Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-27 14:25:21    
China yawa mwanachama muhimu wa WTO

cri

Mkutano wa 6 wa mawaziri wa Shirika la Biashara Duniani, WTO ulifungwa tarehe 18 huko Hong Kong. Mkutano huo umepata baadhi ya maendeleo katika masuala ya kilimo, uidhinishaji wa ombi la kuingia sokoni kwa mazao yasiyo ya kilimo na suala la maendeleo. China ilishiriki mazungumzo mbalimbali ikitaka biashara ifanyike kwa haki na usawa. Maofisa husika wamesema, katika muda wa zaidi ya miaka 4 tangu China ijiunge na WTO, China imepata uzoefu katika mazungumzo ya biashara ya pande nyingi, na inatekeleza ahadi ilizotoa, kufungua masoko ya nchini na kuwa mwanachama muhimu wa WTO.

Alipozungumzia ujumbe China kwenye mkutano wa Hong Kong, katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy alisema, China ilionesha uhodari mkubwa katika mazungumzo ya biashara ya pande nyingi.

"China ni hodari sana katika mazungumzo ya biashara. Mbinu ya mazungumzo toka zamani ni aina moja ya sanaa katika China."

Ikiwa nchi mwenyeji wa mazungumzo, China ilitaka kuzingatia zaidi maslahi ya nchi zinazoendelea. Kwenye mazungumzo ya Hong Kong ujumbe wa China ulitoa wito wa kusamehe ushuru wa forodha, kuondoa viwango vya biashara na kuruhusu mazao yote ya nchi 49 zilizo nyuma kabisa kimaendeleo, na kuzipa nchi zote wanachama wa WTO haki maalumu.

Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai alipozungumzia maoni ya China alisema,

"Jambo muhimu katika mchakato wa utandawazi wa biashara duniani ni kuzingatia nchi zilizo nyingi, kuziwezesha nchi wanachama zinazoendelea zifuatane na hatua za maendeleo, hivyo zinatakiwa kupewa kipaumbele na kutendewa tofauti na kujitahidi kuafikiana kuhusu baadhi ya masuala likiwemo la pamba katika mazungumzo ya Hong Kong, ili kuzifanya nchi wanachama zinazoendelea zinufaike kihalisi na kuimarisha imani yao kuhusu mazungumzo ya duru la Doha.."

Maoni ya China ni habari nzuri kwa wakulima maskini wa nchi wanachama zinazoendelea. China ni sawasawa na nchi nyingi zinazoendelea ambazo zina tofauti kubwa kati ya sehemu na sehemu na kati ya sekta na sekta, wastani wa pato la China kwa kila mtu ni kiasi cha dola za kimarekani 1,400 na iko katika kiwango cha chini. Aidha, idadi kubwa ya watu nchini China ni wakulima, na idadi ya watu maskini wanaoishi chini ya kiwango cha dola moja kwa siku ni zaidi ya milioni 200. Bw. Bo Xilai alisema, ingawa China ina shida nyingi, lakini inakubali kutoa mchango kwa dunia. Mwaka huu, China itaagiza bidhaa kutoka nchi za nje zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 600 na kuanzisha soko jipya na kubwa kwa dunia. Serikali ya China ilitangaza kusamehe madeni ya nchi maskini zinazodaiwa nayo ya kabla ya mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kutokana na kuwa China inaathiriwa vibaya na vizuizi vya biashara duniani, hivyo kwenye mkutano wa Hong Kong China ilihimiza nchi wanachama wa WTO zitambua hadhi yake kamili ya uchumi wa soko huria, kuunga mkono kuchambua na kurekebisha hatua zinazochukuliwa hivi sasa za kupinga kuuza bidhaa kwa bei ya chini sana, ili kuzuia kuchukua ovyo hatua za aina hiyo, kuongeza uwazi na kupinga mwelekeo wa baadhi ya nchi zilizoendelea kuweka vizuizi vya aina mpya katika mambo ya biashara.

Naibu kiongozi wa idara ya utafiti wa uchumi na siasa ya kimataifa ya taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bw. Li Xiangyang alichambua kuwa China kueleza msimamo wake kwenye mkutano wa Hong Kong inamaanisha kwamba inashiriki kwa juhudi kwenye mazungumzo ya biashara ya pande nyingi.

