Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-16 18:47:35    
Mchina anayepanda mboga nchini Sudan

cri
    Bw. Zhang Fenghua alizaliwa mwezi Juni mwaka 1974 mkoani Hubei, China. Mwaka 1988, familia yake ilikwenda huko Wuhan, mji mkuu wa mkoa wa Hubei, kukodi shamba na kupanda mboga na kuwa mkulima mwenye maarifa alipokuwa na umri wa miaka 19. Mwaka 1995, alifungua biashara ya duka la vioo na kupata faida kubwa.

    Mwezi Februali mwaka 2000, rafiki yake aliyekuwa anafanya kazi katika kampuni ya mafuta ya petroli ya China nchini Sudan alirejea nchini China, na alimwambia Bw. Zhang Fenghua kuwa, kila siku alipokuwa nchini Sudan alikuwa anakuta viazi na vitunguu na hawezi kuvumilia tena maisha hayo ya kula chakula bila mboga. Pia alisema, Sudan haina ukosefu wa maji, na mto wa Nile umepita kwenye nchi hiyo, lakini wenyeji wa huko hawapandi mboga.

    Baada ya kujua hali hiyo, Bw. Zhang Fenghua aliamua kwenda Sudan kupanda mboga, na aliamini kuwa hakika atapata faida kubwa. Baada ya hapo, alifanya juhudi kubwa katika kujifunza lugha za kiingereza na kiarabu. Baada ya sikukuu ya Spring ya mwaka 2001, Bw. Zhang Fenghua alipata viza na kwenda Sudan na kuanzisha shughuli za kilimo cha mboga.

    Tarehe 4, mwezi Machi, mwaka 2001, Bw. Zhang Fenghua aliwasili huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan na kupata kazi kwenye mkahawa. Baada ya kufanya uchunguzi kwenye soko la mboga huko Khartoum, aliona kuwa, kuna aina chache za mboga ambazo bei yake ni ghali, na kati ya mboga hizo nyingi ni mbatata na vitunguu. Siku nyingine alikwenda kwenye Wizara ya Kilimo na Misitu ya Sudan ili kupata ushauri, hali iliyomfurahisha ni kuwa, alihitaji kufuata utaratibu rahisi na kugharimia kidogo kukodi shamba nchini Sudan. Kwa kawaida shamba lenye eneo la hekta saba linaweza kukodiwa kwa fedha za dola za kimarekani 300, na kuweza kulitumia kwa muda wa miaka 10.

    Tatizo la kwanza lililomkabili Bw. Zhang Fenghua wakati alipojiandaa kupanda mboga ni njia ya kupata mbolea. Kutokana na ukame na jua kali nchini Sudan, alishindwa kupata mbolea kwa kutumia njia alizozitumia nchini China. Kutokana na kukabiliwa na mazingira mapya ya Sudan, Bw. Zhang Fenghua alifanya majaribio mbalimbali, mwishoni akafanikiwa kupata mbolea kwa kuozesha nyasi.

    Mwezi Juni mwaka 2001, Bw. Zhang Fenghua alikodi shamba lenye eneo la hekta 0.7 karibu na mto Nile, kitongoji cha Khartoum, alinunua vifaa vya kilimo, kuwaajiri wenyeji watatu wa huko, na kuwaomba watu wengine wamtumie mbegu mbalimbali za mboga kutoka China.

    Bw. Zhang Fenghua alipanda kwanza mboga zenye uwezo mkubwa wa kuvumilia ukame kama vile mbilinganya na matango, na kuchukua hatua mfululizo ili kuboresha hali ya ardhi ya huko. Baada ya kufanya juhudi kwa nusu mwaka, hali ya ardhi ya shamba la Bw. Zhang Fenghua ilibadilika na kuwa shamba la ardhi yenye rutuba ambalo linaweza kutoa mazao mengi. Aidha, kutokana na kuwepo kwa mwanga wa jua wa kutosha, na maji ya kutosha, na mbegu za aina mbalimbali za mboga zilizopelekwa Sudan kutoka nchini China, mboga za mbilinganyi, matango na pilipili zinakua vizuri nchini Sudan.

    Mboga mabichi za aina mbalimbali ziliposafirishwa kwenye masoko huko Khartoum zilinunuliwa mara moja. Wakazi wa Khartoum wanapenda kula mboga, lakini hawana uwezo wa kununua mboga zenye bei ghali zinazoagizwa kutoka nchi za nje. Ingawa bei za mboga za Bw. Zhang fenghua zinalingana na bei ya nyama ya huko, lakini ni ndogo sana zikilinganishwa na mboga zinazoagizwa kutoka nchi za nje.

    Mboga zinazopandwa Bw. Zhang Fenghua pia zinawanufaisha maelfu ya wachina wanaoishi huko Khartoum. Zamani wengi kati ya watu hao hawakuweza kuvumilia kuishi huko bila kula mboga na matunda, waliondoka huko na kurudi nyumbani China. Lakini sasa wanaweza kupata mboga wanazopenda kula.

    Mboga zilizopandwa na Bw. Zhang si kama tu zinawanufaisha wachina, pia zinafurahiwa sana na wamarekani, wau kutoka Ulaya na maofisa wa nchi nyingine wanaofanya kazi nchini Sudan. Zamani walikuwa wanakula mboga mara chache, lakini sasa wanaweza kula mboga kila siku.

    Hivi sasa, eneo la shamba la Bw. Zhang Fenghua linazidi kuongezeka kwa haraka. Mwezi Machi mwaka huu, alikodi shamba lenye hekta 14, shamba hilo limekuwa shamba kubwa zaidi lililowekezwa na mgeni nchini Sudan, na kupanda mboga za kichina zaidi ya aina 30.

    Mafanikio ya Bw. Zhang Fenghua yanawahimiza wachina wengi kwenda barani Afrika kuanzisha shughuli za kilimo, na kupata mafanikio. Hivi sasa, mboga za aina nyingi nchini Sudan zinapandwa na wachina, na siku ambazo nchi za Ulaya zilikuwa zinahodhi soko la mboga nchini Sudan zimekwisha. Bw. Zhang Fenghua ndiye mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kuondoa hali hiyo. Kama vyombo vya habari vya kiserikali vya Khartoum vilivyosema, " Bw. Zhang Fenghua kutoka China amebadilisha historia, na hilo ni tukio la kufungua ukurasa mpya wa historia. "