Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-20 19:59:52    
Barua 1218

cri

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la posta Lindi Tanzania ametuletea barua mfululizo akisema kuwa, amepata barua tuliyomtumia pamoja na gazeti la China pictorial, ameambiwa kuwa ujumbe wa watu watano wa Radio China kimataifa ulitembelea Kenya, Tanzania na Zimbabwe. Mama Chen alikuwa Dar es Salaam na kutembelea Zanzibar na kuwa wageni wa sauti ya Tanzania Zanzibar. Mama Chen alidhani kuwa labda Bw Karim yupo Zanzibar na alikuja na zawadi maalum kwa ajili yangu. Kwa kuwa hakuweza kuonana nami, zawadi yangu alimwachia mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar.

Anasema yeye baada ya kupata barua kutoka kwetu nilifanya jitihada ya kumwandikia barua mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar na kuambatanisha barua yetu na kumtumia, jamaa yake aliyeko Zanzibar alikwenda kwa mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar alipeleka barua ili apokee zawadi yake. Anasema mara akiipokea atatujulisha. Ila anasikitika sana kwa kuwa hii ni mara ya pili, anashindwa kuonana na mama Chen, anasema anaomba samahani na sasa yeye yuko huko Lindi na ataendelea kuwepo huko Lindi. Ila anapenda kutoa shukurani zake za dhati kutokana na kumkumbuka na kwa zawadi hizo.

Na kwenye barua yake nyingine aliyotuandikia anasema, zawadi iliyoachwa na mama Chen kwa mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar imeshapokelewa na jamaa yake na anamtunzia, hana budi kwanza kumshukuru mama Chen kwa jitihada na usumbufu uliompata, na anamshukuru tena kwa kumkumbuka. Kwani mama Chen alisumbuka kumtafuta kwa njia ya simu, lakini kwa bahati mbaya yeye ndio yupo Lindi pia anashukuru kwa kupewa taarifa ya zawadi hiyo kuwa imepokelewa na mtu aliyekabidhiwa.

Hapa tunataka kumwambia kuwa, kutokana na juhudi za Bwana Karim katika kusikiliza matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa miaka mingi, tena kutokana na urafiki alioonesha mara kwa mara kwa wafanyakazi wa Radio China kimataifa, kwa mfano katika barua moja tuliyopokea kutoka kwake, Bwana Karim aliweka kahawa, akisema kama ilivyo watu wengi wa Mkoa wa Zhejiang, China wanapenda kunywa chai kijani, huko Tanzania wana kitu kinachoitwa kahawa nyeusi ya Kilimanjaro inayopendwa sana nchini na nje ya Tanzania, alitutumia kahawa hiyo kidogo tuionje na kukumbuka mlima Kilimanjaro, tulipoona kahawa na kusoma barua yake tulitiwa moyo sana, kweli kutokana na wasikilizaji wetu wengi wanapoonesha urafiki kati yao na Radio China kimataifa, ndipo tunapoongeza nguvu ya kuchapa kazi kwa ajili ya kuwatumikia vizuri zaidi, hivyo mama Chen alipata fursa ya kwenda Zanzibar, ingawa Zanzibar pia kuna wasikilizaji wengine, lakini alikuwa na shughuli nyingi, tena yeye na wenzake walikaa kwa siku mbili tu kisiwani Zanzibar. Alidhani kuwa akimpata Bwana Karim ataweza kukutana na wasikilizaji wengine, kwani kwenye daftari yake alipata simu ya Bwana Karim peke yake tu, namba za wengine alikuwa hazifahamu na angepata nafasi basi angekutana na wasikilizaji wengi. Anaomba radhi na anaona kuwa alichofanya kinastahili bila shukrani.

Na Bwana Karim anasema katika barua yake kuwa, atakuwepo Lindi kwa muda mrefu, kwa upande wa usikilizaji anaendelea kama kawaida yake, usikivu ni mzuri sana, lakini ombi lake maalum kuhusu kushiriki katika chemsha bongo ya mwaka huu, amewahi kusikiliza makala mbili tu ya kwanza na ya pili, makala ya tatu na nne hakupata kusikiliza kutokana na kufuatilia biashara katika wilaya mbalimbali huko mkoani Lindi, kwa hivyo anaomba kama itawezekana atumiwe makala ya tatu na nne kwa maandishi, ili aweze kushiriki bila kukosa toka aanze kusikiliza Radio China kimataifa zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Pia anaomba tumsaidie kumwambia Bwana Kassim Abeid Ngea anayekaa Lindi, kama yuko Lindi mjini anamwomba afanye mawasiliano naye kwa njia ya simu No. 0787.187195 ili waweze kujadiliana na kuongeza na kufanikisha usikilizaji wa Radio China kimataifa, yeye yupo mjini karibu kabisa na kituo cha mabasi yaendayo Dar es Salaam, atashukuru sana kama watasaidiana.

