Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-15 20:05:46    
Majengo ya Jadi ya China

cri
Kasri la Kifalme Mjini Beijing

Kasri la Kifalme mjini Beijing ni mfano wa majengo ya kifalme nchini China. Kasri hilo kwa Kiingereza linaitwa "Forbidden City", ni kasri lililokaliwa na wafalme wa Enzi za Ming (1368-1644) na Qing (1616-1911), wafalme 24 waliwahi kuishi katika kasri hilo. Eneo la kasri hilo ni mita za mraba laki 7.2, kuna vyumba 9999, uzio wa kasri hilo ni ukuta mwekundu wenye kimo cha mita kadhaa, urefu wa ukuta huo ni mita 3400, nje ya uzio huo kuna mto uliochimbwa kwa ajili ya kulinda kasri hilo. Aidha kwa ukubwa wa kasri hilo, mtindo wake, na ufahari wake, kasri kama hilo halipatikani katika sehemu nyingine duniani.

Kasri la Kifalme mjini Beijing limegawanyika katika sehemu mbili, majengo katika sehemu ya mbele ni sehemu kwa ajili ya wafalme kufanya sherehe kubwa na kutoa amri, majengo kwenye sehemu hiyo ni ukumbi wa Taihe, Zhonghe, na Baohe. Majengo hayo yalijengwa juu ya jukwaa lenye urefu wa mita 8, kwa mbali yanaonekana kama kasri la peponi. Majengo katika sehemu ya nyuma ni makazi ya wafalme na masuria. Majengo katika sehemu hiyo ni mengi yakiwa ni pamoja na bustani, vyumba vya kusomea na bustani yenye majabali ya ajabu, na kila jengo lina ua wake.

Kutokana na enzi na enzi katika historia ndefu, majengo ya kale yaliyobaki kikamilifu ni machache. Licha ya Kasri la Kifalme mjini Beijing, pia kuna kasri la kifalme katika mji wa Shenyang, na magofu ya makasri ya Enzi ya Han (206-220 K.K.) na Enzi ya Tang (618-907) katika mji wa Xi'an.

Majengo ya Mahekalu

Mahekalu ni moja ya aina ya majengo ya dini ya Buddha nchini China. Mahekalu nchini China yalianzia India, mahekalu hayo ni ishara ya hali ya ustawi wa dini ya Buddha katika historia, ni majengo yenye thamani kubwa kwa ajili ya uchunguzi na usanii.

Wahenga wa China walizingatia sana ulinganifu wa majengo kwenye kando mbili za mstari wa katikati, hali kadhalika kwenye ujenzi wa mahekalu ya dini ya Buddha. Lakini pia kuna mahekalu yaliyojengwa kama bustani. Aina hizo mbili zinayafanya mahekalu nchini China yawe na taadhima na uzuri wa kimaumbile.

Mpangilio wa ujenzi wa hekalu la kale ni kuwa mbele kuna lango, na baada ya kuingia kwenye lango hilo upande wa kushoto na kulia kuna jumba la kengele na jumba la ngoma, na nyumba kubwa inayokabili lango ni ukumbi wa mungu, ndani ya ukumbi huo kuna sanamu za walinzi wanne wa peponi, nyuma ya ukumbi huo na kuendelea ni ukumbi wa mwasisi wa dini ya Buddha, Sakyamuni. Ukumbi huo ni mkubwa na ni muhimu kabisa kuliko majengo yote ndani ya hekalu. Mahekalu yaliyojengwa kabla ya enzi za Sui (581-618) na Tang (618-907) kwa kawaida hujengwa pagoda mbele ya hekalu au katikati ya ua wa hekalu, na baada ya enzi za Sui na Tang nafasi ya jengo la pagoda imechukuliwa na ukumbi mkubwa, na pagoda hujengwa katika ua mwingine.

Idhaa ya Kiswahili 2005-12-15