Mkutano wa siku mbili wa viongozi wakuu wa nchi za Kiislamu ulimalizika tarehe 8 huko Mecca, Saudi Arabia. Viongozi hao walitoa wito wa kuzitaka nchi za Kiislamu ziimarishe umoja wao na kupambana na siasa kali, na kuhamasisha uenezi wa uvumilivu na upole.
Viongozi wa nchi 57 wanachama za Baraza la Kiislamu walihudhuria mkutano huo na walijadili changamoto na hatua za kukabiliana na changamoto hizo katika karne ya 21.
Kwanza, kwa kauli moja viongozi hao wanaona kuwa, siasa kali ni moja ya vyanzo vya kusababisha ugaidi, wanatumai kuondoa fikra zinazosababisha ugaidi kwa kuenzi uvumilivu na upole unaoshikiliwa na dini ya Kiislamu. Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema kuwa Uislamu ni "dini ya upole", na inapinga "fikra kali kupita kiasi na kujitenga na dunia". Taarifa hiyo inasisitiza hatua mbalimbali zichukuliwe zikiwa ni pamoja na mageuzi ya elimu shuleni kuenzi maadili ya Kiislamu ya kusameheana, kuvumiliana na kuzungumza.
Pili, taarifa inashutumu aina zote za ugaidi na kupinga mashambulizi ya kigaidi kwa visingizio vyovyote, na kuunga mkono nchi wanachama za Baraza la Kiislamu zinazokumbwa na ugaidi. Taarifa inasisitiza kuwa vitendo vyovyote vya kigaidi lazima viadhibiwe vikali, na kuwaadhibu kisheria wale watu wanaounga mkono, kufadhili na kuchochea vitendo vya kigaidi. Taarifa inasisitiza kwamba ugaidi hauna uhusiano wowote na dini, kabila la watu, rangi ya ngozi na nchi, ni lazima kutofautisha wazi kati ya vitendo vya kigaidi na vitendo vya kupinga wakaliaji kwa nguvu wa nchi za nje.
Tatu, mkutano unasisitiza kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuungana pamoja na kupinga shutuma zote zisizo za kweli kutoka nje. Mkutano huo pia umeonesha wasiwasi kuhusu uchukivu na upinzani uliotokea duniani dhidi ya dini ya Kiislamu na kuzitaka serikali za nchi zote duniani ziheshimu uhuru wa kuamini dini na kuwaheshimu wawakilishi wa dini, wala sio kuwashambulia kwa nia mbaya kwa kisingizio cha uhuru wa kusema. Mkutano unataka kuanzisha idara ya kutetea haki za binadamu ndani ya Baraza la Kiislamu na kutunga katiba ya haki za binadamu za Waislamu.
Nne, viongozi walioshiriki kwenye mkutano huo wameafikiana kuhusu kuimarisha umoja wa dunia ya Kiislamu, kulifanyia mageuzi Baraza la Kiislamu ili kukabiliana kwa pamoja changamoto zinazoikumba dinia ya Kiislamu. Katibu mkuu wa Baraza la Kiislam Ekmeleddin Ihsanoglu alisema, mkutano huo umepitisha Taarifa ya Mecca na mpango wa mageuzi ya Baraza la Kiislamu ili kukabiliana na changamoto inayoikabili dunia ya Kiislamu katika karne ya 21. Licha ya Taarifa hiyo mkutano huo pia umepitisha maazimio mengi yakitaka nchi wanachama za Baraza la Kiislamu zitoe mchango mkubwa zaidi katika kustawisha uchumi wa taifa, kuweka sura nzuri ya dini ya Kiislamu duniani.
Tano, mkutano umefanya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa dunia ya Kiislamu katika uchumi na biashara. Taarifa imezitaka nchi wanachama za Baraza la Kiislamu ziimarishe biashara kati ya nchi hizo na kuunga mkono benki ya Kiislamu ianzishe mfuko maalum ili kuhimiza uchumi wa nchi wanachama na kutatua matatizo yanayoikumba dunia ya Kiislamu.
Wachambuzi wanaona kuwa mkutano huo unapinga kidete utetezi wa siasa kali na kutaka kuenzi uvumilivu na upole, msimamo huo utasaidia kuondoa fikra za kusababisha ugaidi na utakuwa na athari za kina kwa dunia ya Kiislamu na hata kwa juhudi za kupambana na ugaidi duniani kote, na mageuzi ya Baraza la Kiislamu yatasaidia kuimarisha nguvu ya umoja wa nchi za Kiislamu na kutoa mchango mkubwa katika mambo ya kimataifa na katika mapambano dhidi ya ugaidi duniani.
Idhaa ya kiswahili 2005-12-09
|