Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-08 17:30:43    
Wachina waishio kwenye nyumba za mapangoni

cri

Nyumba za mapango ni makazi ya siku nyingi ya wakazi waishio kwenye uwanda wa juu wa udongo wa manjano ulioko katika sehemu ya kaskazini magharibi mwa China.

Katika kijiji cha Huayuantun cha mji wa Yanan, mkoani Shanxi, kaskazini magharibi mwa China, kuna familia mia kadhaa, nyingi kati ya hizo zinaishi kwenye nyumba ya mapangoni. Bw. Zhang Zhijun mwenye umri wa miaka 53 mwaka huu ni mkulima wa kawaida wa kijiji hicho, watoto wake wawili wa kiume wote wameoa. Bw. Zhang alisema kuwa, familia yake imeishi kwenye nyumba ya mapangoni kwa vizazi vingi.

"Tunapenda sana kuishi kwenye nyumba ya mapangoni, hakuna joto katika siku za joto, na hakuna baridi katika siku za baridi. Nyumba ya mapangoni ninayoishi ilijengwa na babu yangu, na wajukuu wangu wamezaliwa hapa. Siwezi kuacha kuishi kwenye nyumba hiyo ya mapangoni."

Zaidi ya miaka elfu 4 iliyopita, watu walioishi kwenye uwanda wa juu wa udongo wa manjano wa mkoa wa Shanxi walikuwa na desturi ya kuishi kwenye nyumba ya mapangoni zilizojengwa kwenye miteremko. Kwa sababu udongo manjano wa huko unanata na ni mgumu, hivyo si rahisi kwa mapango kubomoka. Kujenga nyumba za mapangoni ni rahisi, tena hakuhitaji gharama kubwa, ukiishi ndani hakuna joto wala baridi. Hivyo hadi leo, bado kuna makazi mengi ya mapango kwenye uwanda wa juu wa udongo wa manjano. Inakadiriwa kuwa, idadi ya watu waishio kwenye nyumba za mapangoni inafikia zaidi ya milioni 40.

Kwa kawaida, nyumba ya mapangoni ina urefu zaidi ya mita 3, upana mita 3 hivi, kina cha kuingia ndani kinaweza kufikia hata mita 20. Milango ya nyumba za mapangoni yote inaelekea upande wa kusini kwa ajili ya kuingiza mwangaza wa jua.

Kuna aina kadhaa za nyumba za mapangoni, yaani nyumba za mapango ya udongo, mawe, na ya matofali. Nyumba za mapango ya matofali zinaonekana ni maridadi zaidi kuliko nyumba za mapango ya aina nyingine.

Nyumba za mapangoni za Bw. Zhang Zhijun kwa jumla ni nyumba nne zilizojengwa kwenye mteremko mmoja wa mlima, na kuna safu tatu. Nyumba mbili za mapango zilizojengwa mwaka 1962 ziko kwenye safu ya juu, nyumba tatu za mapango ya matofali ziko katika safu ya pili, ambayo anakaa Bw. Zhang Zhijun na mke wake na familia ya mtoto wake mdogo, na nyumba tatu nyingine za mapango ya mawe zilizojengwa baadaye ziko katika safu ya chini, wanaishi mtoto wake mkubwa na familia yake.

Nyumba ya mapango ya matofali ya familia ya mzee Zhang ina eneo zaidi ya mita 20 za mraba, mwangaza wa jua unaingia ndani kwa kupitia dhirisha na kuleta mwanga ndani vizuri. Katika sehemu ya ndani kabisa ya nyumba ya mapango kuna Kang kubwa inayounganishwa na jiko. (Kang ni aina ya kitanda kikubwa kilichojengwa kwa matofali au udongo, chini ya kitanda hicho kuna tundu linalounganishwa na dohani, siku za baridi watu huchoma kuni ili kuleta joto kwa kitanda. Kang hutumiwa katika sehemu ya kaskazini ya china yenye baridi). Kwenye kuta tatu zinazozingira Kang zinabandikwa picha na karatasi zilizokatwa, picha hizo si kama tu ni mapambo, bali pia zinaweza kuzuia matandiko yasigusane moja kwa moja na ukuta. Mtafiti wa sanaa za huko Bw. Wang Kewen alisema:

"Katika sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Shanxi, wakazi wa huko wamekuwa na sanaa maalum ya mapangoni. Nyumba za mapangoni zimekuwa kama dunia yao ndogo, wanawake wa huko wanapenda kupamba dunia yao kwa kubandika picha kwenye ukuta, dari na madirishani."

Nyumba za mapangoni na sanaa za mapangoni za huko zinawavutia watalii wengi wa nchini China na nchi za nje. Hivi sasa mzee Zhang ametumia nyumba zake za mapango kuanzisha shughuli za utalii za mapango, kuwahudumia watalii kwa vyakula vyenye umaalum wa wenyeji. Akisema:

"Biashara yangu ni nzuri zaidi kuliko familia nyingine zisizokuwa na nyumba za mapangoni, watalii kutoka sehemu nyingine wakija kwangu na kukaa kwenye Kang husifu hali ya nyumba za mapangoni. Tunawahudumia watalii hao kwa vyakula vya kienyeji. Sisi pia tunafanya maonesho ya mchezo wa Yangge ya Shanxi. Wageni kutoka nchi za nje wanapenda kutazama maonesho ya sanaa ya ukataji karatasi."

Hivi sasa watu wengi wa mji wa Yanan wamefahamu thamani ya nyumba za mapangoni wanakoishi kwa vizazi vingi, na kutumia nyumba hizo za mapangoni kuendeleza shughuli za utalii, kwa kuboresha maisha yao. Mji wa Yanan pia umeanzisha sehemu kadhaa za vivutio vya nyumba za mapangoni na kuwaonesha watalii uzuri wa mapango. Hoteli ya mapango ya mawe ya Yanan ambayo ni kundi kubwa kabisa la mapango duniani imekuwa kivutio kipya cha utalii cha Yanan. Hoteli hiyo ina safu nane yenye mapango 300, kwenye kuta za mapango zilitundikwa picha zilizochorwa na wakulima wenyeji wa huko, kwenye madirisha zilibandikwa karatasi za ukataji, na kwenye vizingiti vya madirisha viliwekwa vikapu vya maua mabichi. Mbele ya mapango kuna kinu cha mawe cha kusaga unga, meza na viti vya mawe, inaonesha vizuri hali ya kifamilia ya wakulima wa huko. Ili kukidhi mahitaji ya wageni wa aina mbalimbali, baadhi ya nyumba za mapangoni zina vitanda, na nyingine zimejengwa Kang ya kienyeji. Ndani ya nyumba hizo za mapangoni kuna vyoo, na vifaa vingine vya kimaisha. Bw. Xu Changjun kutoka Shanghai aliyeishi katika hoteli hiyo ya mapango alisema:

"Watu wengi wanaoishi mijini hawajawahi kuona mapango. Huu ni umaalum wa kikabila, ingawa zana zilizoko ndani zimebadilika, lakini vitu vingi vya kiutamaduni bado vimehifadhiwa."

Kwa upande mwingine, wakati watu wa sehemu nyingine nchini China wanapomiminikia Shanxi kuona maisha ya nyumba za mapangoni, baadhi ya wakulima wa huko wameacha mapango na kujenga nyumba za ghorofa.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-08