"Msimamo wa China ulioelezwa kwenye mkutano wa Hong Kong ni wa kufuatilia maendeleo. Kwa upande mmoja mapendekezo mengi iliyotoa China yanawakilisha matakwa ya nchi nyingi wanachama zinazoendelea. Kwa mfano, uhimizaji wa biashara huria ya mazao ya kilimo, kuzipa nchi zinazoendelea haki maalumu na kuhimiza nchi zilizoendelea kufungua masoko ya mazao yasiyo ya kilimo. Kwa upande mwingine, China ilitoa baadhi ya mapendekezo kwa ajili ya maslahi yake yenyewe, kwa mfano inataka nchi wanachama wa WTO zitambue haraka iwezekanavyo hadhi yake ya uchumi wa soko huria, na kuipa haki maalumu ya nchi mwanachama mpya wa WTO, hali ambayo inaonesha kukomaa kwa ustadi wa kushiriki kwenye mazungumzo ya biashara ya pande nyingi kwa China."

Licha ya kushiriki kwa juhudi kwenye utungaji wa kanuni za biashara ya kimataifa, China pia inatekeleza kwa makini ahadi ilizotoa wakati ilipojiunga na WTO. Katika miaka 4 iliyopita, China ilipunguza kwa mara 4 ushuru wa forodha ambao hivi sasa umepungua hadi 9.9% kutoka kiwango cha 15.3% kabla ya kujiunga na WTO.

Kupungua kwa kiwango kikubwa kwa ushuru wa forodha, kumehimiza uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje kuongezeka kwa karibu 30% kila mwaka, lakini gharama ndogo ya nguvukazi na muundo wa uzalishaji wa bidhaa za kiwango cha wastani na cha chini, vimeleta mikwaruzano mingi katika shughuli za biashara. Mwaka huu, Umoja wa Ulaya na Marekani ziliamua kuweka tena viwango vya usafirishaji wa bidhaa za nguo zinazotoka China. Ingawa China inakabiliwa hali mbaya, lakini iliendelea kuwa na mazungumzo na Umoja wa Ulaya na Marekani kwa kufuata maagizo husika ya WTO, na kuinua kiwango cha ushuru wa forodha kwa bidhaa za nguo zinazosafirishwa kwa nchi za nje. Mwakilishi wa kwanza wa Benki ya Dunia aliyeko hapa Beijing Bw. Bert Hofman aliipongeza China kwa kufuata barabara kanuni za WTO, alisema "Katika miaka kadhaa iliyopita, vitendo vilivyofanywa na serikali ya China katika upande huo ni vya kupendeza, wakati ilipotokea migogoro, China ilijitahidi kutenda vitendo kwa kufuata maagizo husika ya WTO, ingawa mara nyingi China iliingia katika hasara."

Katika upande wa kufungua masoko, China pia ilifanya vizuri. Hivi sasa kampuni za nchi za nje zinaruhusiwa kuanzisha kampuni za ubia nchini China katika sekta za mawasiliano ya habari na bima. Katika sekta ya benki, ambayo inafuatiliwa zaidi, hivi sasa benki za kigeni zinaruhusiwa kuanzisha shughuli kuhusu fedha za Renminbi kwa viwanda na kampuni katika miji 25 ya China, ambapo hatua za mchakato zimekuwa haraka zaidi kuliko ahadi iliyotoa China. Mbali na shughuli za benki za kigeni ambazo zinaongezeka kwa kasi ya 30% kwa mwaka, mashirika 18 ya nchi za nje yamekuwa na hisa katika benki 16 za China, zikiwemo benki mbili za biashara za serikali, na jumla ya uwekezaji ni dola za kimarekani karibu bilioni 13. Kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa, ifikapo mwishoni mwa mwaka 2006, China itafungua kabisa soko la sekta ya benki.

Hata hivyo, jumuiya ya kimataifa imekosoa baadhi ya upungufu wa China katika miaka minne iliyopita tangu ijiunge na WTO, hususan kuhusu hifadhi ya haki-miliki ya kielimu. Kamati ya biashara ya Marekani na China pamoja na jumuiya ya biashara ya Umoja wa Ulaya zinaona kuwa, China bado ni dhaifu katika hifadhi ya haki-miliki ya kielimu, tena inakosa uwazi. Hivi sasa China imeanzisha kwa hatua ya mwanzo mfumo wa sheria unaoendana na kanuni za kimataifa kuhusu haki-miliki ya kielimu, na kushirikiana na mashirika yote ya kimataifa ya kulinda haki-miliki ya kielimu.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-27