Mazungumzo kati ya Iran na nchi tatu zinazouwakilisha Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kuhusu suala la nyuklia yataanza tena mwezi Januari mwakani. Magazeti ya Ulaya yanaona kuwa kutokana na hali ilivyo sasa, inaonesha kuwa mazungumzo hayo hayatakuwa na matumaini makubwa.
Ofisa wa Russia mjini Tehran tarehe 26 alisema kuwa Russia inasubiri jibu la Iran kuhusu kuhamishia shughuli za kusafisha uranium nchini Russia. Kutokana na maneno aliyosema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bw. Hamid-reza Asefi kukataa kukiri kuwa Iran iliwahi kupata pendekezo la Russia la kuhamisha shughuli za kusafisha uranium nchini Russia, kwenye mkutano na waandishi wa habari ofisa huyo wa Russia alisema kuwa, Russia kweli imekabidhi waraka wake kwa Iran, waraka huo unasisitiza kuwa pendekezo lililotolewa na Russia la kuanzisha shirika la kusafisha uranium kwa ushirikiano kati ya Russia na Iran linaendelea kuwa na kazi yake.
Bw. Asefi alipokataa kukiri kupata pendekezo la Russia alisema, kwa vyovyote vile, Iran itakubali tu mapendekezo ya haki, nayo ni kuruhusu Iran ishughulikie kazi ya kusafisha uranium Iran.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki tarehe 26 alisema, Iran inapenda kushauriana na nchi yoyote kuhusu suala la nyuklia, lakini hii haimaanishi kuwa Iran ni lazima ipate ruhusa ya watu wengine katika utafiti wa teknolojia ya uranium. Alisisitiza kuwa Iran haiwezi kukubali sera ya ubaguzi.
Mazungumzo kati ya Iran na Umoja wa Ulaya yalisimama mwezi Agosti kutokana na Iran kurejesha shughuli za kusafisha uranium. Lakini baada ya kutafakari pande mbili za maslahi na hasara Umoja wa Ulaya haukuomba mkutano wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa uliofanyika mwezi Septemba uwasilishe suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Uslama, ili kurejesha tena mazungumzo hapo baadaye. Mwishoni mwa mwezi Novemba kutokana na kuhimizwa na Umoja wa Ulaya na Marekani, mkutano wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa uliamua kutowasilisha kwa muda suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Uslama, mkutano huo ulitumai kuwa Umoja wa Ulaya na Iran zingefanya mazungumzo kuhusu pendekezo la Russia la kuhamisha shughuli za kusafisha uranium nchini Russia, lakini pendekezo hilo lilikataliwa na Iran.
Wachambuzi wanaona kuwa hivi sasa misimamo ya Umoja wa Ulaya na Iran imebadilika kidogo ikilinganishwa na ya zamani, kwamba Iran siku zote inashikilia haki yake ya kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani na kutokana na hali inavyobadilika hivi sasa Iran inasisitiza haki yake ya kuendeleza teknolojia hiyo nchini mwake. Lengo la kushiriki kwenye mazungumzo yatakayorudishwa ni "kutapa imani ya jumuyia ya kimataifa kuhusu shughuli zake za kusafisha uranium nchini Iran". Msimamo wa Umoja wa Ulaya umelegezwa kidogo, kwamba ulikuwa ukitetea kutoruhusu Iran kugusa shughuli zote za kusafisha uranium lakini sasa umekubali kimya Iran ishughulikie kazi ya kusafisha uranium kwenye ngazi ya chini.
Vyombo vya habari vya Ulaya vinachambua kwamba ugumu wa msimamo wa Irani unatokana na uungaji mkono wa wananchi wake na kuona kuwa Iran ni moja ya nchi zilizosaini "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia", kwa hiyo kutumia nishati ya nyuklia kwa ajili ya amani ni haki yake kisheria. Pili, Marekani imezama ndani ya matope ya Iraq na Afghanistan, na suala la nyuklia la penisula la Korea, na Iran ni nchi ya pili ya kuzalisha mafuta kwa wingi duniani, katika wakati ambapo bei ya mafuta imekuwa ikipanda bila kushuka, nchi za Magharibi hata zikiiwekea vikwazo Iran hazitaungwa mkono na nchi nyingine za Magharibi, achilia mbali kutumia nguvu za kijeshi.
Baadhi ya magazeti ya Ulaya yanasema kuwa kama mazungumzo yatakayofanyika hayatafikia makubaliano, yumkini nchi tatu za Umoja wa Ulaya na Marekani zitaiwekea Iran tarehe ya mwisho ya kutatua suala la nyuklia la Iran.
Idhaa ya kiswahili 2005-12-27
|