Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-20 16:00:13    
Nafasi kubwa ya biashara ya vitu vya baraka vya michezo ya Olimpiki

cri

Tangu kuthibitishwa kwa "wanasesere wa baraka" kuwa vitu vya baraka vya michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 katika mwezi uliopita, bidhaa zenye michoro ya "wanasesere wa baraka" hivi sasa zinauzwa kwa wingi kwenye miji mikubwa nchini China. Habari kutoka sehemu nyingi zinazouza bidhaa hizi zinasema kuwa, bidhaa za "wanasesere wa baraka" zimekwisha, katika baadhi ya miji midogo na sehemu za vijijini ambako hakuna maduka yaliyopata leseni ya kuuza vitu hivyo kuhusu michezo ya Olimpiki, watu wengi wanaomba marafiki au jamaa zao wanaoishi katika miji mikubwa wawatumie kwa njia ya posta. Wataalamu wanakadiria kuwa bidhaa za "wanasesere wa baraka" zitaileta China faida ya mamilioni ya dola za kimarekani.

Katika duka moja linalouza bidhaa za michezo ya Olimpiki, mwandishi wetu wa habari aliona wateja wengi waliotaka kununua "wanasesere wa baraka". Bw. Lu Lin alibahatika kupata seti ya mwisho ya "wanasesere wa baraka".

"Nimepata seti moja, seti nyingine niliyonunua hivi sasa ni kwa ajili ya rafiki yangu, mimi pia nimenuia kwenda huko."

Dada Jiang Jin vilevile alitaka kununua "wanasesere wa baraka", lakini aliwakosa, alisema kwa masikitiko kwamba leo amekosa "wanasesere wa baraka" anaowapenda, hivyo alichagua skafu moja yenye michoro ya "wanasesere wa baraka".

"Ninataka sana nipate 'wanasesere wa baraka', ninawapenda sana. Lakini nilifika hapa mara tatu, na kila mara niliambiwa wote wameuzwa."

Vitu vya baraka vya michezo ya Olimpiki ya Beijing ni wanasesere watano wenye taswira za samaki, panda, moto mtakatifu wa Olimpiki, Paa wa Tibet na mbayuwayu. Majina ya wanasesere hao watano yakiunganishwa pamoja yana maana ya Beijing inakukaribisha!

Watu wengi wakiwemo wageni wamevutiwa na maumbo ya wanasesere hao wa baraka. Bibi Anna Allabert kutoka Russia alisema, "Ninawapenda sana wanasesere hao wa baraka, wanasesere hao ni wenye umaalum wa kichina, ninataka kununua wengi ili nikawape zawadi marafiki zangu."

Bibi Suenaga Yuki kutoka Japan pia alieleza furaha yake akisema, "Wanasesere hao wanapendeza sana kuliko nilivyotarajia, nitafurahi sana kama nitaweza kupata seti moja." Bibi Samantha Sowassey kutoka Canada anasema anapenda sana kurejea nyumbani kwao akiwa na zawadi ya wanasesere wa baraka. Alisema,

"Kuna vitu vitano vya baraka vya michezo ya Olimpiki ya Beijing, jambo hilo linanifurahisha sana, ninapenda mwanasesere mwenye sura ya panda, nitawapa zawadi watoto wa kaka yangu, nafikiri watafurahi sana."

Meneja wa duka moja linalouza bidhaa kuhusu michezo ya Olimpiki ya Beijing bibi Wang Xiaoyan alisema, hivi sasa kuna aina zaidi ya 300 za bidhaa zenye sura za wanasesere wa baraka zikiwa ni pamoja na skafu, fulana, vitu vinavyotumika madarasani na beji. Lakini watu wengi zaidi wanapenda wanasesere wanaotengenezwa kwa vitambaa vyenye manyoya. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kwamba siku hizi bidhaa hizo zinauzwa haraka sana. Aliongeza, "Hapo nyuma pato letu kutokana na mauzo lilikuwa kati ya Yuan elfu 10 na elfu 20 kwa siku. Tangu tuanze kuuza wanasesere wa baraka, pato letu limeongezeka kwa haraka na linakaribia Yuan milioni 10 katika muda wa karibu mwezi mmoja uliopita. Hivi sasa wateja wanaweza kununua vitu vilivyoko dukani wala siyo kununua vitu wanavyotaka wenyewe."

