Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-08 17:03:15    
Maisha ya watawa wa madhehebu ya kibudha ya Kitibet

cri

Hekalu la Mingzhulin lililoko katika wilaya ya Zhalang, kusini mwa mkoa unaojiendesha wa Tibet linamilikiwa na kikundi cha Ningma cha madhehebu ya kibudha ya Kitibet, lina watawa 54 na limekuwa na historia ya miaka zaidi ya 300.

Mtawa Jiangbaijincang mwenye umri wa miaka 70 ni mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa kidemokrasia ya hekalu hilo. Alisema hivi sasa hekalu la Mingzhulin linafuata njia ya kujitegemea, yaani kujimudu kwa kuanzisha lenyewe shughuli za uzalishaji, na maisha ya watawa yameboreshwa kidhahiri.

"Shughuli zetu muhimu ni kutengeneza udi wa kitibet ambao unajulikana nchini China na duniani. Biashara ya kuuza udi ni muhimu katika kuliletea pato hekalu letu."

Mtawa Jiangbaijincang alisema hekalu la Mingzhulin lina eneo lisilozidi hekta 0.7, lina mashamba ya kulima nafaka na mboga, lina misitu, ng'ombe wa maziwa, yak, mabasi matatu ya abiria, pia limefungua maduka mawili madogo yanayouza vitu vya matumizi ya nyumbani. Mapato yanayotokana na shughuli hizo pamoja na mapato ya kuuza tikiti za kuingia kwenye hekalu hilo na msaada uliotolewa na waumini, mwaka jana mapato ya jumla ya hekalu la Mingzhulin yalizidi Yuan laki nane. Isitoshe kila mwaka serikali inatenga fedha maalum kwa ajili ya kukarabati majengo ya hekalu na kuhifadhi vitu vya kale.

Mtawa Jiangbaijincang alisema mapato hayo licha ya kutumiwa katika kuhifadhi vitu vya kale na kukarabati majengo ya hekalu, kiasi kikubwa cha mapato hayo kinatumiwa katika kuboresha maisha ya watawa. Watawa wote wanashiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kupewa kifuta jasho kutokana na kazi zao. Watawa pia wanatunukiwa fedha kutokana na bidii zao za kujifunza ujuzi wa kidini na kufuata nidhamu ya hekalu.

Waandishi wetu wa habari walipofika huko waliwakuta watawa wakila chakula cha mchana. Mtawa Cidanwangzhu alisema Chakula cha mchana kilikuwa mikate na kitoweo cha maboga kukaangwa na vipande vya nyama, Cidanwangzhu alichukua mikate mitatu na bakuli moja ya mboga na nyama, kama visingetosha aliweza kuchukua zaidi.

Katika sehemu ya kusini ya Hekalu la Mingzhulin kuna jumba lenye ghorofa mbili, ambalo ni makazi ya watawa. Kila mtawa anapewa chumba kimoja chenye mita 7 za mraba. Baimakezhu mwenye umri wa miaka 34 alijiunga na hekalu hilo zaidi ya miaka 20 iliyopita, na amekuwa mtawa wa ngazi ya juu. Kila mwezi anaweza kupata ruzuku kidogo, ameridhika na maisha ya huko. Akisema:

"Kamati ya usimamizi wa kidemokrasia ya hekalu inatuandalia mafunzo kuhusu mambo ya sheria au kusoma magazeti mara mbili kwa mwezi."

Mchana Mtawa Baimakezhu anasoma msahafu, kujifunza lugha ya kale ya India na lugha ya Kitibet ya kale, kujifunza ujuzi wa kalenda na dawa na tiba za kitibet. Usiku anajifunza msahafu au kufanya usafi. Zaidi ya hayo, Baimakezhu na watawa wengine hualikwa kufanya shughuli za kidini nyumbani kwa wanakijiji, au kuzisaidia familia zenye matatizo kufanya kazi shambani. Mtawa Baimakezhu aliongeza kuwa, hekalu la Mingzhulin pia linaandaa mashindano ya kuzungumza Kichina, kuandika kichina na uchoraji, au kufanya maonesho ya michezo ya sanaa. Shughuli hizo si kama tu zimeongeza ujuzi wao wa kichina, bali pia zimechangia kwenye maisha yao baada ya masomo.

Imefahamika kuwa, hivi sasa mahekalu yote ya mkoani Tibet yanaendesha shughuli zao kwa kujitegemea, na maisha ya watawa yameboreshwa. Hekalu la Sanye linaendesha huduma za Taxi, mkahawa na hoteli; hekalu la Zashilunbu lina watawa zaidi ya 800, na baadhi ya watawa hao licha ya kufanya shughuli za kidini, pia wanafanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza samani na kufanya shughuli za utalii.

Mtawa Basan mwenye umri wa miaka 18 alijiunga na hekalu la Zashilunbu zaidi miaka mitano iliyopita. Alisema:

"Watawa wengi wa Hekalu la Zashilunbu wanafanya kazi zinazohitaji kutumia nguvu nyingi mbali na shughuli za kidini. Watawa zaidi ya 300 kati ya 800 kila asubuhi ya mapema wanasoma msahafu, na kuanza kufanya kazi saa tatu ya asubuhi. Baadhi yao wanasimamia kumbi za kuwekea sanamu za buddha, wengine wanafanya uzalishaji mali, ulinzi wa usalama, au kukarabati vitu vya kale."

Ofisa anayeshughulikia shughuli za kidini mkoani Tibet Bw. Wang Qingchan alifahamisha kuwa, serikali ya China inatekeleza sera ya kuamini dini kwa uhuru mkoani Tibet, watawa baada ya kujifunza mambo ya kidini katika mahekalu na kupewa vyeti, wana haki ya kuendesha shughuli za kidini nje ya mahekalu. Kila mwaka wanapewa likizo ya siku 20. Watawa wazee kila mwaka wanapewa malipo ya uzeeni ya Yuan 900 hadi 1200, pia wanaweza kupata matunzo ya uzeeni na matibabu kutoka serikali kama wakazi wa kawaida wanaostaafu.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-08