Upigaji kura za maoni ya raia kuhusu katiba mpya ulifanyika tarehe 18 nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kupiga kura za maoni ya raia zaidi ya miaka 40 iliyopita, nchi hiyo imepiga hatua muhimu katika kutimiza amani ya kudumu nchini humo.
Siku hiyo wapiga kura waliojiandikisha wapatao milioni 25 walipiga kura katika vituo elfu 36 vilivyokuwepo nchini humo. Wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo waliochoshwa na vurugu za vita wameonesha uchangamfu mkubwa juu ya upigaji kura huo wa maoni ya raia kuhusu kuikubali katiba mpya au la. Wakati wa kujiandikisha kwa wapiga kura, wananchi wengi walishiriki kwa juhudi, hata baadhi ya wakimbizi walioishi nchi jirani kwa kukwepa vurugu za vita katika miaka kumi kadhaa iliyopita pia walirudi nyumbani kushiriki kwenye mchakato huo wa kidemokrasia. Siku ya upigaji kura, ingawa kutokana na sababu fulani milango ya vituo kadhaa ilichelewa kufunguliwa, lakini wapiga kura walisuburi nje ya milango mapema ya siku hiyo, hata misururu ilitokea nje ya vituo vingi vya upigaji kura. Wapiga kura walisema, ingawa uenezi kuhusu upigaji kura huo haukufanyika kwa nguvu kubwa, na watu wengi bado hawakuelewa vilivyo yaliyomo ya katiba mpya, lakini wanapenda kushiriki kwenye upigaji kura huo ili kusukuma mbele mchakato wa amani ambao si rahisi kupatikana.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Bwana Maru tarehe 18 usiku alitangaza kuwa, kutokana na kuwa wapiga kura wengi wa sehemu kadha wa kadha bado walisubiri nje ya vituo ili kupiga kura, upigaji kura huo uliahirishwa kukamilika kwa saa 24 hadi saa 11 jioni tarehe 19, na matokeo ya upigaji kura huo yatajulikana tarehe 26 mwezi huu.
Kutokana na katiba mpya, rais atachaguliwa moja kwa moja na wananchi, muda wa madaraka yake ni miaka mitano, na anaweza kuchaguliwa kwa vipindi viwili tu; waziri mkuu atateuliwa na rais baada ya kufanya mashauriano na kundi la watu wengi katika bunge; ugawanyaji wa mikoa ya nchi nzima utakuwa mikoa 25 na mji mmoja unaotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu; na mikoa kadhaa yenye maliasili nyingi za madini itakuwa na madaraja ya kujiendesha.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe ilitokea mwezi Agosti mwaka 1998 nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Mwezi Desemba mwaka 2002 pande mbalimbali zilizopambana zilisaini Makubaliano ya amani ya pande zote, na kuunda serikali ya mpito tarehe 30 Juni mwaka 2003. Kutokana na katiba ya kipindi cha mpito, muda wa mpito ni miaka miwili, na nchi hiyo ingefanya uchaguzi mkuu kabla ya mwishoni mwa mwaka 2005. Lakini mchakato wa amani ulikumbwa na vikwazo vingi, na uchaguzi mkuu uliahirishwa mara kwa mara. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, Bunge la nchi hiyo lilipitisha katiba mpya ambayo imeweka msingi kwa uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa vyama vingi katika zaidi ya miaka 40 iliyopita. Kama katiba mpya itaweza kupitishwa katika upigaji kura huo, si kama tu itaweka msingi wa kisheria wa kukomesha vurugu za kivita na kukamilisha kipindi cha mpito nchini humo, bali pia itatandika njia kwa ajili ya uchaguzi wa bunge na rais utakaofanyika tarehe 30 Juni mwaka 2006. Hivyo, upigaji kura huo umechukuliwa kuwa ni hatua moja muhimu itakayoweza au la kwa kukamilisha vizuri muda wa serikali ya mpito na kuunda utawala wa kidemokrasia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Jumuiya ya kimataifa iliyowahi kutoa mchango mkubwa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imetoa msaada mkubwa kwa ajili upigaji kura huo wa maoni ya raia.
Idhaa ya Kiswahili 2005-12-19
|