Katika miaka ya karibuni, kutokana na uongozi wa Umoja wa Afrika na uhimizaji mkubwa wa jumuyia ya kimataifa, nchi mbalimbali za Afrika zimetambua kwamba kulinda amani na usalama barani Afrika ni sharti la lazima la kustawisha bara lao katika karne ya 21.
Mwaka huu ni mwaka ambao nchi za Afrika zimefanya juhudi kubwa katika kutafuta amani, na matokeo pia yanaonekana wazi. Moja kati ya matokeo hayo ni kuwa uchaguzi wa rais na uchaguzi wa wabunge umefanyika kwa mara ya kwanza nchini Liberia baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14, na rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Afrika amechaguliwa. Kuhusu suala hilo mtaalamu wa mambo ya Afrika wa Nigeria. Bw. Salim anasema,
"Serikali ya Liberia bado inakabiliwa na matatizo mengi yaliyotokana na vita vilivyofanyika kwa miaka mingi, uchumi na miundo mbinu imeharibika vibaya, ukosefu wa ajira ni mkubwa na ufisadi unashamiri. Kazi ya serikali hiyo ni nzito."
Mbali na Liberia, nchini Sudan, serikali ya umoja wa kitaifa na serikali inayojiendesha ya kusini mwa Sudan zimeanzishwa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu baada ya miaka 21 ya vita wenyewe kwa wenyewe. Kuazishwa kwa serikali hizo kuna umuhimu mkubwa katika kuleta amani na maafikiano ya kitaifa. Kuanzishwa kwa serikali ya mpito ya Somalia mwishoni mwa mwaka jana kumemaliza hali ya "kuishi ugenini" nchini Kenya wa serikali ya nchi hiyo na kurudi nchini Somalia na kuweka msingi wa kuongoza taifa hilo kulijenga upya. Isitoshe, nchi ambazo zilikuwa na migogoro mingi kama Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi na Cote d'Ivoire pia zinaelekea kuwa tulivu.
Pamoja na hali inayoelekea kuwa na amani na utulivu, uchumi barani Afrika pia umepata maendeleo. Kutokana na takwimu za benki ya dunia, ongezeko la uchumi wa Afrika mwaka huu litafikia 3% hadi 5%, hayo ni maendeleo makubwa. Kwa mfano Angola, kutokana na hali ya utulivu na ujenzi wa miundo mbinu kuharakishwa, maliasili ya mafuta imevutia mashirika mengi ya mafuta kuwekeza nchini humo.
Wachambuzi wanaona kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kuwa watu wa Afrika wanataka kupata maisha yenye utulivu, na pia yanatokana na juhudi za jumuyia ya kimataifa na hasa Umoja wa Afrika. Umoja wa Afrika ulioanzishwa mwaka 2002 umetoa mchango mkubwa katika juhudi za kuleta amani na utulivu, kusukuma mageuzi, kupunguza umaskini na kuendeleza uchumi. Umoja huo usio na miaka mingi tokea uanzishwe, mwaka 2005 licha ya kuanzisha jeshi lake la kulinda amani ili kupambana na hali ya dharura ya migogoro barani Afrika, pia unajitahidi kusuluhisha migogoro. Mtaalamu wa mambo ya Afrika Bw. Salim alisema,
"Umoja wa Afrika bado unakabiliwa na changamoto nyingi, lakini utapiga hatua na kutatua matatizo yaliyopo. Nina hakina kwamba Umoja huo utatoa mchango mkubwa zaidi."
Umoja wa Afrika licha kutoa mchango katika mambo ya siasa, nao pia umehimiza maendeleo ya uchumi barani Afrika. Bw. Dai Yan aliyekuwa balozi wa China katika nchi nyingi za Afrika alisema,
"Nchi za Afrika lazima zitilie mkazo katika ujenzi wa miundo mbinu, maendeleo ya kilimo, mawasiliano ya barabara na teknolojia ya upashanaji habari. Huu ni mwongozo wa fikra za Umoja wa Afrika."
Mafanikio makubwa ya Umoja wa Afrika katika miaka mitatu iliyopita ni wazi, lakini matatizo yake pia ni dhahiri. Bw. Dai Yan alisema,
"Mkakati wa Umoja wa Afrika ni sawa kabisa, lakini utekelezaji wake utakumbwa na matatizo mengi. Bara la Afrika linakabiliwa na taathira mbaya ya utandawazi duniani, ni vigumu kufuata njia ya maendeleo endelevu. Bara hili ni sehemu maskini kabisa duniani, msingi wa uchumi ni dhaifu ambao ni rahisi kutikiswa na uchumi wa kimataifa."
Wachambuzi wanasema, kama Umoja wa Afrika unajitahidi kuleta utulivu huku ukihimiza utandawazi wa uchumi, na kusawazisha misimamo wa nchi mbalimbali za Afrika, bara la Afrika linaweza kujitoa mapema kutoka kwenye umaskini na vita na kuelekea kwenye amani na maendeleo.
|