Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-26 15:29:11    
Heri ya Krismasi

cri

Tarehe 25 Desemba ni sikukuu ya Krismasi, katika kipindi hiki tumewaandalia nyimbo kadhaa za kusherehekea siku hiyo na kwa kutumia nafasi hii tunawatakia heri ya Krismasi.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo "Tunakutakia Heri ya Krismasi". Huu ni wimbo wa miaka mingi katika Uingereza, unaimbwa na Kwaya ya Wasichana Watakatifu wa Chuo Kikuu cha Sanaa cha Mji wa Nanjing. Kwaya hiyo ina waimbaji saba tu ambao wanaonekana kama malaika kwa sura na sauti zao tamu na nyororo, wimbo huo umeonesha jinsi watu wanavyofurahi wanaposherehekea sikukuu ya Krismasi. Wimbo unasema "Tunakutakia heri ya Krismasi, tunakutakia maendeleo katika mwaka mpya! Tugawie keki na kitafunwa cha tini na tukuambie habari njema. Tunakutakia heri ya Krismasi, tunakutakia furaha ya mwaka mpya!"

Watu wa Ulaya wanazichukua kuwa rangi nyekundu, kijani na nyeupe kuwa ni rangi za Krismasi. Siku ya Krismasi inapokaribia, nyumba zao hupambwa kwa rangi hizo. Rangi nyekundu ni maua na mishumaa, rangi ya kijani ni miti ya Krismasi ambayo huwa ni mivinje ikimaanisha maisha marefu. Miti hiyo hupambwa kwa maua, nyota na taa za kumetameta. Katika mkesha wa Krismasi watu wanaimbaimba na kuchezacheza pembezoni mwa mkrismasi. Baba Krismasi anayepambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe ni mtu anayekaribishwa zaidi katika pilikapilika za Krismasi. Watoto wanapokuwa kabla ya kulala huweka soksi zao kando na mito yao ya kulalia ili baba Krismasi akija awawekee zawadi ndani ya soksi. Sasa sikilizeni wimbo unaoimbwa na Yang Kun, "Mkesha wa Krismasi"

"If you were beside me, then I could here angels, and I'd give you rainbows for Christmas."

Miaka zaidi ya kumi iliyopita, vitu vya kusherehekea Krismasi vilikuwa vigeni kabisa kwa Wachina, lakini hivi sasa kutokana jinsi maingiliano ya utamaduni yanavyozidi kuimarika kati ya Mashariki na Magharibi Wachina wengi wanasherehekea sikukuu za Magharibi, vijana wengi wanafanya tafrija za aina mbalimbali za familia, wachumba au za marafiki katika mkesha Krismasi wakivaa kofia za aina mbalimbali za Krismasi wanaimba, wanacheza na wanaongea kwa furaha. Wazazi huwawekea soksi watoto wao kando ya mito yao ya kulalia na baada ya wao kushikwa na usingizi wazazi huwatilia zawadi na pipi ndani ya soksi hizo. Baadhi ya wazazi wazee huwatumia kadi za Krismasi marafiki zao na jamaa zao walioko mbali kuwatakia baraka.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo "Baba Krismasi Anakuja", ni wimbo ulioimbwa na mwimbaji mwanamke Chen Lin, unasema, "Baba Krismasi mwenye nyusi nyeupe, kofia nyekundu anarukaruka barabarani huku akipiga mluzi, taa za rangi zinametameta, na watu wanampigia vigelegele."

Kabla ya sikukuu ya Krismasi, nchini China mahoteli mengi hupambwa kwa mikrismasi na maduka makubwa yanauza vitu na zawadi za Krismasi, kama kofia za baba Krismasi, soksi za kuwekea zawadi, vitu vya kupamba mivinje, na wauzaji wengi pia wanapambwa kwa kofia nyekundu au kujipamba kama baba Krismasi kuwazawadia wateja zawadi ndogo.

Wasikilizaji wapendwa mliosikia ni muziki ulioimbwa na Bendi ya Maua na wimbo ulioimbwa ni "Usiku wa Amani". Wimbo huu unasema, "usiku mtulivu, usiku wa amani umefika, sauti tukufu zasikika nje ya madirisha, usiku mtulivu, kesho yote yatakuwa mapya, na matumaini hayatakuwa mbali, nyota zinametameta mbinguni, mwaka mpya utakuja mara baada ya usiku kupita, na maisha yatakuwa mapya."

Jingle Bells ni wimbo unaopendwa sana na Wachina, unawaletea furaha tele ya sikukuu, tukiwa tunakaribia mwisho wa kipindi hiki tunawakaribisha mburudike na wimbo huu ulioimbwa na kwaya ya Bata Mweusi.

Kwaya ya Bata Mweusi ina waimbaji wanawake watatu, sauti zao ni safi na nyororo. Wimbo unasema, "kwa kigari cha kuteleza kwenye theluji tunakimbia kwenye upepo wenye theluji, tunapita makonde, tunaimba na kucheka. Kengele zinalia zikichangia furaha!"

Idhaa ya kiswahili 2005-12-26