Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-13 20:25:28    
Barua 1213

cri
Msikilizaji wetu Raheli budeba wa Chuo cha Ualimu Ndala, sanduku la posta 9 Ndala Tabora Tanzania ametuletea barua akisema madhumuni ya barua hii ni kutuarifu kuwa barua tulizomtumia zote amezipata, lakini kilikuwa ni kipindi kibaya kwani alikuwa anakabiliwa na mtihani wa taifa, kwa hilo anaomba samahani kwa kuchelewa kutujibu. Pia anaomba tumtumie jarida lingine kwani majarida mengi hakubahatika kuyapata.

Anasema alipokuwa shule alikuwa hapati nafasi ya kusikiliza radio, alikuwa anapata nafasi hiyo akirudi nyumbani, lakini sasa atakuwepo nyumbani kwa muda mrefu ameshamaliza mitihani na anaweza kusikiliza kwa makini matangazo yetu ili aweze kuelewa zaidi mambo yanayoendelea. Atajaribu kujibu maswali kwa kutumia akili yangu pia matokeo yatakapotoka naomba tumtumie majibu yake ili aweze kufahamu zaidi.

Msikilizaji wetu mwingine Damas M. Bundala ambaye barua zake huhifadhiwa na Bw R.C. Irimani wa sanduku la posta 659 Victoria, Mahe Shelisheli ametuletea barua akianza kwa kutusalimu. Anasema yeye huko Mahe anaendelea vizuri na shughuli zake za kila siku, na pia anatumai kuwa nasi tunaendelea hivyohivyo. Kwanza angependa kutupa pongezi kwa kuchapisha toleo la kwanza la jarida dogo la Daraja la urafiki. Anaamini kuwa kutokana na juhudi za idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa na wasikilizaji kwa ujumla, tutaendelea kulikuza na kulipendezesha zaidi.

Pia anatuarifu kuwa anuani yake imebadilika. Hii ni kwa sababu ya kumalizika kwa mkataba wa baba yake huko Shelisheli. Lakini yeye mwenyewe ataendelea kuwepo huko ili amalizie masomo yake, hivyo anatuomba tutumie anuani yake mpya. Anatuomba msamaha kwa kutotujulisha mapema, kwani alishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali za kifamilia.

Lakini anasema anaamini kuwa tutamwelewa, kwani haikuwa mipango yake kufanya hiyo. Vilevile anasema atajitahidi kufungua anuani ya barua pepe ili aweze kurahisisha mawasiliano kati yake na sisi. Kwa sasa anaendelea kusikiliza matangazo yetu na kusoma matangazo yetu na kufuatilia vipindi vyetu mbalimbali kupitia kwenye mtandao wa Internet.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Damas Bundala, asiwe na wasiwasi, tunawashukuru wasikilizaji wetu kwa juhudi zao zote za kudumisha mawasiliano na idhaa yetu ya Radio China kimataifa, na juhudi zao hizo zinatutia moyo tuendelee kuchapa kazi zaidi.

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija Kiliwi shule ya msingi mwamashimba division sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania anasema katika barua yake kuwa, anapenda kutumia fursa hii ya kuipongeza idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa mengi kuhusu matukio mbalimbali ulimwenguni hususan watangazaji wafuatao ambao anawapongeza Mama Chen, Pomboo, Luda, Fadhili Mpunji, Pamoja na watangazaji wengine wote wa Radio China Kimataifa nao pongezi zake zote wazipokee kwa kazi zao zote wanazozifanya kwa ajili ya wasikilizaji.

Mwisho katika kumaliza barua yake hii anaitakia idhaa hii ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa iendelee kuwatangazia wasikilizaji mengi yanayotokea kila kukicha kote ulimwenguni. Pia urafiki kati yake na Radio China Kimataifa udumu zaidi. Anatutakia kazi njema yenye mafanikio mema.

Tunamshukuru kwa dhati kwa salamu na pongezi zake za dhati, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yake.

Msikilizaji wetu Mogire Machuki klabu ya wasikilizaji wa CRI sanduku la posta 646, Kisii Kenya, anaanza barua yake kwa kutusalimu. Anasema huko aliko hali ni shwari na wanaendelea kusukuma gurudumu la maisha huko wakifurahia vipindi vya matangazo yenayopitia idhaa ya Kiswahili ya KBC na kwenye masafa mafupi.