Tunatumai kuwa wasikilizaji wao wawili watawasiliana na kusaidiana. Lakini hata hivyo kwa sasa hata kama tutamtumia makala ya 3 na 4, hataweza kuwahi kutuletea majibu, akiweza kupata fursa ya kutembelea tovuti yetu kwenye mtandao wa Internet atasoma makala hizo nne, anuani yetu ni www.cri.cn, chagua Kiswahili hapo ataweza kusoma na kusikiliza vipindi vyetu mbalimbali, makala nne za chemsha bongo kuhusu Taiwan kisiwa cha hazina cha China zote zimewekwa kwenye kipindi cha sanduku la barua.

Msikilizaji wetu Martin Nyongesa Wafula wa sanduku la posta 127 Bungoma Kenya anasema katika barua yake kuwa, anatushukuru kwa ajili ya kumchagua mwenzao kutoka Bungoma Bwana Xaviel Telly Wambwa kuwa mshindi wa chemsha bongo ya mwaka uliopita, hakika amewaelezea mengi juu ya kukaa kwake mjini Beijing, ambayo ni mambo ya kustajaabisha hata hawataki amalize kuwaambia mambo mazuri kuhusu China. Anasema Bwana Wambwa amekuwa kivutio cha wengi hapo katika mkoa wao, na amemwabia ikiwezekana aandike kitabu juu ya safari yake nchini China. Kwa kweli China ni nchi ya kutamanika na wengi. Angependa kuchukua fursa hii kumshukuru Bwana Xavier Telly Wambwa pamoja na Radio China kimataifa CRI kwa ajili ya zawadi ya nguo pamoja na zawadi nyingine ambazo aliwaletea kutoka CRI, watu wengi wanashangaa sana kuona wakiwa wanavaa fulana za CRI wanawauliza maswali mengi sana, lakini majibu yote tu ni CRI. Kwa niaba ya wasikilizaji wa CRI wa Afrika mashariki, anatushukuru sana.

Kuhusu jarida la daraja la urafiki, anasema anaendelea kujifunza mengi ambayo hakuwa anafahamu hapo nyuma. Furaha yake kubwa ni kwamba hivi sasa amekuwa na picha za wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kama Mama Chem, Fadhili Mpunji na wengineo kwenye meza yake, hii inamfurahisha sana. Akifungua radio na kujua anayetangaza na anafanana na vipi, huwa anafurahi sana. Na amefurahishwa pia na ujumbe wa mkuu mpya wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gennian (msikilizaji wetu huyo alikosea kusema yeye ni mkuu wa idhaa ya Kiswahili) amejitolea na bila shaka ataboresha daraja la urafiki kati ya CRI na wasikilizaji wake. Anasema anatumai kuwa jarida letu ni bora na litaendelea kutolewa, na anachukua fursa hii kutukaribisha wafanyakazi wa CRI kutembelea mji wao Bungoma, Kenya, ambako anasema bila shaka tutajifunza mengi kwa maana mji huu uko karibu na mlima maarufu Elgon .

Na msikilizaji wetu Mogire O. Machuki wa kijiji cha Nyakware sanduku la posta 646 Kisii Kenya hivi karibuni ametuletea barua akisema, anaendelea kuchapa kazi kama kawaida, pia anaendelea kufurahia matangazo na vipindi vyetu vya radio kila mara, na kama alivyotuarifu kwenye barua zake za hapo awali ni kwamba anaendelea kufurahia tovuti ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Tovuti yenyewe ni bahari ya kujiongezea maarifa kuhusu taifa la watu wa China na uhusiano uliopo kati ya China na mataifa kadha wa kadha duniani kote.

Anasema anatushukuru kwa barua tuliyomwandikia hivi karibuni, na kumtumia bahasha zilizolipiwa gharama za stempu, na toleo la mwezi Novemba 2005 la jarida la China Today. Pokea zake za heri kwa kazi njema ya kudumisha mawasiliano. Anasema, ili Radio China kimataifa iwe kipenzi cha wengi, muhimu ni kuzidisha mawasiliano na wasikilizaji wake.