Kwa hivi sasa nchini China kuna maduka 28 yaliyopata leseni za kuuza bidhaa kuhusu michezo ya Olimpiki ya Beijing, licha ya hayo kuna vituo zaidi ya 160 vya muda vinavyouza vitu vya aina hiyo ambavyo viko katika baadhi ya miji mikubwa ikiwemo ya Beijing, Shanghai, Shenzhen, Qingdao, Nanjing na Chengdu.

Mjumbe wa kamati ya wataalamu wa uchumi kuhusu michezo ya Olimpiki ambaye ni profesa wa kitivo cha biashara cha chuo kikuu cha wananchi cha China Bw. Lu Dongbin anakadiria kuwa, pato kutokana na mauzo ya wanasesere wa baraka litazidi dola za kimarekani milioni 300. Alisema, "Nilipataje hesabu hiyo? Pato kutokana na mauzo ya vitu vya baraka na vya kumbukumbu vya michezo ya Olimpiki ya Sydney lilikuwa dola za kimarekani karibu milioni 300. Kutokana na hali ya hivi sasa ya China, idadi wageni kutoka nchi za nje itakuwa kubwa zaidi kuliko tulivyokadiria, idadi hiyo ikiunganishwa na idadi ya watalii wa nchini, mauzo ya bidhaa za michezo ya Olimpiki yatakuwa makubwa zaidi kuliko yale ya Sydney, kwa hiyo ninafikiri kuwa pato kutokana na mauzo ya vitu hivyo litazidi dola za kimarekani milioni 300."

Bw. Lu alifafanua kuwa makadirio hayo ni pato la mauzo ya bidhaa za wanasesere wa baraka peke yake, jumla ya mapato ya sekta zote zinazohusu wanasesere wa baraka itakuwa kubwa zaidi kuliko hesabu hiyo. Mwandishi wetu wa habari alitembelea kiwanda kimoja cha wanasesere wa baraka ambapo aliona mistari yote ya utengenezaji wa wanasesere ikifanya kazi kwa uwezo wake wote. Hata hivyo wanasesere wanaotengenezwa na kiwanda hicho bado hawawezi kutosheleza mahitaji ya watu. Mfanyakazi wa kiwanda hicho bibi Wang Hong alieleza sababu yake kuwa katika utengenezaji wa wanasesere, kukata kitambaa chenye manyoya kuna kazi ngumu, kushona, kujaza pamba, kazi ya kumalizia na kufunga. Kazi iliyo ngumu zaidi ni utengenezaji wa utosi wa mwanasesere. Alisema, "Kazi ya kutengeneza utosi wa mwanasesere Huan Huan ni ngumu zaidi, kwani utosi wake ni mfano wa moto, ni kazi kubwa kwelikweli, kila mfanyakazi wetu anaweza kutengeneza wanasesere 18 tu kwa siku."

Meneja wa kiwanda hicho hakudokeza idadi ya wanasesere wanaotengenezwa kwa siku pamoja na faida zao, lakini kutokana na hali ya pilikapilika ya kiwandani tunaweza kufahamu kuwa faida ya kiwanda siyo ndogo.

Mwandishi wetu wa habari aliambiwa kuwa kwenye soko la hisa za kampuni, vyeti vya hisa vinavyohusika na michezo ya Olimpiki siyo vinahusika na kampuni za ujenzi wa majumba na viwanja vya michezo vya Olimpiki pamoja na vifaa vya ujenzi peke yake, kampuni zote zinazopata leseni za uzalishaji wa bidhaa kuhusu wanasesere wa baraka na mauzo yake pia zinafuatiliwa na watu.

Ili kustawisha masoko ya bidhaa kuhusu wanasesere wa baraka, kamati ya uratibu wa michezo ya Olimpiki ya Beijing imechukua hatua za kisheria kulinda haki-miliki ya kielimu ya wanasesere wa baraka. Hivi sasa idara ya utekelezaji wa sheria nchini pia imezidisha adhabu kwa wale wanaohujumu haki-miliki ya kielimu ya wanasesere wa baraka ili kulinda maslahi ya soko la wanasesere wa baraka.

Idhaa ya Kiswahili 2005-12-20