Pamoja na barua hii ameambatanisha majibu ya Chemsha Bongo ya Taiwan-kisiwa cha hazina cha China. Majibu hayo yameambatanishwa na majina ya wanachama wapya ambao kwa pamoja wanaunda klabu ndogo ya wasikilizaji CRI wakati wa maadhimisho maalumu ya kutimia miaka miwili tangu viongozi wa ngazi ya juu ya CRI kutembelea hapa kisii. Anasema mengi hana ila anatutakia kazi njema.

Tunashukuru sana kwa barua yake na juhudi zake za kutufuatilia kila mara, hatuwezi kusahau safari ile ya Kisii, Kenya, ni matumaini yetu kuwa, ziara hiyo ya Kisii Kenya itakuwa kumbumbuku ya daima na itakuwa daraja la kudumisha urafiki kati yetu na wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Sorca M. Ngeresa wa sanduku la posta 1708 Kisii Kenya, kwenye barua yake kwanza ameanza kwa salamu, akitumai kuwa sisi tunaendelea vizuri. Yeye huko akiwa ni mwanachama mpya wa Radio China Kimataifa anatuomba tumtumie bahasha ambazo zimelipiwa gharama za stempu hili aendelee kuwasiliana nasi kwa njia iliyo safi kabisa. Wao hapo kwa jamii yao wanapenda kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa, kwa sababu ya matangazo yetu na vipindi vyetu wanapokea kwa njia iliyo safi. Anasema yeye ni mwanafunzi na yuko katika kidato cha pili katika shule ya upili ya Miriri.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff 172 Bungoma Kenya anasema, ni matumaini yake ni kuwa kazi inaendelea vilivyo katika idhaa hii waipendayo. Anasema huko Bungoma yeye ni mzima na wanatupata vizuri sana ingawa wanaendelea na hekaheka za kila siku. Hata hivyo angependa kutufahamisha ya kuwa maswali ya mashindano ya chemsha bongo yaliwafikia ingawa mara hii maswali haya yalionekana kuwa magumu. Kwa hivyo ombi lao ni kuwa tunaposoma makala, tuzisome kwa makini zaidi ili waweze kusikia vizuri zaidi. Jambo lingine ni kwamba kulingana na matangazo yetu, tumewaarifu kuwa wanaweza kutusikiliza kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Jumamosi ni saa tisa hii imekuwa sawa kabisa, lakini siku ya jumapili matangazo yanatakiwa kuanza saa nane na nusu lakini kwa wakati mwingine inaanza saa nane kamili. Kwa hivyo wanashitukia tu kuwa tumesharudia makala kuhusu Taiwan.

Ombi lao ni kuwa itakuwa vizuri kama tutaweza kurudia tena hayo makala ya kwanza na pili. Jambo lingine ambalo yeye na wenzake Allan Wachie, Xarier Telly Wambwa, Konje, Anaseti na wengine wamejaribu kuangalia kwenye tovuti na bado hawaona makala hizo. Kwa hivyo wanatuomba tuziweke haraka iwezekanavyo ili waweze kujibu maswali ya chemsha bongo kwa wakati..

Hapa tunapenda kumwambia kuwa, makala 4 hizo zimewekwa kwenye tovuti yetu katika kipindi cha Sanduku la barua tangu tusome mpaka sasa. Labda hawakupekua vizuri, msisahau anuani ya tovuti yetu ni www.cri.cn, chagua Kiswahili mtakuta vipindi vyetu mbalimbali. Makala za chemsha bongo ziko kwenye kipindi cha sanduku la barua.

Msikilizaji Braheem S.J. Kirusha 111 Ulyankulu-Tabora, Tanzania anasema katika barua yake kuwa, ni msikilizaji na mfwatiliaji mzuri wa vipindi mbalimbali vya Radio China Kimataifa na anafurahishwa sana na ufanisi tulio nao katika utayarishaji wa vipindi vyetu, kwani ameweza kujifunza mambo mengi kupitia vipindi mbalimbali vya Radio China Kimataifa. Vilevile amejifunza na kufahamu mengi juu ya China baada ya kusoma Risala ya mwaka 2005 katika makala ya Daraja la Urafiki iliyotolewa na mkuu wa Radio China Kimataifa Bw. Wang Geng Nian, hivyo basi lengo la waraka huu ni kuomba kuwa mwanachama wa Radio China Kimataifa ili aweze kuwa karibu zaidi nasi, kwani kwa kufanya hivyo anaamini atajifunza mambo mengi zaidi.

Tunamkaribisha kwa furaha kuwa msikilizaji wetu mpya, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutuletea maoni na mapendekezo yake ili tuandae vizuri zaidi vipindi vyetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-13