Bwana Machuki pia anasema katika barua yake kwamba anaiunga mkono ziara ya Rais Hu Jintao wa China huko Ujerumani, haswa wakati kama huu ambapo kuna mabadiliko ya utawala nchini Ujerumani. Akiwa huko jijini Bonn na Berlin Rais Hu Jintao alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Ujerumani na kufanya mkutano na chansela Angel Merkel wakizungumzia mambo kadha wa kadha kuhusu uhusiano kati ya China na Ujerumani, habari za kuvutia ni kwamba Ujerumani ilikubali kuiuzia China magari moshi 40 ya mwendo kasi. Anasema China ni taifa ambalo halijali rangi au taifa bali wachina wanapenda raia wote duniani waishi kama ndugu wa toka nitoke. Hii ndio sababu haswa China bara inapigania kurejesha kisiwa cha Taiwan. Taiwan ni sehemu moja ya China, sasa kuna haja gani Taiwan ijitenge? Imedhihirika wazi kwamba wakazi wa Taiwan asili yao ni China, na Je mbona wakazi wa Taiwan waishi maisha ya upweke hali wanatambulika huko China bara? Ni matumaini yake kuwa kutatokea siku njema ambapo kutakuwa na muungano wa China.

Anasema mwaka huu ndio unaelekea ukingoni na anaona kuwa mwaka huu wa 2005 umeenda vizuri sana, kwa sababu hivi sasa Radio China kimataifa imefanikisha ratiba mpya ya kutangaza vipindi vyake. Anasema ameridhika na mabadiliko haya mengi ambayo yalipendekezwa wakati ujumbe wa Radio China kimataifa ulipotembelea wasikilizaji wake huko Kisii Kenya mwaka 2003. Alipohutubia wasikilizaji wapenzi wa Radio China kimataifa kwenye semina hiyo tarehe 18 Septemba ,2003 katika hoteli Zonic hapo Kisii, mama Chen alifahamisha kwa kina jinsi Radio China kimataifa inavyojikakamua na kufikia hatua iliyo sasa hivi. Siku hiyo mama Chen pia aliwaarifu wasikilizaji kuwa yuko karibu kustaafu, aghalabu baada ya miaka miwili au mitatu hivi. Sasa miaka miwili ndio imeisha na hivi punde huenda sauti ya mama Chen itafifia kwenye mitambo ya Radio China kimataifa. Kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka miwili tangu ujumbe wa Radio China kimataifa kuzuru hapo Kisii, wasikilizaji walichangia hoja kwamba mchango wake kwa kuandaa vipindi bado unahitajika. Anasema Mama Chen ni kipenzi cha wasikilizaji wengi, ni mtangazaji ambaye wasikilizaji wamekuwa wakimthamini kwa miaka mingi sasa. Kwa mfano ziara ya mama Chen hapo Kisii Kenya mwaka 2003 na Nairobi Kenya 2005 na Dar es Salaam Tanzania iliifanya CRI iwe karibu na wasikilizaji wake, na ilidhihirisha kuwa mama Chen ni mtu wa watu. Anasema upendo walionao kwa mama Chen hajui atauelezea vipi, wamejawa na mawazo juu ya kustaafu kwa mama Chen.

Kuhusu suala hilo hapa tunapenda kumwambia Bwana Machuki kuwa, wiki zilizopita tumewaambia wasikilizaji wetu kuwa, mama Chen alipozungumzia hali ya idara ya Kiswahili aliwahi kusema kuwa, hivi sasa idara hiyo imekuwa na vijana wengi wapya, yeye karibu atastaafu, kwa kweli ifikapo mwishoni mwa mwaka 2006, mama Chen atastaafu rasmi, lakini kutokana na hali ya hivi sasa ya idara hii kuwa na vijana wengi na wafanyakazi wenye uzoefu ni wachache, vijana hao bado wanahitaji misaada. Hivyo baada ya kustaafu rasmi, mama Chen hakika ataendelea kufanya kazi katika idara hii na kuwasaidia vijana, anamshukuru sana Bwana Machuki kwa moyo wake wa udhati, asiwe na wasiwasi, mama Chen ataendelea kuchapa kazi kwa ajili ya kuongeza urafiki kati ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake.

Idhaa ya Kiswahili 2005-12-20