Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-21 20:00:10    
Hali ya lishe ya wakazi wa China

cri

Ripoti kuhusu hali ya lishe ya wakazi wa China iliyotolewa siku za karibuni na idara husika ya China imeonesha kuwa, kutokana na umaskini na kutopata mchaganyiko mzuri wa chakula, baadhi ya wanavijiji wa sehemu ya magahribi ya China hawapati lishe ya kutosha, ambapo wakazi wa miji na sehemu za pwani wanakabiliwa na tatizo linalotokana na kula vyakula vyingi kupita kiasi na vyakula wanavyokula havina mchanganyiko wa kutosha. Hali mbili zilizotajwa zote zitaleta athari mbaya kwa afya ya binadamu. Hivi sasa, wataalamu wametoa mapendekezo mengi kuhusu kuboresha hali ya lishe kwa wakazi wa China na serikali ya China imechukua hatua mbalimbali ili kila mwananchi awe na hali nzuri ya lishe.

Mtaalamu wa lishe wa China Bw. Jiang Jianping alisema kuwa, kutopata lishe ya kutosha na kula vyakula vyingi kupita kiasi, hali hizo mbili zote ni kutokuwa na hali nzuri ya lishe, hivi sasa hali hii inaleta athari mbaya kwa afya ya wakazi wa China.

"Magonjwa yanayotokana na kula vyakula vyingi kupita kiasi yanaongezeka, kama vile ugonjwa wa moyo unaohusiana na mshipa wa damu, shinikizo la damu la kupanda, kisukari, na unene kupita kiasi. Hivi sasa, idadi ya wagonjwa wa shinikizo la damu la kupanda imefikia milioni 160, na watu watatu kati ya kumi wana tatizo la kuwa na uzito kupita kiasi na tatizo la unene kupita kiasi; hali ya lishe ya watoto vilevile hairidhishi, kutokana na kuchagua kula vyakula wanavyopenda peke yake au kula kupita kiasi, watoto wengi zaidi wa mijini ambao ni mtoto pekee kwenye familia wananenepa sana, ambapo wanapatwa na magonjwa ya watu wazima wakiwa na umri mdogo.

Mtaalamu huyo amechambua chanzo cha hali hiyo akisema, vyakula wanavyokula wakazi wa China vingi ni mboga, wanakula kidogo, nyama ambazo zina virutubisho vingi vya madini, hali hii inawafanya baadhiya wakazi wa mijini na vijijini wakose madini ya Calcium, madini ya chuma, madini ya Zinki, Vitamin A na Vitamin B2. Kwa upande mwingine, hali ya kupika vyakula kupita kiasi inapunguza lishe iliyo ndani ya vyakula hivyo. Aidha, kutokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu lishe na kutojua kuchagua mchaganyiko mzuri wa vyakula ni sababu nyingine inayowafanya baadhi ya wakazi wa China kutokuwa na hali nzuri ya lishe.

Watu wazima kutokuwa na hali nzuri ya lishe kunaaathiri afya ya watoto wao moja kwa moja. Katika vijiji vya China, watoto wachanga ambao uzito wao haufikii uzito wa wastani ni asilimia 14, na hali yao ya lishe ni ya wasiwasi. Uchunguzi mmoja unaonesha kuwa , kati ya wanafunzi zaidi ya milioni 200 wa shule za msingi na za sekondari wa China, wawili kati ya watano wana upungufu wa madini ya Calcium, na watatu kati ya kumi wana upungufu wa damu kutokana na kukosa madini ya chuma. Katika sehemu maskini, baadhi ya vijana wanapatwa na ugonjwa wa kupungukiwa damu na kuwa na tatizo la kupinda mgongo.

Katika miaka 10 iliyopita, kutokana na juhudi za wataalamu wa lishe, harakati kadhaa zenye lengo la kuboresha hali ya lishe ya wanafunzi zinatekelezwa hapa China. Kwa mfano, katika harakati ya soya, serikali ilitenga fedha ili kumwezesha kila mwanafunzi wa sehemu maskini apate kikombe kimoja cha maziwa yaliyochanganywa na unga wa soya kila sika, hali kadhalika mpango wa maziwa, na mpango wa mchanganyiko mzuri wa vyakula. Mtaalamu Zhao Jianping akizungumzia harakati hizo alisema:

"Tukiangalia uzoefu wa nchi mbalimbali duniani katika jambo hilo, nchi hizo zinazingatia hali ya lishe ya watu tokea wakiwa watoto, baadhi ya nchi zimetekeleza mpango wa maziwa, nyingine zimetekeleza mpango wa mchanganyiko mzuri wa vyakula tangu nusu karne iliyopita, hata miaka 100 iliyopita. Hivi sasa, kiwango cha maisha ya wachina kimeinuka kidhahiri, uzalishaji mali kwa kila mwananchi umezidi dola za kimarekani 1000, huu ni wakati mwafaka kufanya kazi hiyo. Naona kuwa katika siku za usoni, serikali yetu inapaswa kujiongezea mwamko wa kuinua hali ya lishe ya wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari, na kuweka kazi hiyo kwenye mpango wake wa kazi."

