Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-22 20:27:49    
Wachina wengi zaidi waanza kusherehekea sikukuu ya Krismas

cri

 

Krismas ni sikukuu inayosherehekewa zaidi katika nchi za magharibi, lakini katika miaka ya hivi karibuni, Wachina wengi zaidi pia wameanza kusherehekea sikukuu hiyo.

Bwana Liu Song mwenye umri wa miaka zaidi ya 30 ni mfanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza mabasi ya umeme cha Beijing, kabla ya wiki mbili zilizopita, alinunua mti wa Krismas na kuuwekea sebuleni na kuupamba kwa taa za rangi. Bw. Liu alisema, katika mkesha wa Krismas yeye na mke wake watakwenda mkahawa kula chakula cha kimagharibi. Akisema:

"Katika mkesha wa Krismas tutakwenda kula chakula cha kimagharibi kwenye mkahawa maarufu wa Maxim, halafu tutatembelea maduka yatakayofunguliwa usiku mzima."

Kama familia ya Bw. Liu Song, katika mji wa Beijing na sehemu nyingine nchini China, katika miaka ya hivi karibuni, familia nyingi zaidi na zaidi zinapanga kusherehekea sikukuu ya Krismas kwa ajili ya kujiburudisha.

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kuinuka kwa kiwango cha maisha, uwezo wa matumizi wa Wachina unaongezeka siku hadi siku, na kutokana na sera ya kufungua mlango kwa nchi za nje na kuimarika kwa maingiliano kati ya Wachina na watu wa nchi za nje, sikukuu ya Krismas imeanza kupokelewa na Wachina wengi zaidi, na usalama, utulivu na baraka zinazoonekana kwenye sikukuu ya Krismas zinaweza kukidhi matakwa na matarajio ya watu ya kuishi maisha mazuri.

Katika sikukuu ya Krismas watu hupeana zawadi, kufanya mikusanyiko au kuwaandalia marafiki na jamaa karamu. Lakini sherehe ya sikukuu ya Krismas nchini China ina umaalum wa kichina, watu wengi wanaifanya kama fursa mpya ya kukusanyika pamoja. Kwa mfano, vijana wengi wanasherehekea sikukuu ya Krismas kwa shangwe pamoja na wanafunzi wenzao na marafiki. Mwanafunzi wa kidato cha nne wa chuo kikuu cha viwanda cha Beifang cha Beijing Xu Mingze alisema:

"Mwaka huu nitashiriki kwenye tafrija ya dansi ya kuvaa kinyago cha usoni, ili kusherehekea sikukuu yangu ya mwisho ya Krismas katika maisha yangu ya chuoni kwa njia maalum."

Familia zenye watoto zinazingatia jinsi ya kuwafurahisha watoto wao katika sikukuu hiyo. Bi. Lu Xiaohui kutoka mji wa Shanghai ameomba mapema kushiriki kwenye shughuli za kusherehekea sikukuu hiyo zilizoandaliwa na kiwanda kimoja kinachotengeneza vyakula. Akisema:

"Kiwanda hicho cha vyakula kimeandaa shughuli za kusherehekea sikukuu ya Krismas, yaani wazazi waende na watoto wao kutengeneza keki kwa mikono yao wenyewe. Tunataka kushiriki kwenye shughuli hizo pamoja na mtoto wetu wa kiume mwenye umri wa miaka 6 ili tuburudike kwa pamoja."

Kama kiwanda hicho kilichofanya, maduka mengi nchini China yanatumia fursa hiyo kuandaa shughuli za aina mbalimbali za kusherehekea sikukuu ya Krismas ili kustawisha biashara. Maduka mengi yamebandika matangazo mapema kuhusu kufanya biashara usiku mzima, au kupunguza bei za bidhaa katika mkesha wa Krismas, mikahawa mikubwa pia imeandaa chakula maalum cha kusherehekea sikukuu ya Krismas. Katika mtaa maarufu wa kibiashara wa Wangfujian mjini Beijing, maduka makubwa kwa madogo yote yametundika mapambo yanayohusika na sikukuu ya Krismas. Mwuza duka Bw. Zeng Hua alisema:

"Mwaka huu duka letu limeandaa bidhaa aina mia moja hivi za Krismas, kama vile mzee Krismas na mbwa Krismas, ambazo zinapendwa sana na wateja."

Si kama tu wakazi wa mijini wanasherehekea sikukuu ya Krismas, wakulima wa sehemu mbalimbali nchini China pia wameanza kusherehekea sikukuu ya Krismas. Katika mkoa wa Heilongjian, kaskazini mashariki mwa China, hali ya hewa ni baridi sana, ardhi yote imefunikwa na theluji. Kwenye madirisha ya nyumba ya mkulima Wang Jiwen wa wilaya ya Tanyuan, zilibandikwa sanamu za mzee Krismas zilizokatwa kwa karatasi nyekundu. Mkulima Wang alisema kuwa, hivi sasa familia nyingi kwenye kijiji chake pia zinasherehekea sikukuu ya Krismas.

Baridi na theluji ni ishara moja ya sikukuu ya Krismas. Mwanzoni mwa mwezi Desemba, hali ya hewa katika sehemu nying nchini China ilianza kuwa baridi kwa ghafla. Katika upepo wenye baridi, mapambo ya Krismas yenye rangi mbalimbali yanametameta na kuwavutia sana wapita njia.