoendelea ziondoe vizuizi kwa bidhaa za kiteknolojia, na aliongeza kuwa China itatekeleza ahadi ilizotoa wakati ilipojiunga na Shirika la Biashara Duniani, WTO, kufungua masoko na kuboresha mazingira ya ushirikiano wa kimataifa katika shughuli za kiuchumi na kibiashara.
Idhaa ya Kiswahili 2005-12-06
|