Katika mwaka 2001, serikali ya China ilianzisha Kituo cha Maendeleo na Hali ya Lishe kwa Wananchi, ambacho kinashughulikia utekelezaji wa harakati za kuboresha hali ya lishe ya wananchi, zikiwemo kufanya utafiti wa sera na sheria husika, na kuwaelimisha wananchi kuhusu ujuzi husika na kutoa ushauri kwao. Ili kutatua tatizo la baadhi ya wakazi wa China kuwa na upungufu wa virutubisho vya lishe, kituo hicho kinatumia uzoefu wa nchi nyingine na kutumia ufumbuzi wa kuongeza virutubisho vya lishe ndani ya unga wa ngano, mchele, mafuta na vyakula vyingine, ili wakazi wa China waweze kupata virutubisho vya lishe za kutosha kutoka kwenye vyakula.

Katika mwaka 2002, Kituo cha Maendeleo na Hali ya Lishe ya Wananchi kilianzisha kazi ya majaribio katika mji wa Lanzhou, mkoani Gansu, kaskazini magharibi mwa China. Kituo hicho kiliweka madini ya chuma, madini ya Zink, Vitamin E na virutubisho vyingine vya lishe ndani ya unga wa ngano. Wakulima zaidi ya 1000 wanaoishi kwenye vitongoji vya mji wa Lanzhou wanakula unga wa ngano wa aina hiyo kwa hiari.

Mwanzoni, wakulima hao hawakugundua tofauti kati ya unga wa ngano wa aina hiyo na wa kawaida, kwani ladha yake haina tofauti. Lakini baada ya kula unga wa ngano wa aina hiyo kwa miaka mitatu, wakulima hao wanajisikia mabadiliko makubwa kwenye afya zao. Bi. Chen Guilan ni mmoja wa wakulima hao, akimwambia mwandishi wetu wa habari alisema:

"Nilikuwa naona mara kwa mara ukavu kwenye macho yangu, na midomo yangu ilikuwa inatokewa na vidonda mara kwa mara, na ngozi ya miguu na mikono ilikuwa inachubuka, na nilikuwa sina nguvu siku zote na nilikuwa napatwa na mafua. Baada ya kula unga wa ngano wa aina mpya, matatizo hayo yote yameondoka, sasa naona sina tatizo."

Kutokana na mabadiliko hayo makubwa yanayoletwa na unga wa ngano uliowekwa virutubisho, wakazi wengi zaidi wameanza kula unga wa ngano wa aina hiyo. Mtaalamu wa Kituo cha Maendeleo na Hali ya Lishe ya Wananchi Bw. Yu Xiaodong alifahamisha kuwa, unga wa ngano ni chakula muhimu kwa wakazi wa China, kutia virutubisho vya lishe kwenye unga wa ngano kutokana na mahitaji tofauti ya wakazi wa sehemu tofauti, ni njia rahisi na salama ya kuboresha hali ya lishe ya wananchi. Hivi sasa, unga wa ngano wa aina hiyo unauzwa katika miji na mikoa 19, na mchele uliowekwa virutubisho vya lishe utaanza kuuzwa katika siku za karibun. Habari zinasema kuwa pande husika zinaendelea kuweka virutubisho hivyo kwenye mafuta, chumvi na sosi, na kuwashawishi wakazi wa China wale vyakula hivyo na kupika kwa viungo hivyo.

Bw. Yu Xiaodong alisema kuwa serikali ingeonesha umuhimu mkubwa zaidi katika kuboresha hali ya lishe ya wananchi, akisema:

"Serikali yetu inakabiliwa na kazi mbili, ya kwanza ni kuweka virutubisho vya lishe kwenye vyakula mbalimbali, ya pili, kuwafuatilia zaidi wakazi wa sehemu maskini, kuweka mkazo katika kuboresha hali ya lishe ya watu hao, kuinua kiwango cha afya zao, ili wasiingie kwenye mzunguko mbaya wa "kuwa wagonjwa kutokana na umaskini, na kuwa maskini kutokana na kuugua".

Hivi sasa, kuwa na upungufu wa ujuzi wa lishe kwa watu wa China ni moja ya chanzo muhimu ya wakazi kutokuwa na hali nzuri ya lishe, ndiyo maana wataalam wametoa mwito wa kujenga mfumo wa kutoa ushauri wa kitaalamu, ili wakazi wa China waweze kupata ushauri wakati hali yao ya lishe inapokuwa mbaya, kama wanaweza kupata dawa wakati wanapougua.