Maafa yaliyosababishwa na Tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 26 Desemba mwaka 2004 chini ya Bahari ya Hindi yalisababisha vifo vya watu karibu laki 2.3, ambapo idadi ya watu waliokumbwa na maafa ilifikia milioni 2.2, na hasara za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za kiuchumi za hazikuweza kuhesabiwa.
Mwaka mmoja umepita, wananchi wa sehemu zilizokumbwa na maafa wanafanya ukarabati kwa juhudi kubwa chini ya misaada ya serikali na jumuiya ya kimataifa. Lakini kutokana na makadirio ya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, sehemu zilizokumbwa na maafa hayo zinapaswa kufanya juhudi kwa miaka mitano hadi 10 ndipo zitakapoweza kufufua hali yao ya kabla ya maafa na kutimiza maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Nchi zilizokumbwa na maafa zote ni nchi zinazoendelea, hivyo ukarabati wa nchi hizo baada ya maafa unahitaji ushirikiano wenye juhudi kubwa wa jumuiya ya kimataifa, ama sivyo kucheleweshwa kwa kazi ya ukarabati kutaathiri vibaya sana maendeleo ya jamii ya binadamu.
Katika mwaka mmoja uliopita, jumuiya ya kimataifa imetoa misaada ya hali na mali kwa ajili ya ukarabati wa sehemu zilizokumbwa na maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea chini ya bahari ya Hindi. Shirika la hali ya hewa la dunia tarehe 23 mwezi huu lilidokeza kuwa, mfumo wa kutoa tahadhari kuhusu maafa ya tsunami kwenye Bahari ya Hindi unajengwa kwa utaratibu, na unatazamiwa kuzinduliwa katikati ya mwaka 2006. Baada ya kuzinduliwa, mfumo huo utahakikisha idara za huduma za hali ya hewa za nchi zote zilizoko kwenye sehemu hiyo zinapata habari na tahadhari kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya dakika 2.
Ingawa jumuiya ya kimataifa imefanya juhudi kubwa, lakini hali ya hivi sasa ya sehemu zilizokumbwa na maafa ya tsunami bado haifurahishi, mchakato wa ukarabati baada ya maafa bado unakabiliwa na taabu kubwa.
Ofisa wa kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa alidokeza, watu wengi walionusurika katika maafa, hivi sasa hata hali yao ya makazi ni chini ya kigezo cha kimataifa kilichowekwa kuhusu haki za binadamu, aidha haki za wanawake na watoto wa sehemu zilizokumbwa na maafa hazijaweza kuhakikishwa ipasavyo.
Ingawa nchi nyingi zina nia na maoni ya pamoja kuhusu kuzisaidia sehemu zilizokumbwa na maafa katika ukarabati, lakini kutokana na sababu mbalimbali, mapendekezo mengi mazuri bado hayajaweza kutekelezwa.
Kutokana na takwimu zisizokamilika, jumuiya ya kimataifa iliahidi kutoa michango ya dola za kimarekani bilioni 5 kwa nchi zilizokumbwa na maafa ya tsunami, na nchi na jumuiya nyingi pia zimeahidi kupunguza au kufuta madeni yanayodaiwa kwa nchi zilizokumbwa na maafa. Lakini mpaka sasa misaada mingi bado haijatolewa. Katibu mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa Jacques Diouf hivi karibuni alisema, kutokana na kucheleweshwa kwa utoaji wa misaada ya fedha na teknolojia kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, wakazi wa sehemu zilizokumbwa na maafa hawajaweza kupata misaada kwa wakati. Alisisitiza nchi mbalimbali zinapaswa kuanzisha mfuko wa akiba ya fedha ili kukabiliana na maafa ya dharura.
Maafa yaliyotokea katika sehemu za Bahari ya Hindi si kama tu yametoa onyo kwa binadamu wote kuwa, ni lazima kuheshimu dunia ya maumbile na kuthamini dunia, ili kushinda maafa ya kimaumbile. Binadamu wote wakifanya juhudi kwa pamoja ndipo dunia itakapoweza kusonga mbele kwa mwelekeo wa masikilizano zaidi.
|