Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-16 14:15:10    
Kuondoka kwa askari wa kulinda amani la Umoja wa Mataifa kumezidisha hali ya wasiwasi kati ya Ethiopia na Eritrea

cri

Askari wa kulinda amani nchini Eritrea walilazimika kuondoka kuanzia tarehe 15, hii inamaanisha kuwa juhudi za naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Jean Marie Guehenno hazikufanikiwa kama ilivyotazamiwa, hali kati ya Ethiopia na Eritrea imezidi kuwa mbaya.

Katika siku hiyo, kundi la kwanza la askari 90 wa Umoja wa Mataifa waliotoka Marekani, Canada na nchi za Ulaya waliondoka kutoka Asmara, mji mkuu wa Eritrea na kwenda hadi Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Habari zinasema kuwa Eritrea inataka askari 180 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waondoke. Tarehe 14 Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ya mwenyekiti ikisema kuwa uamuzi wa kuondoa askari wa Umoja wa Mataifa uliofanywa na Baraza la Usalama ni kwa ajili ya usalama wa askari wake, msimamo wa Eritrea wa kutoshirikiana umefanya askari hao kutoweza kutimiza jukumu lao.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Marie Guehenno anayefanya uchunguzi kwenye mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea tarehe 15 alisema, kutokana na kukataliwa, hakuweza kukutana na maofisa wa Eritrea ili kuwashawishi wabadilishe madai ya kuondoa askari wa Umoja wa Mataifa.

Tarehe 6 serikali ya Eritrea iliiarifu jeshi la Umoja wa Mataifa ikitaka iondoe askari wa kulinda amani waliotoka Marekani, Canada, Russia na nchi za Ulaya waondoke ndani ya siku 10, na haikueleza sababu yoyote. Kuondoka kwa askari hao kumezidisha hali ya wasiwasi kwenye mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan tarehe 7 alisema, uamuzi wa serikali ya Eritrea ni hujima kwa madaraka ya katibu mkuu aliyopewa na Baraza la Usalama", aliitaka serikali ya Eritrea ibatilisha uamuzi huo bila masharti yoyote, na huku Annan alituma Marie Guehenno na watu wake kwenda huko kusuluhisha kutokana na kuwa nchi mbili zilipeleka askari wengi mpakani.

Bw. Marie Guehenno alipokuwa nchini Ethiopia alikutana na waziri mkuu wa Ethiopia, waziri mkuu alisema, Ethiopia inaweza kurudisha nyuma askari wake kwa masharti, kisha alikwenda Eritrea akijaribu kukutana na maofisa wa nchi hiyo lakini alikataliwa. Kutokana na hali hiyo Baraza la Usalama limeamua kuondoa baadhi ya askari wake hadi upande wa Ethiopia.

Sababu muhimu ya serikali ya Eritrea kutaka kuondoa askari wa Umoja wa Mataifa ni mgogoro wa mpaka.

Ethiopia na Eritrea zilikuwa ni nchi moja, baada ya vita wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka zaidi ya 30, mwezi Aprili mwaka 1993 Eritrea ilifanya upigaji kura za maoni chini ya uangalizi wa jumuyia ya kimataifa, na kisha ikatangaza kuwa nchi huru. Eritrea inashikilia mpaka wake uliowekwa mwaka 1902, lakini Ethiopia inashikilia mpaka unaomilikiwa sasa, kwa hiyo mgogoro wa mpaka umekuwa unazidi kuwa mkubwa siku hadi siku, na ndugu wa tumbo moja sasa wamekuwa maadui. Mwezi Mei mwaka 1998 vita vililipuka na kusababisha vifo vya watu elfu 70 na watu karibu milioni moja walipoteza makazi yao. Nchi hizo mbili zilisaini mkataba wa amani mwishoni mwa mwaka 2000, na mwezi Aprili mwaka uliofuata Umoja wa Mataifa ulipeleka askari wake wa kulinda amani, kwa kusimamiwa na askari hao hali ya wasiwasi iliwahi kupungua.

Mwezi Oktoba mwaka huu Eritrea ilipiga marufuku helikopta za askari wa Umoja wa Mataifa kuruka kwenye anga la nchi hiyo, na baadaye ilipiga marufuku askari wa Umoja wa Mataifa kufanya doria wakati wa usiku na kuamrisha kufunga vituo 18 vya ukaguzi kati ya vituo 40. Muda mfupi baadaye, Eritrea na Ethiopia zilipeleka askari kwenye mpaka, hivi sasa Eritrea ina askari elfu 80 mpakani na Ethiopia ina askari laki 1.5.

Wachambuzi wanaona kuwa mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo mbili ni suala lililoachwa na wakoloni wa zamani, nchi mbili hizo zinapaswa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa msimamo wa kusameheana na kutatua suala hilo kwa mujibu wa hali ilivyo. Ni kwa kushauriana tu kwa usawa na kusuluhishwa na jumuyia ya kimataifa, ndipo suala la mpaka lingeweza kutatuliwa.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-16