Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-21 16:02:24    
Dawa za makabila madogo madogo nchini China zina nafasi kubwa ya kuendelezwa

cri

Mganga mwenye umri wa miaka 73 wa kabila la Wamiao mkoani Guizhou, Bw. Xiong Anfu, ana matumaini ya miaka mingi, ya kuandika tiba zote za kienyeji anazozijua kwenye karatasi na kuzijulisha duniani.

Bw. Zhang Yi wa taasisi ya utafiti wa dawa za makabila madogo madogo katika Chuo Kikuu cha Mji wa Chengdu alisema, "Dawa za makabila madogo madogo zina nafasi kubwa ya kuendelezwa, hivi sasa dawa zilizopo za makabila hayo ni sehemu ndogo tu na zina nafasi kubwa kuendelezwa."

Kwa kufanya uchunguzi mara kadhaa, nchini China kuna dawa za makabila madogo madogo zaidi ya aina 8,000, kati ya dawa hizo, aina 1908 ni za kabila la Watibet, 1342 ni za kabila la Wamongolia, aina 600 ni za kabila la Wauygur na aina 500 ni za kabila la Wamiao. Kila kabila lina sifa zake za tiba kwa dawa zake tofauti na kabila lingine.

Bw. Zhang Yi alisema, dawa za makabila madogo madogo zina sifa zake katika tiba ya magonjwa sugu, kama vile ugonjwa kulemaa, kuvuja damu kichwani, donda ndugu tumboni, baridi yabisi, kifafa na kimeta, na baadhi yao zinaleta matokeo mazuri zaidi kuliko dawa za Kimagharibi.

Wazazi wa mganga Xiong Anfu walikuwa wakulima lakini ni waganga waliosifiwa kwa uhodari wa tiba, wao walikuwa hodari kwa kutibu uvimbe wa maini, shinikizo la damu na ugonjwa wa kisukari. Bw. Xiong Anfu ni mrithi wa kizazi cha tano, alianza kujifunza tiba alipokuwa na umri wa miaka 6 na hadi sasa ameponesha wagonjwa wengi wasiohesabika, amekusanya tiba za kienyeji kutoka kwa raia karibu elfu kumi na nyingi kati ya hizo zinatibu sana. Yeye mwenyewe alianzisha hospitali moja na kiwanda kidogo cha chakula cha kuongeza afya. Lakini haridhiki na hali hiyo, kwani watu wanaoomba dawa zake wanakuwa wengi siku hadi siku.

Kutokana na takwimu, hivi sasa dawa ambazo tayari zimetengenezwa za makabila madogo madogo zimefikia 600, na viwanda vya kutengenezea dawa hizo vimefikia 200, mapato ni kiasi cha yuan bilioni tano kwa mwaka. Wataalamu wanaona kuwa kwa ujumla dawa za makabila madogo madogo ni chache na zinahitaji kuendelezwa kwa ngazi ya juu zaidi na kwa teknolojia ya kisasa, nafasi ya kuendeleza dawa za makabila madogo madogo ni kubwa.

Naibu mkurugenzi wa Kamati ya Makabila Madogo Madogo ya China Bw. Yang Jianqiang alisema, dawa za makabila madogo madogo nyingi zaidi ni za kimaumbile na hazina madhara ya kikemikali, kwa hiyo zitakuwa na hali nzuri katika soko. Katika kipindi cha kutekeleza "Mpango wa 11 wa Miaka Mitano ya Maendeleo" serikali itahimiza zaidi mashirika ya kuzalisha bidhaa zinazohitajiwa na watu wa makabila madogo madogo zikiwemo dawa za makabila hayo, na itasaidia zaidi yale mashirika yanayozalisha bidhaa ambazo zinahitajiwa na watu wa makabila madogo madogo na pia kwa watu wengine.

Bw. Xiong Anfu alidokeza kuwa, hivi sasa kampuni moja ya Hong Kong inataka kushirikiana naye kwa kuwekeza yuan milioni 50 kwa lengo la kuendeleza dawa za shinikizo la damu na ugonjwa wa kisukari. Alisema, "Hivi sasa tunazungumza namna ya kushirikiana kwa hisa, kwa kuungwa mkono na sera za serikali, tuna uhakika wa kufanikisha utengenezaji wa dawa hizo za kabila la Wamiao."

Idhaa ya Kiswahili 2005-12-21