Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-07 18:14:26    
WTO yapitisha makubaliano kuhusu nchi maskini kupata dawa za bei rahisi

cri

Nchi 148 za wanachama wa Shirika la Biashara Duniani, WTO tarehe 6 huko Geneva zilipitisha makubaliano ya kuziruhusu nchi maskini zisizo na viwanda kununua dawa za bei rahisi zisizolindwa na hataza ili kudhibiti maradhi yenye maambukizi makali.

Haki-miliki ya kielimu na afya za umma ni moja ya mada muhimu iliyozungumzwa kwenye mazungumzo ya Doha yaliyoanza mwaka 2001. Suala nyeti la mazungumzo hayo ni kuziwezesha nchi zinazoendelea za jumuiya hiyo kupata dawa kwa bei rahisi zinazotibu Ukimwi, malaria na kifua kikuu huku zikilinda haki-miliki ya nchi wanachama zilizoendelea katika uzalishaji wa dawa mpya. Watu wanaona kuwa suala linalohusika siyo la kibiashara tu, bali ni suala linalohusika zaidi na ubinadamu.

Nchi nyingi zinazoendelea zinapendekeza kufanya marekebisho juu ya vifungu vya "makubaliano kuhusu haki-miliki zinazohusika na biashara", kuongeza aina za dawa zisizolindwa na hataza ili kutatua tatizo la nchi wanachama wa WTO zisizo na uwezo wa uzalishaji wa dawa kukosa dawa za bei nafuu. Nchi zilizoendelea zenye kampuni nyingi kubwa za dawa zikiwemo Marekani na Uswisi zina wasiwasi kwamba hatua hiyo huenda italeta tishio kwa hataza ya dawa zake. Marekani iliwahi kupendekeza kuanzisha shirika la utoaji msaada kwa maradhi yenye maambukizi makubwa, ikitarajia kutatua mgongano kati ya afya za watu wa nchi zinazoendelea na ulinzi wa hataza za dawa kwa njia ya kuzidisha msaada wa fedha wala siyo kurekebisha "makubaliano ya haki-miliki zinazohusika na biashara.

Mwishoni mwa mwaka 2002, wakati nchi nyingi wanachama zilipokaribia kuafikiana kuhusu makubaliano yaliyorekebishwa, mwakilishi wa Marekani alisema kutokana na kulegezwa sana kwa vifungu vya mswada huo, hivyo ni lazima kuongeza maelezo kuhusu mswada huo kwamba nchi wanachama haziruhusiwi kupata dawa zinazotibu magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kunenepa kupita kiasi, kuhema kila wakati, kisukari na matatizo kuhusu nguvu za uzazi. Maoni hayo tofauti yalikwamisha mazungumzo kuhusu dawa. Baada ya hapo, Umoja wa Ulaya ulitoa orodha ya magonjwa na dawa husika.

Baada ya kufanyika kwa mazungumzo magumu kwa miezi 20, baraza la WTO lilifikia makubaliano ya muda tarehe 30 mwezi Agosti mwaka 2003 yakiruhusu nchi zinazoendelea zisizo na uwezo wa kuzalisha dawa kuagiza dawa za bei rahisi zisizolindwa na hataza na kutozuiliwa na haki-miliki ya dawa wakati afya ya umma inapokabiliwa na tishio la maambukizi makubwa ya maradhi. Lakini dawa hizo zinazoagizwa kutoka nchi za nje haziruhusiwi kutumika kwa kujipatia faida, wala haziruhusiwi kusafirishwa kwenye masoko ya dawa ya nchi zilizoendelea.

Hadi hivi sasa miaka zaidi ya miwili imepita. Mkutano wa mawaziri wa WTO utafanyika hivi karibuni huko Hong Kong, baadhi ya nchi zinazoendelea, hususan nchi za Afrika zinatarajia suala kuhusu dawa litathibitishwa kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, la sivyo, njia hiyo ikiwa ni ya utatuzi ya muda inaweza kubatilishwa wakati wowote. Kwa hiyo, makubaliano yaliyopitishwa safari hiyo yanachukuliwa ni uthibitishaji kwa mpango wa utatuzi wa muda uliopitishwa tarehe 30 mwezi Agosti mwaka 2003, zinatarajia mpango huo uthibitishwe kutokana na "marekebisho ya makubaliano ya haki-miliki ya kielimu zinazohusika na biashara", na utafanya kazi rasmi ya kisheria baada ya kuidhinishwa na theluthi mbili za nchi wanachama wa WTO. WTO inakadiria kuwa kwa kuchelewa kabisa, makubaliano hayo yataanza kufanya kazi kabla ya tarehe 1 mwezi Desemba mwaka 2007.

Nchi nyingi zinazoendelea hususan nchi za Afrika zimetoa pongezi kwa makubaliano hayo. Katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy amesema kupitishwa kwa makubaliano hayo kumeonesha azma ya nchi wanachama wa WTO ya kutaka utaratibu wa biashara ya pande nyingi unufaishe ubinadamu na maendeleo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-12-07